Jumatatu, 18 Desemba 2017

Waziri Ndalichako aongoza Harambee ya kuchangia ujenzi wa mabweni shule ya Sekondari Sovi

Zaidi ya shilingi milioni Mia moja zimepatikana wakati wa Harambee ya Ujenzi wa mabweni ya  wasichana katika shule ya sekondari Sovi iliyopo  kata ya Mtwango Mkoani Njombe.

fedha hizo zimepatikana wakati wa  harambee iliyoongozwa na Waziri wa Elimu, Sayasni na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako  mwishoni mwa wiki  mkoani Njombe ambapo amewataka  vijana kuwa wazalendo, pamoja na kuhakikisha wanasoma kwa bidii kwa maslahi ya Taifa.

Waziri Ndalichako pia  amewasihi vijana kuhakikisha wanaipenda nchi yao pamoja na kujiepusha na makundi ambayo hayana tija kama vile utumiaji wa dawa za kulevya, kujiingiza kwenye makundi ya uhalifu, na utumiaji wa pombe vitendo ambavyo havina faida kwa maisha yao ya sasa na ya baadae.

Waziri Ndalichako amesema kuwepo kwa mabweni kutawapunguzia wanafunzi kutembea umbali mrefu, kuwaepusha na vishawishi vya barabarani wakati wa kwenda na kurudi shuleni  na hivyo watatumia muda wao mwingi kwenye kusoma.

Ndalichako amesema kazi ya Serikali ni kuboresha miundombinu, na kuhakikisha mahitaji muhimu ya wanafunzi yanapatikana shuleni hivyo wanafunzi nao lazima watimize wajibu wao kwa kuhakikisha wanasoma na kufaulu katika mitihani yao.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka amesema mkoa wake unatambua jitihada zinazofanywa na Serikali ya awamu ya Tano katika kutatua changamoto mbalimbali katika sekta ya Elimu.


Amesema katika mkoa wake kati ya Shule Kumi za sekondari za umma shule Tisa zina mabweni lengo likiwa ni kuondoa changamoto ya upatikanaji wa mimba kwa wanafunzi, pamoja na kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wanaomaliza kidato cha Nne.




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni