Ijumaa, 2 Machi 2018

Naibu Waziri Ole Nasha: Kuna ubadhirifu wa fedha za Serikali.


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe.william Ole Nasha ameitaka  ofisi ya Mkuu wa wilaya, Musoma, Polisi na Takukuru kuhakikisha ndani ya wiki mbili inafanya  uchunguzi wa namna fedha za  ujenzi wa Miundombinu ya  Shule ya Sekondari Kasoma zilivyotumika kwa kuwa kuna harufu ya ubadhirifu wa fedha hizo.

Naibu Waziri Ole Nasha ametoa agizo hilo  mkoani Mara baada ya kufanya ziara ya kukagua ujenzi na ukarabati wa Miundombinu ya Shule inayonengwa na Wizara hiyo kupitia programu ya Lipa kulingana na matokeo, (P4R).

Mheshimiwa Ole Nasha amekiri kuridhishwa na ujenzi uliofanyika katika baadhi ya shule za mkoa ambazo amezitembelea ni  pamoja na Shule ya Msingi Kamuguruki  na Shule Sekondari na  Nyasho.

Waziri Ole Nasha pia amewataka walimu  wote nchini kuhakikisha wanafuata maadili yao ya kazi pamoja na kuacha mara moja  kujihusisha na vitendo vya kimapenzi na wanafunzi.

Amesema kuwa wizara yake imepokea taarifa juu ya baadhi ya walimu kujihusisha kimapenzi na wanafunzi  jambo ambalo ni kinyume cha sheria za nchi pamoja na maadili ya utumishi wa umma.

Naibu Waziri huyo amesisitiza kuwa  serikali haitamvumilia mwalimu yeyote mwenye tabia kama hizo na kuongeza kuwa mwalimu atakayebainika kushiriki vitendo hivyo atashtakiwa kwa mujibu wa sheria za nchi.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri  Ole Nasha ameahidi kutoa mabati Mia Tano kwa ajili ya  shule ya sekondari kiara na kujenga madarasa matatu katika shule  Msingi ya Kiara zilizoezuliwa kufuatia mvua kali iliyonyesha jana usiku na kufanya uharibifu wa madarasa mawili ya shule hiyo.

Pia Naibu Waziri Ole Nasha ametembelea chuo cha Maendeleo ya Wananchi Bweri
Kilichopo Wilayani Musoma mkoani Mara.

 Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. William Ole Nasha akipata maelezo kutoka kwa wanafunzi wanaosomea  fani ya ufundi umeme kutoka kwenye Chuo cha  Maendeleo ya Wananchi Bweri kilichopo Mkoani Mara.

Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe.William  Ole Nasha akipata maelezo juu ya hatua za ujenzi wa shule ya Sekondari Kasoma ambapo Naibu Waziro ametoa Wiki mbili kwa Wilaya ya Musoma, Takukuru na Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi mara baada ya kubaini kuwepo kwa ubadhirifu wa fedha za ujenzi katika shule hiyo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni