Jumatatu, 9 Novemba 2015

USHAURI WANGU KWA SERIKALI JUU YA UBORESHAJI WA MIUNDOMBINU YA ELIMU.


Josias Charles.

Baada ya mchakato mzima wa Kampeni kukamilisha na hatimaye Serikali kuundwa na Chama cha Mapinduzi kupitia kwa aliyekua mgombea wake wa Urais Mh. Dkt. John Pombe Magufuli tunapaswa kuungana wote na kutoa mawazo yenye lengo la kujenga uchumi wa Nchi Yetu.

Kumekuwepo na tatizo sugu la ukosefu ama kuwa na miundombinu mibovu mbalimbali ya Elimu Kama Madarasa, Maktaba, Mabweni, Maabara, Madawati nk. Ukosefu wa miundombinu hii umekwamisha ama kudumaza utoaji wa Elimu nchini.

Binafsi napenda kuishauri Serikali ya awamu ya Tano kuwekeza katika kuimarisha Elimu ya ufundi (VETA) na kuweka sera madhubuti itakayowabana wahitimu wa vyuo vya ufundi kujitolea kama sehemu yao ya mafunzo lakini pia ikiwa kama sehemu ya Kujitolea kujenga Taifa.


Mitaala ya Elimu ya ufundi Kama itatolewa kwa kipindi cha miaka miwili basi mwaka mmoja utumike kwa mafunzo darasani na mwaka mmoja kwa mafunzo kwa vitendo yaani( FIELD). Wanachuo wote wa VETA hata kama watasoma bure lakini wakatakiwa kufanya field kwa mwaka mzima watakua wameshiriki kwa kiwango kikubwa katika Ujenzi wa Taifa letu.

Mfano wanafunzi 10,000 wakichukua mafunzo ya ufundi kwa mwaka kwa uwiano tuu wa mafundi uashi 5000 na mafundi seremala 5000 kisha baada ya masomo ya mwaka mmoja wakaenda field kwa Mwaka mmoja kujenga Shule, hospitali, vituo vya afya, kutengeneza samani za ofisi tutapunguza gharama kiasi gani?

Nchi Yetu tuna raslimali nyingi ikiwemo raslimali watu lakini hatujaweza kuiendeleza. Naomba tuwekeze katika  kuendeleza raslimali tulizo nazo kwa manufaa ya Taifa letu.

Baada ya kuhitimu mafunzo ya miaka miwili tunao uwezo wa kuwatengenezea ajira vijana hawa na kuwawezesha mitaji inayotokana na shughuri zao katika jamii kwa kujitolea kwa mwaka mzima.

Hebu fikiria Serikali inaagiza samani za ofisi kiasi gani kwa mwaka? Pesa kiasi gani inatumika? Vipi kama vijana waliohitimu VETA mafunzo ya miaka miwili tena kwa kujitolea kujenga Taifa kwa mwaka mzima wakisajiriwa na  kampuni na kupata soko la uhakika toka Serikali na kuachana na uagizwaji wa samani za kichina tutapunguza tatizo la ajira kwa kiwango gani?

Vipi kama vijana walio soma ufundi uashi na kujitolea kujenga Taifa kwa mwaka mzima  wakapewa mikataba ya kujenga nyumba kama za NHC na Majengo mengine mengi tutapunguza tatizo la ajira kwa kiwango gani?

Tuna amini Serikali ya awamu ya Tano ipo makini na inalenga kila MTU afanye kazi kutimiza kauli mbiu ya "HAPA KAZI TU"

Mawaziri, Wabunge, na viongozi wote wa Serikali onyesheni ubunifu kulifanya Taifa letu lisonge mbele.

Kwa Leo inatosha.

HapaKaziTu