Jumatatu, 19 Februari 2018

TAARIFA KWA UMMA



TAARIFA KWA UMMA
Nimepokea kwa masikitiko makubwa sana taarifa ya kifo cha Akwilina  Bafhata Akwiline aliyekuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo cha Usafirishaji (NIT).
Kifo hicho kimetokea wakati askari wakiwa wanadhibiti maandamano yaliyokuwa yakifanyika tarehe 16/02/2018 kwenye eneo la Mkwajuni Wilaya ya kinondoni, jijijini Dar es salaam.

Napenda kutumia fursa hii kutoa pole sana kwa Familia ya Ndugu,  jamaa na marafiki wote wa Akwilini.  Pia napenda kutoa pole kwa Uongozi na Jumuia ya Chuo cha Usafirishaji, wanafunzi wote nchini na wananchi wote kwa ujumla.

Ndugu Akwilini ni binti aliyekuwa anatambua na kuthamini umuhimu wa Elimu, na alijitoa kuhakikisha kuwa anasoma kwa bidii kwa manufaa yake binafsi, familia yake na kwa manufaa mapana ya taifa taifa.  Kifo chake kimetokea wakati akiwa kwenye kutekeleza wajibu wake kama mwanafunzi wa kupeleka barua mahali alipokuwa anatarajia kufanya mazoezi kwa vitendo yatakayoanza tarehe 27/02/2018. Kifo hicho cha kusikitisha kimezima ndoto yake Serikali ikekipokea kwa masikitiko makubwa sana. 

Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Joseph Pombe Magufuli amesikitishwa  na kuhuzunishwa sana na kifo cha mwanafunzi Akwilini na anaungana na familia, ndugu jamaa na watanzania wote kuwapa pole za dhati kutokana na msiba huo. 
Serikali inatumia fedha nyingi kuwasomesha wanafunzi kuanzia Elimu msingi, sekondari na hutoa mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya juu kwa sababu tunatambua mchango wa Elimu katika maendeleo ya nchi yetu. Marehemu Akwilini alikuwa ni miongoni mwa wanufaika wa Mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu. 

Mimi  Waziri mwenye dhamana ya  sekta ya Elimu nimesikitika sana kuona binti huyo amepoteza maisha yake akiwa katika kutekeleza shughuli za kielimu.

Wizara yangu itagharamia shughuli zote za mazishi ya Marehemu Akwilina hadi hapo atakapopumzishwa katika makao yake ya milele. 
Namuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Dk. Leonard Akwilapo kusimamia shughuli zote za msiba huo hadi  Akwilina atakapozikwa katika nyumba yake ya milele. 

Nitumie fursa hii kuviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuwafikisha mara moja wahusika waliosababisha kutokea kwa tukio hilo kwenye vyombo vya sheria ili  wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria za nchi yetu.

Nawasihi sana watanzania wenzangu tujiepushe kukiuka tarataibu na miongozo inayokuwa inatolewa ikiwemo  maandamano na vitendo vyote ambavyo vinaweza kusababisha maafa kwa watu wasio na hatia.

Mungu aiweke roho ya Marehemu Akwilini mahala pema peponi Ameni

Imetolewa na:

Prof Joyce Lazaro Ndalichako
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia.
18 / 02/2018


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni