Jumanne, 26 Septemba 2017

MBINU ZA KUFUNDISHIA ZIMEPUNGUZA UTORO - KKK MKOANI SINGIDA

Walimu wanaofundisha darasa la awali hadi la tatu katika shule ya msingi Nyerere, Mughanga na shule ya wanafunzi wenye mahitaji Maalumu Ikungi zote zilizopo mkoani Singida wameeleza kuwa  mbinu za kuimba, kucheza, kujifunza kwa kushirikisha wanafunzi zinawasaidia wanafunzi kuelewa kwa haraka pamoja na kuwa na umahiri wa  kusoma na kuandika na kuhesabu.

Akizungumza na timu ya wanahabari walio katika ziara ya kufuatilia hali ya ufundishaji na ujifunzaji wa KKK na kuangalia hali ya uboreshaji wa miundombinu mkoani humo Mwalimu Salome Kyomo amepongeza jitihada za serikali za kuwapatia walimu mafunzo ya KKK kwa kuwa mbinu na zana za kufundishia zimeboreshwa.


Kwa upande wake mratibu wa taaluma wa  shule ya msingi Nyerere Lisu Mnyambi amesema shule hiyo ilipokea kiasi cha shilingi Milioni 192 kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Programu ya Lipa kulingana na matokeo. ambazo zimetumika kujenga vyumba vya madarasa 8, ujenzi wa matundu ya vyoo na hivyo kupunguza  msongamano wa wanafunzi madarasani.

Walimu wa shule ya Msingi Mughanga mkoani Singida  wakiwa kwenye moja ya darasa la Pili ambalo mbinu mbalimbali za kujifunzia na kufundishia , (KKK) zipo katika darasa hilo.


Baadhi ya vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Nyerere iliyopo mkoani Singida ambayo imejengwa na fedha zilizotolewa na  Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Program ya lipa kulingana na Matokeo, (P4R)


Mwanafunzi wa darasa la Pili katika Shule ya Endeberg iliyopo Manyara vijijini akisoma kile kilichoandaliwa na Mwalimu wake huku wanafunzi wengine wakimsikiliza. Lengo la Mwalimu hapo ni kujua wanafunzi wake wanaelewa kile alichowafundisha.

KKK NA UBORESHAJI MIUNDOMBINU GEITA

Mkuu wa mkoa wa Geita Meja Jenerali Ezekiel Kyunga amesema ujenzi na uboreshaji wa miundombinu unaotekelezwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia  programu ya Lipa kulingana na Matokeo ( P4R ) umepunguza changamoto ya uhaba wa madarasa uliokuwa unaukabili mkoa huo kutokana na kuwepo kwa mwitikio mkubwa wa wazazi wa kuandikisha watoto kujiunga na darasa la kwanza.

Kyunga amesema mkoa huo ulipatiwa kiasi cha shilingi milioni 194 kutoka Programu ya P4R ambazo zimejenga madarasa Nane, kuweka umeme shuleni hapo na uchimbaji wa  kisimana hivyo kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji.


Shule za msingi zilizotembelewa ni pamoja na Nguzombili,   Kalangalala ambazo zina madarasa ya awali mpk darasa la tatu, (madarasa yanayoongea)pamoja na kituo cha wanafunzi wenye mahitaji maalumu  kilichopo kwenye shule ya Mbugani.

Mwanafunzi wa  darasa la kwanza wa Shule ya msingi kalangalala iliyopo mkoani Geita akisoma ubaoni mbele ya wanafunzi wenzako pale alipotakiwa kufanya hivyo na Mwalimu wake. Hii ni kufuatia ziara ya Maafisa wa kitengo cha mawasiliano Wizarani pamoja na wanahabari ambao wanafuatilia ujifunzaji na ufundishaji wa KKK.


Programu ya Lipa kulingana na matokeo imesaidia kupunguza changamoto ya uhaba wa vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Nguzo mbili, iliyopo mkoani Geita pia shule hiyo umeweza kuweka umeme na kuchimba kusoma na hivyo kutatua changamoto ya maji shuleni hapo


Moja ya darasa linaloongea lililopo kalangalala, mkoani Geita ambalo hutumiwa na wanafunzi wa awali shuleni hapo. Kuanzishwa kw mtaala wa KKK kumewafanya wanafunzi kupenda shule, imesaidia kupunguza utoro kwa wanafunzi na pia imechangia ufaulu wa wanafunzi.

TATHMINI YA MWAKA 2016, P4R

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na OR - TAMISEMI kwa kushirikiana na Washirika  wa maendeleo leo wamekutana mjini Dodoma kufanya Tathmini  ya utekelezaji wa Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo ( EP4R)  kwa mwaka 2016/17 ili kuona mafanikio yaliyopatikana, changamoto na kuweka mikakati ya kutatua changamoto zilizopo katika suala la utoaji wa Elimu bora Nchini.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo Mratibu wa Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo  Gerald Mweli kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia amesema programu hiyo inafanya tathmini ili kujua hali halisi ya utekelezaji wa majukumu, kwa kiasi gani mradi umefanikiwa lakini pia kuona changamoto na namna ambavyo serikali kwa kushirikiana na washirika wa watakavyozitatua.

Mweli ametaja  mafanikio yaliyopatikana kupitia mradi huo,kuwa ni pamoja na  kujenga na kukarabati  miundombinu chakavu ya shule za Msingi na Sekondari zipatazo 361 kutoka katika Halmashauri 129, vyumba vya mdarasa 1,435, mabweni 261, majengo ya utawala 11, mabwalo 4, vyoo 2,832, nyumba za walimu 12, maktaba 4, na uwekaji wa maji katika shule nne (4).

Kwa upande wa vyuo vya ualimu programu imefanikiwa kukarabati  vyuo 10 vya ualimu ikiwa ni pamoja na kununua  compyuta 260 zitakazowawezesha walimu  kutekeleza  majukumu yao kwa urahisi, magodoro 6,730 yatakayotumiwa na wanafunzi pamoja na viti 1976 kwa ajili ya wanachuo.


Aidha, programu imenunua vifaa vya maabara 1,696 kwa ajili ya shule za sekondari ambavyo zitasaidia katika ufundishaji wa masomo ya sayansi na kuongeza uelewa kwa wanafunzi.