Jumatano, 24 Mei 2017

Wasichana na Wanawake kuwezeshwa kupitia elimu


Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknoloji Dkt Leonard Akwilapo leo amefungua warsha ya kuanzishwa kwa mradi wa pamoja wa uwezeshaji wa wasichana na wanawake  kupitia elimu kwa lengo la kuwatafakarisha wilaya lengwa (Ngorongoro, Kasulu, Sengerema,micheweni na mkoani pemba) juu ya vikwazo vya elimu kwa wasichana katika maeneo yao na kubuni mikakati mbalimbali ya kukabiliana navyo ili wasichana wapate fursa ya kujiendeleza kielimu na kukuza fursa ya kuwa raia bora Zaidi.

Mradi huu wenye thamani ya dola za kimarekani milioni tano unafadhiliwa na shirika la Kimataifa la Maendeleo la Korea (KOICA) kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ambapo unatarajiwa kuwanufaisha wasichana na wasichana 8,000 walioko shuleni na wasichana 600 walio nje ya shule, kwa kuwapatia fursa ya kuimarisha ujuzi wao wa msingi, ufundi na ujuzi wa kawaida ambao utawawezesha kuwa raia bora katika nchi yao na ulimwengu kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kuchangia kikamilifu katiak maendeleo ya Tanzania.

Akizungumza wakati wa ufunguzi Katibu Mkuu amesema Awamu ya kwanza ya mradi huu unalenga nchi tatu ambazo ni Tanzania, Mali na Nepal na utaratibiwa na Wizara ya elimu Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto na Wizara ya katiba na Sheria na kutekelezwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni pamoja na UNFPA na UN Women.

Mradi huu ni sehemu ya mpango wa ulimwengu kupitia mashirika ya UNESCO, UNFPA na UN Women kwa ajili ya kuwawezesha wasichana kupitia elimu uliozinduliwa katika nchi sita duniani kote.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt Leonard Akwilapo akifungua warsha ya kuanzishwa kwa mradi wa pamoja wa uwezeshaji wa  Wanawake na Wasichana kupitia Elimu, mkutano ambao umefanyika jijini Dar es salaam hii leo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt Leonard Akwilapo akifuatilia Makala zilizoandaliwa kuonyesha namna Wasichana  na Wanawake wanavyofurahia kupata Elimu ya namna ya kujikinga na matatizo katika jamii yanayoambatana na mila potofu kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni. (UNESCO.)

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt Leonard Akwilapo akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa warsha mara baada ya ufunguzi wa warsha ya kuanzishwa kwa mradi wa pamoja wa uwezeshaji wa wasichana na Wanawake kupitia Elimu.Hakuna maoni:

Chapisha Maoni