Jumatano, 1 Novemba 2017

Waziri kuwasilisha msimamo wa Tanzania kwa UNESCO leo


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce   Ndalichako leo anawasilisha taarifa  yenye msimamo wa Serikali ya  Jamuhuri ya muungano wa Tanzania katika mkutano mkuu wa 39 wa shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi, Utamaduni, habari na Mawasiliano -UNESCO.

 Waziri Ndalichako pia tayari ameshiriki mikutano mbalimbali inayohusu tume za UNESCO zilizoanza oktoba 30, 2017 ambapo amepokea taarifa mbalimbali zinazohusu fursa mbalimbali za namna ya kupata misaada ya maendeleo kutoka UNESCO na washirika wake wa kimataifa, pia viongozi wa Tume za Taifa za  UNESCO  duniani kubadilishana uzoefu na kupeana mbinu mbalimbali za kuandika kazi miradi kwa maslahi ya nchi zao.

Mkutano huo mkuu wa 39 wa UNESCO ulianza juzi Oktoba 30, 2017 ambapo  Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni -UNESCO -IRINA BOKOVA alisema Tume hiyo   ina nguvu kwa sababu ya ushirikiano inaoupata kutoka kwa nchi wanachama.

Katika mkutano huo waziri wa Elimu Profesa Ndalichako ameambatana na Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa Balozi Samwel Shelukindo, Mkurugenzi wa Sera na Mipango Petro Lyatuu kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya UNESCO  Dkt. Moshi Kimizi.
Mkutano huo Mkuu hufanyika kila baada ya miaka miwili na unahusisha nchi zote wanachama za UNESCO.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni