Jumatatu, 20 Novemba 2017

Waziri Ndalichako: Ili shule isajiliwe lazima ikidhi vigezo

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema ili shule isajiliwe lazima iwe imekidhi vigezo ikiwa ni pamoja na kuwa na madarasa ya kutosha, nyumba za walimu, ofisi za walimu, matundu ya vyoo, pamoja na maabara endapo shule itakuwa ni ya Sekondari.

Waziri Ndalichako ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi wa halmashauri ya Mbulu iliyopo mkoani Manyara ambapo amesema ni kweli serikali inahitaji ziwepo shule nyingi ambazo zinavigezo, siyo kuwa na shule ambazo hazina vigezo.

"Shule za nyasi katika Serikali hii ya awamu ya tano zitabaki kuwa historia kwa kuwa serikali inajenga na kuboresha miundombinu ya kujifunzia na ile ya kufundishia, sasa ili shule isajiliwe lazima iwe imekidhi vigezo siyo bora shule bali tunahitaji shule zilizobora na zenye viwango vinavyokubalika" amesema Waziri Ndalichako.

Waziri Ndalichako amesema   kazi ya usajili ni nyepesi sana ambayo haichukui muda mrefu endapo vigezo vinakuwa vimetimia,  lakini kazi kubwa ni kuhakikisha miundombinu bora inayokubalika inakuwepo ili shule iweze kusajiliwa.

 Hivyo amewasihi wadau wote wa Elimu kuhakikisha shule zinapojengwa zinazingatia na kukidhi  vigezo kabla ya kusajiliwa.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni