Alhamisi, 26 Juni 2014

Bodi Mpya ya Huduma za Maktaba yazinduliwa

Mgeni Rasmi Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Consolata Mgimba akikabidhi zana za kazi kwa Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Huduma za Maktaba nchini Lambetha Mahai wakati wa kuzindua bodi hiyo.



Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Huduma za Maktaba nchini Dkt Alli Mcharazo akitoa maelezo kwa Mgeni rasmi Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Consolata Mgimba kuhusu kazi mbalimbali zinazofanywa na bodi hiyo









TAARIFA ZA UZUSHI KUHUSU WAZIRI WA ELIMU

Taarifa za uzushi zilizojitokeza jana katika baadhi ya mitandao ya kijamii kuwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mhe. Dkt. Shukuru Kawambwa amepata ajali na kufariki akiwa safarini kuelekea Mwanza hazifai na zinaleta usumbufu kwa watumishi, familia na jamii kwa ujumla .

Tunaomba watu wanaoeneza taarifa za kizushi za aina hii waache kufanya hivyo ili kuepusha usumbufu unaojitokeza.

Jumatatu, 23 Juni 2014

CHINA KUFADHILI WANAFUNZI WA ELIMU YA UFUNDI NCHINI

Mjumbe wa Baraza la Ushauri wa Kisiasa la China (Chinese Peoples Political Consultative Conference – CPPCC) Dkt. Annie Wu amesema kuwa atatoa ufadhili wa nafasi za masomo kwa wanafunzi wa Kitanzania kwenda kusoma elimu ya ufundi nchini China kwa lengo la kukuza na kudumisha  mahusiano mazuri yaliyopo kati ya Tanzania na China.
Dkt. Wu amekuja nchini kwa mwaliko rasmi wa Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo amefanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome ofisini kwake na kusema kuwa anatimiza ahadi yake aliyotoa awali ya kusaidia kuinua Elimu ya Ufundi nchini.
 Dkt. Wu alitoa ahadi ya ufadhili wa nafasi za masomo kwa wanafunzi wa Kitanzania kwenda kusoma elimu ya ufundi nchini China wakati Profesa Mchome alipofanya ziara ya kikazi mwezi huu nchini China na kukutana na kufanya mazungumzo na vingozi mbalimbali  wa nchi hiyo wa namna ya kuimarisha uhusiano uliopo kati ya Tanzania na China katika masuala ya elimu.
Kutokana na ufadhili huo uliotolewa na Dkt. Wu, Profesa Mchome amesema ufadhili huo umekuja wakati muafaka ambapo Serikali inaimarisha elimu ya Ufundi ili kuwaandaa vijana katika kujiajiri wenyewe pindi wanapomaliza masomo yao ya ufundi.

“Ni wakati sasa vijana wachangamkie fursa hii, wasome masomo ya Ufundi  ili wapate ufadhili na hatimaye wanapomaliza masomo yao waweze kujiajiri badala ya kusubiri kuajiriwa” Alisema Profesa Mchome. 

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi Dkt. Primus Nkwera amepokea ufadhili huo kwa furaha na kuwataka wanafunzi kuchangamkia nafasi hizo zitakapotangazwa. 
“Dkt. Wu ni mmoja kati ya marafiki wa Tanzania ambao wanakuja mara kwa mara  nchini na kuhamasika na  kujali Elimu ya Ufundi, wengi wao hutoa vipaumbele katika elimu Msingi na Elimu ya Juu,” anasema Dkt. Nkwera, anaendelea kusema pia ”Mahusiano ya Tanzania na China yametimiza miaka 50 hivyo kuja kwake kunaonyesha urafiki wa kweli tulio nao kati ya Tanzania na China”.
Pamoja na kushika nafasi za juu katika Baraza la Ushauri wa Kisiasa la China Dkt. Annie Wu ni mfanyabiashara ambaye amesaidia kuanzishwa kwa Jumba la Sanaa (Culture House) lililoko Beijing ambalo pamoja na mambo mengine jumba hilo linatumika kuuza vinyago kutoka kwa Wafanyabiashara wa Tanzania.
Kuanzia Jumatatu wiki Hii Tanzania itapokea ugeni kutoka nchini China utakaoongozwa na Makamu wa Rais wa Nchi hiyo ambapo mambo mbalimbali yanayozihusu nchi hizi mbili yatajadiliwa


Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Profesa Sifuni Mchome (katikati)akikabidhi zawadi ya kinyago kwa Mjumbe wa Baraza la Ushauri wa Kisiasa la China (Chinese Peoples Political Consultative Conference – CPPCC) Dkt. Annie Wu

Alhamisi, 12 Juni 2014

Waziri Kawambwa Afunga Mafunzo ya Maafisa Elimu Kuhusu Kukabiliana na Majanga Katika Taasisi za Elimu

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dkt. Shukuru Jumanne Kawambwa, Mwishoni mwa Wiki amefunga Mafunzo ya Kuwajengea Uwezo Maafisa Elimu Vifaa na Takwimu (SLOs) na Maafisa Elimu Taaluma (DAOs) (Msingi Na Sekondari) Tanzania Bara Kuhusu Kukabiliana na Majanga Katika Taasisi za Elimu, Yaliyofanyika ADEM - Bagamoyo Kuanzia tarehe 19/05/2014  hadi  06/06/2014.

Mafunzo haya yalishirikisha jumla ya Maafisa Elimu Vifaa na Takwimu na Maafisa Elimu Taaluma (Msingi na Sekondari) wapatao 636 kutoka Tanzania Bara. Maafisa hawa wanahusika moja kwa moja katika kusimamia utekelezaji wa utoaji Elimu bora nchini katika ngazi ya halmashauri chini ya mkakati mpya wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now) katika sekta ya elimu.
Mafunzo haya yatawawezesha kusimamia utoaji wa elimu bora shuleni na pia kutumia mbinu mbalimbali walizojifunza katika kuzuia na kukabiliana na majanga yanapotokea katika maeneo yao. Maafisa hao wataweza kutoa elimu kuhusu majanga kwa walimu, wanafunzi, viongozi na wadau wote wa elimu katika halmashauri zenu. Aidha, Elimu waliyoipata itawawezesha pia kuwa na uwezo wa kusimamia, kufuatilia na kuimarisha miundombinu shuleni na kuchukua hatua za tahadhari zitakayowezesha kukabiliana na majanga, mbalimbali kama vile umuhimu wa milango ya majengo ya shule kufungukia nje, kuwa na vifaa vya kuzima moto na kuwa na visanduku vya huduma ya kwanza.
Shule zetu zimekuwa zikikumbwa na majanga mbalimbali kwa mfano moto, mafuriko na vimbunga. Majanga haya yameleta athari kubwa kwa maisha ya walimu na wanafunzi, katika majengo yakiwemo madarasa, nyumba za walimu, maabara na vyoo.  Samani za shule, vifaa vya kufundishia na kujifunzia, barabara, huduma za maji na umeme, viwanja vya michezo na mazingira yote ya shule yamekuwa yakiharibiwa na majanga. Imeshuhudiwa moto ukiteketeza shule za Sekondari za Shauritanga, Idodi, Morogoro n.k na kusababisha vifo kwa wanafunzi na kuharibika kwa miundo mbinu ya shule. Pia tumeshuhudia mafuriko yakisababisha kutoendelea kwa masomo katika Wilaya za Kilosa, Kyela, Ilala, Mvomero n.k mafuriko haya yalisababisha shughuli za shule kukwama.
Serikali inaamini kuwa baada ya mafunzo haya, washiriki wataweza kutimiza majukumu haya mapya kama ifuatavyo:
  •  kuunda Kamati za kukabiliana na Majanga Shuleni;
  • kuandaa mipango kazi ya kukabiliana na majanga katika ngazi ya halmashauri na shule;
  • kuboresha miundombinu ya shule ikiwemo milango kufungikia nje, kuweka vizima moto (fire extinguishers), ndoo za michanga na kuboresha mazingira ya shule;
  • kujenga uelewa wa pamoja wa namna ya kukabiliana na majanga miongoni mwa walimu, wanafunzi na jumuiya inayozunguka shule
  •  kujenga mtandao (network) wa kukabiliana na majanga kati ya shule na jumuiya inayozunguka shule;
  • kufanya ufuatiliaji na tathmini kuhusu majanga shuleni; nakuandika taarifa sahihi kuhusu uwezekano wa kutokea majanga na madhara ya majanga shuleni mara yanapotokea.


Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dkt. Shukuru Kawambwa akimtunuku Cheti mmoja wa Wahitimu wa Mafunzo ya Kuwajengea Uwezo Maafisa Elimu Vifaa na Takwimu (SLOs) na Maafisa Elimu Taaluma (DAOs) (Msingi Na Sekondari) Tanzania Bara Kuhusu Kukabiliana na Majanga Katika Taasisi za Elimu

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dkt. Shukuru Kawambwa akitoa hotuba ya kufunga Mafunzo ya Kuwajengea Uwezo Maafisa Elimu Vifaa na Takwimu (SLOs) na Maafisa Elimu Taaluma (DAOs) (Msingi Na Sekondari) Tanzania Bara Kuhusu Kukabiliana na Majanga Katika Taasisi za Elimu;



Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dkt. Shukuru Kawambwa akimtunuku Cheti mmoja wa Wahitimu wa Mafunzo ya Kuwajengea Uwezo Maafisa Elimu Vifaa na Takwimu (SLOs) na Maafisa Elimu Taaluma (DAOs) (Msingi Na Sekondari) Tanzania Bara Kuhusu Kukabiliana na Majanga Katika Taasisi za Elimu;


Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dkt. Shukuru Kawambwa akimtunuku Cheti mmoja wa Wahitimu wa Mafunzo ya Kuwajengea Uwezo Maafisa Elimu Vifaa na Takwimu (SLOs) na Maafisa Elimu Taaluma (DAOs) (Msingi Na Sekondari) Tanzania Bara Kuhusu Kukabiliana na Majanga Katika Taasisi za Elimu
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dkt. Shukuru Kawambwa (mwenye suti nyeusi katikati)  akiwa katika picha ya pamoja na Wahitimu wa Mafunzo ya Kuwajengea Uwezo Maafisa Elimu Vifaa na Takwimu (SLOs) na Maafisa Elimu Taaluma (DAOs) (Msingi Na Sekondari) Tanzania Bara Kuhusu Kukabiliana na Majanga Katika Taasisi za Elimu