Ijumaa, 9 Machi 2018

Naibu Waziri Ole Nasha asisitiza uadilifu na utunzaji wa siri za ofisi.


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. William Ole Nasha amewataka watumishi wapya wa Wizara hiyo kuwa waadilifu katika utendaji kazi pamoja na kutunza siri katika maeneo wanayofanyia kazi.

Naibu Waziri Ole Nasha ametoa rai hiyo mjini Dodoma wakati wa akifunga mafunzo kwa waajiriwa wapya wa Wizara hiyo, mafunzo ambayo yamelenga kuwakumbusha taratibu, sheria na miongozo ya kazi inayotakiwa katika utumishi wa umma.

Naibu Waziri huyo amesema anaamini mafunzo yaliyotolewa yatawawezesha kuwa watumishi bora wa umma ambao wanafahamu vema mipaka ya kazi, taratibu za kiutumishi lakini pia haki na wajibu katika utendaji kazi.

Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia, Mhe.William Ole Nasha akifunga mafunzo ya watumishi wapya wa Wizara hiyo ambapo amewataka kuzingatia maadili ya Utumishi wa Umma,ikiwa ni pamoja na kutunza Siri za ofisi.

Pamoja na mambo mengine Naibu Waziri Ole Nasha amemuagiza Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu wa Wizara hiyo Moshi Kabengwe kuandaa utaratibu wa mafunzo kwa watumishi wengine wa Wizara hiyo ili kuwakumbusha taratibu, kanuni na miongozo kwa lengo la kuepuka ukiukaji wa maadili na pia kuleta chachu ya mabadiliko katika utendaji kazi miongoni mwa watumishi.


Nae mmoja wa watumishi aliyeshiriki mafunzo hayo Lazaro Julius kutoka Ofisi ya Kamishna wa Elimu wa Wizara hiyo amesema mafunzo hayo ni muongozo thabiti katika kutekeleza majukumu ya kazi za kila siku katika utumishi wa umma ambapo ameahidi kuzingatia na kutekeleza yote yaliyoelekezwa.

Mafunzo  kwa waajiriwa wapya wa Wizara hiyo yamefanyika kwa siku Nne kuanzia Machi 6, na yameshirikisha waajiriwa wapya kutoka wizara ya Elimu Makao Makuu na Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo.

Watumishi wapya wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wakifuatilia mafunzo Maalumu ya namna wanavyotakiwa kutekeleza majukumu yao katika Utumishi wa Umma ambayo yamefanyika mkoani Dodoma.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni