Alhamisi, 11 Septemba 2014

WAZAZI WATAKIWA KUSIMAMIA NIDHAMU YA WATOTO



Waziri wa Elimu na Mafunzo  ya Ufundi Mhe. Dkt. Shukuru Kawambwa  amewataka  wazazi kusimamia ipasavyo maadili ya watoto wao ili waweze kufanikiwa na kufikia malengo  waliyojiwekea kitaaluma. Pia aliwataka kushirikiana na walimu katika kuhakikisha watoto wanakuwa na nidhamu ya kuridhirisha katika jamii inayowazunguka.   

Dkt Kawambwa alitoa wito huo katika mahafari ya kuwatunuku vyeti wanafunzi wa darasa la saba katika shule ya Msingi  Kongo iliyopo Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani. Ambapo aliwataka walimu na wazazi kuhakikisha wanawasisitiza wanafunzi kutii sheria za shule kama vile uvaaji wa sare sahihi ya shule, kuheshimiana na utumiaji wa lugha nzuri.

“Wazazi tuna jukumu kubwa la kusimamia suala la maadili ya  watoto wetu. Hili ni suala ambalo huwezi kulitenanisha na mafanikio bora kitaaluma. Mara nyingi mtoto wenye nidhamu na maadili mema daima hufanya vizuri darasani na yule asiye na nidhamu huporomoka katika taaluma. Nasisitiza nidhamu na taaluma huenda pamoja, haiwezekani kuvitenganisha hata mara moja.” Alisisitizi Dkt. Kawambwa.
Aidha, aliwataka wanafunzi wote nchini wanaomaliza darasa la saba kujiandaa vyema kufanya Mitihani yao inayotarajiwa kuanza,  kujitahidi kutulia na kutumia vyema maarifa yote waliyopata kutoka kwa walimu wao. Aliwakumbusha kwamba watakapomaliza mitihani yao wasijisahau na kufikiri kuwa sasa elimu ndio basi bali watambue kuwa safari ya kutafuta elimu ndio inaanza.

Dkt Kawambwa aliwataka kutenga muda wa kujiandaa kwa masomo ya sekondari mara wanapomaliza mitihani yao ya darasa la saba. "Nawasihi muwe raia wema wenye kuwajibika katika jamii yote. Maisha sio lele mama! wekeni juhudi katika masomo, elimu ndio msingi bora wa maisha, msidanganyike hakuna njia ya mkato katika kufanikiwa katika maisha".  aliongeza Dkt. Kawambwa. 
Waziri Kawambwa aliwataka walimu wote nchini kutambua kuwa shughuli za kila siku shuleni zinahitaji juhudi za hali ya juu. Aliwataka kuboresha  zaidi utendaji kazi wao ili kufikia matarajio ya Taifa ya kuwa na  watu walioelimika na wenye uwezo wa kuhimili  changamoto zinazotokana na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia.

Waziri aliwasisitiza walimu kukabiliana na changamoto zinzojitokeza katika sekta ya elimu kwa kuacha kufanya kazi kwa mazoea, badala yake kuhakikisha wanapanga mipango yao, wanajiwekea malengo ya muda mfupi na mrefu na kubuni mikakati sahihi inayotekelezeka ambayo itawezesha kufikia malengo waliyojiwekea.  

Aidha, aliwashauri wazazi  kutoa ushirikiano wa hali ya juu katika suala zima la kufanikisha matokeo mazuri ya ufaulu kuanzia madarasa ya awali, la kwanza hadi darasa la Saba. "Yote haya yanawezekana pale tutakapotekeleza wajibu wetu wa kusimamia vyema yale yote wanayofundishwa watoto wetu wanapokuwa shuleni. Watoto hupewa mazoezi mbalimbali (homework) na walimu wao ili wazifanye wanapokuwa nyumbani, ni jambo la msingi tukitenga muda kusimamia katika eneo hili. "

  Pia aliwataka wazazi kuhakikisha wanatimiza jukumu lao la kuwapatia watoto mahitaji muhimu yanayotakiwa shuleni.  Kwani mara nyingi utoro wa Wanafunzi shuleni huchangiwa sana wanafunzi wanapo shindwa kupatiwa mahitaji yao ya shule.

Aliwataka wanafunzi wanaobaki shuleni kujitahadi  kuzingatia Masomo. Kwani kipindi walichonacho shuleni ni kifupi sana, lakini ni kipindi  muhimu sana katika kuandaa maisha yao ya baadaye. Amewataka kuwasikivu, kutii sheria za shule, tekeleza majukumu yao wanayopewa katika masomo, kuepuka vitendo viovu katika jamii. Alwasihi kuwa na nidhamu inayopendeza machoni na mioyoni mwa wazazi, walezi na walimu wao. 

Shule ya Msingi Kongo ilianzishwa mwaka 1976 ikiwa na wanafunzi 38 na sasa ina wanafunzi 612 kuanzia Darasa la Awali hadi Darasa la Saba. Wanafunzi 72 wanaohitimu Elimu ya Msingi katika Shule hii mwaka huu.. 

















Hakuna maoni:

Chapisha Maoni