Alhamisi, 2 Novemba 2017

Ndalichako: Tanzania imedhamiria kufikia malengo ya maendeleo endeleve

Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imedhamiria kufikia malengo ya Maendeleo endelevu kwa kuhakikisha inatimiza malengo yaliyowekwa ikiwa ni pamoja na kutoa Elimu bure kuanzia Elimu ya awali mpaka kidato cha Nne, uboreshaji wa miundombinu ya kujifunzia na kufundishia, uboreshaji wa vyuo vya ualimu pamoja na kuboresha mazingira kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

Hayo yameelezwa jana na Waziri wa Elimu , Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako wakati akihutubia mkutano mkuu wa 39 wa UNESCO, Mjini Paris nchini Ufaransa, ambapo katika kufikia malengo hayo walimu 68,799 tayari wamepatiwa mafunzo maalumu ya mtaala ulioboreshwa, KKK.

Waziri Ndalichako aliwaeleza wajumbe wa mkutano huo kuwa suala la wanafunzi wenye mahitaji maalumu bado linahitaji kuangaliwa kwa mapana zaidi hivyo kuziomba nchi wanachama kutoa kipaumbele katika kuandaa  mazingira ambayo yatakuwa rafiki kwa wanafunzi wa kike na wale wa kiume ambao wana mahitaji maalumu.

Waziri Ndalichako Pia alieleza kuwa tayari vifaa vya maabara na vitabu kwa shule za Sekondari limesambazwa kwa nchi nzima ili kutilia mkazo masomo ya Sayansi.


Waziri Ndalichako pia tayari ameshiriki mikutano mbalimbali inayohusu tume za UNESCO zilizoanza oktoba 30, 2017 ambapo amepokea taarifa zinazohusu fursa mbalimbali za namna ya kupata misaada ya maendeleo kutoka UNESCO na washirika wake wa kimataifa.

Pia kupitia mkutano huo Mkuu viongozi wa Tume za Taifa za  UNESCO  duniani wanapata fursa ya kukutana na kubadilishana uzoefu na kupeana mbinu mbalimbali za kuandika kazi miradi kwa maslahi ya nchi zao.

Mkutano huo mkuu wa 39 wa UNESCO ulianza Oktoba 30, 2017 ambapo  Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni -UNESCO -IRINA BOKOVA alisema Tume hiyo  imekuwa na mafanikio kutokana na  ushirikiano inaoupata kutoka kwa nchi wanachama.

Katika mkutano huo waziri wa Elimu Profesa Ndalichako ameambatana na Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa Balozi Samwel Shelukindo, Mkurugenzi wa Sera na Mipango Petro Lyatuu kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya UNESCO  Dkt. Moshi Kimizi.

Mkutano huo Mkuu hufanyika kila baada ya miaka miwili na unahusisha nchi zote wanachama za UNESCO.




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni