Jumatano, 20 Agosti 2014

Benki ya Dunia Kusaidia Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa Katika Sekta ya Elimu

Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia wamesaini makubaliano ya mkopo wa Shilingi bilioni 203 za Kitanzania (Dola za Marekani milioni 122) kwa ajili ya   kusaidia, kukuza na kuendeleza Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) katika sekta ya Elimu wenye lengo la kuimarisha na kuboresha elimu ya msingi na sekondari.
Makubaliano hayo yalitiwa saini na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Dkt. Servacius Likwelile  kwa niaba ya Serikali na Benki ya Dunia iliwakilishwa na Mkurungezi Mkazi wa Benki hiyo nchini, Philippe Dongie. Makubaliano hayo yamefanyika leo jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi Dkt. Servacius Likwelile  amesema  fedha zilizopatikana zitasaidia Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa katika Elimu kuboresha ubora wa Elimu ya Msingi na Sekondari.
Aidha, Dkt. Likwelile alisema Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa katika Elimu umelenga pamoja na masuala mengine Kuimarisha ufaulu na kuboresha uwazi shuleni kwa kupitia upangaji wa shule kitaifa kwa kuzingatia matokeo ya mitihani kwa shule za msingi na sekondari kwa kuzingatia ubora wa ufaulu na kutekeleza upimaji wa ujuzi wa stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa darasa la pili katika shule zilizochaguliwa.
Mpango huo pia umelenga kutoa  motisha kwa shule zote za Msingi na Sekondari zilizoonyesha maendeleo katika  ufaulu na zilizofanya vizuri ili kuboresha  viwango vya ufaulu na kutoa motisha zisizo za kifedha na kuondoa madai ya muda mrefu ya walimu  wa shule za Msingi na Sekondari ili Kuondoa malalamiko ya walimu hao.

Aidha, Dkt. Likwelile alisema Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa umelenga kuzisaidia shule na kuondoa ugawaji wa rasilimali usiozingatia usawa kwa kutengeneza na kusambaza vifaa vya kujifunzia kwa vitendo kwa shule za Msingi na Sekondari, kuandaa Mafunzo ya KKK kwa walimu wa shule za Msingi, utekelezaji wa  programu ya kujenga uwezo wa walimu na wanafunzi  katika ufundishaji na Ujifunzaji na kuboresha mfumo wa ufuatiliaji wa Ruzuku za Uendeshaji wa Shule.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwakilishi wa Benki ya Dunia aliipongeza Tanzania kwa kupata mkopo huo na kuitaka Serikali kutumia vizuri fedha ilizozipata  kama ilivyokusudiwa ili kuboresha Elimu nchini.
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome, ameishukuru Benki ya Dunia kwa fedha itakayotolewa ambayo itasaidia katika kuhakikisha kuwa utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) katika sekta ya Elimu unafanikiwa.

Aidha, Naibu Katibu Mkuu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Dkt. Deo Mutasiwa alisema Wizara yake imejiandaa kikamilifu kuhakikisha kuwa fedha zitakazopatikana zinatumika kama zilivyokusudiwa na kuhakikisha zinawafikia walengwa.





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni