Jumatano, 7 Machi 2018

Serikali imesema haitasita kuvunja mkataba na Kampuni ya Skywards Construction


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mheshimiwa  Wiliam Ole Nasha, amesema Serikali haitasita kuvunja Mkataba na Kampuni ya Skywards Construction inayopaswa kujenga miundombinu ya ufundishaji na ujifunzaji katika Chuo cha Ualimu Ndala kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Nzega, mkoani Tabora.

Naibu Waziri ametoa Kauli hiyo baada ya Kampuni ya Skyward Construction  iliyopaswa kujenga Mabweni, Vyumba vya Madarasa, Ukumbi, Maktaba, Maabara na Matundu ya vyoo kutoonekana katika eneo la ujenzi tangu alipokabidhiwa kutekeleza mradi huo mapema mwezi Januari 27, 2018.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mheshimiwa  William Ole Nasha akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega Jacob Mtalitinya juu ya changamato zinazoikabili Shule ya Sekondari Kampala katika kukamilisha ujenzi wa Miundombinu ya ufundishaji na ujifunzaji.

Akizungumza akiwa kwenye ziara ya kukagua utekelezaji wa Miradi inayotekelezwa na Wizara yake kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matoke- EP4R, Naibu Waziri  Ole Nasha amesema Kampuni hiyo tangu ikabidhiwe Mradi haijawahi kufika eneo la mradi kuanza ujenzi na bila taarifa yoyote hivyo kuacha maswali mengi yasiyokuwa na majibu.
‘Kampuni hii ilipaswa kuanza kazi Februari 24, 2018 cha kushangaza hadi sasa haijaonekana eneo la Mradi bila taarifa yoyote. Kampuni hii ya Skyward Constuction inapaswa kujua imeingia mkataba na mikataba hii huwa ina taratibu zake, kama kuna jambo haliendi sawa ni bora akaeleza kwa kuwa Serikali haitasita kuvunja mkataba nae.’ Alisisitiza Naibu Waziri Ole Nasha.

Naibu Waziri Ole Nasha amezitaka Kampuni mbalimbali za ujenzi  kuhakikisha zinazingatia Mikataba, kwani kuchelewa kukabidhi Mradi kwa wakati  kunaisababishia Serikali gharama zisizo za lazima kwa kuwa vifaa vya ujenzi vitapanda bei lakini pia Mradi kushindwa kukidhi kusudio la kuwepo kwa wakati huo.

Nae Mkuu wa Chuo cha Ualimu Ndala Abinego Ndikumwe amesema pamoja na Serikali kukarabati na kujenga miundombinu ya ujifunzaji na ufundishaji bado Chuo hicho kina changamoto za upatikanaji wa Maji, ukosefu wa  usafiri kwa matumizi ya Chuo, Bwalo na ofisi za Wafanyakazi.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. William Ole Nasha akikagua ujenzi wa Miundombinu ya  Shule ya Sekondari Mwanzoli, iliyojengwa na Wizara hiyo kupitia Progamu ya Lipa kulingana na Matokeo, EP4R ambapo mara baada ya ukaguzi huo Naibu Waziri amekiri kuridhishwa na ukarabati huo na kuzitaka shule nyingine kuuga mfano huo.

Akiwa Wilayani Nzega Mhe. Ole Nasha ametemtembelea Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Nzega na Mwanhala, Shule ya Sekondari Kampala na Shule ya Sekondari Mwanhala ambapo akiwa kwenye Shule ya Sekondari Mwanzoli na amekiri kurdhishwa na namna Shule hiyo ilivyotekeleza mradi wa ujenzi wa miundombinu ya shule, ambapo ameahidi Wizara yake itahakikisha inakamilisha ujenzi wa Maabara, na  Nyumba mbili za Walimu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni