Jumatano, 16 Mei 2018

EP4R ILIVYOSAIDIA KUONDOA CHANGAMOTO YA MIMBA KWA WANAFUNZI WA KIKE MKOANI LINDI.


Wakuu wa shule za Sekondari mkoani Lindi wamesema kuwa ujenzi wa mabweni unaotekelezwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia mradi wa Lipa Kulingana na matokeo, yaani EP4R katika mkoa huo utasaidia sana kuondoa changamoto ya wananfunzi wa kike kupata mimba wakiwa katika umri mdogo.

Wakizungumza na wanahabari kutoka vyombo mbalimbali Mkuu wa shule ya sekondari ya Ruangwa Mwalimu Herber Ngonyani amesema kupitia mradi wa EP4R shule hiyo imeweza kujenga mabweni Mawili ambayo yanauwezo wa kuchukua wanafunzi Laki moja na sitini kwa wakati mmoja, huku Mkuu wa shule ya Sekondari Nkowe Ahmed Maliki akikiri kuwa shule yake  imejenga mabweni mawili yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi mia moja na ishirini na nane kwa mara moja.
Muonekano wa bweni katika Shule ya Sekondari Ruangwa Wilayani Ruangwa Mkoani Lindi. Bweni hilo limejengwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R).


Wakuu hao wa shule wameeleza kwa muda mrefu watoto wa kike katika wilaya hiyo wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kutembea umbali mrefu na hivyo kukumbana na vishawishi ambavyo hupoteza ndoto za wanafunzi hao.

“ Nikiri kuwa mwamako wa Elimu katika Wilaya yetu bado uko chini hivyo hata hamasa ya wazazi na watoto nayo iko chini katika suala zima la Elimu, sasa hiki ambacho Wizara ya Elimu, Sayansi  na Teknolojia inachokitekeleza kupitia mradi wa Lipa kulingana na matokeo kwa kweli ni mkombozi kwa watoto wa kike kwa kuwa sasa watasoma kwa utulivu tena wakiwa katika mazingira ya shule kutokana na ujenzi huu wa mabweni,”anasema Mwalimu Herbert Ngonyani.


Kwa upande wake Mkuu wa shule ya Sekondari ya Nkowe Ahmed Maliki amessitiza kuwa uwepo wa mabweni utasaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa changamoto ya utoro miongoni mwa wanafunzi pamoja na kuwasidia wanafunzi wa kike kupuka mazingira hatarishi ya kutembea umbali mrefu takribani kilometa 4 hadi tano kwa siku kwa ajili ya kufika shuleni. 
Muonekano wa bweni katika Shule ya Sekondari Nkowe Wilayani Ruangwa Mkoani Lindi. Bweni hilo limejengwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R). Bweni hilo litasaidia kuondoa changamoto ya wanafunzi wa kike kupata mimba katika umri mdogo.

Mwalimu Malik amesema kuwa mabweni hayo yatasaidia siyo tu kuhuduia wanafunzi wa wanaotoka kwenye mkoa wa Lindi pekee bali wananfunzi kutoka mikoa mbalimbali watanufaika na mabweni hayo.


Katika kutekeleza uboreshaji wa Miundombinu ya shule za msingi, moja ya shule ambazo zilipatiwa fedha za kujenga miundombinu hiyo ni pamoja na shule ya msingi Nangumbu ambayo ilipatiwa kiais cha shilingi Milioni sitini na sita kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa vitatu na matundu ya vyoo sita lakini shule hiyo imeweza kujenga vyumba vya madarasa vinne, ofisi moja na matundu kumi ya vyoo.

Timu ya wananhabari ambayo imeambatana na maafisa wa Kitengo cha Mawasiliano cha Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kesho itaendelea na ziara yake Mkoani Mtwara ikiwa na lengo la kuangalia hali ya uboreshaji wa miundombinu ya shule za Msingi na Sekondari inayotekelezwa kupitia program ya lipa kulingana na matokeo.
Muonekano wa moja ya darasa liliojengwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R) katika Shule ya Sekondari Nkowe iliyopo katika Wilaya ya Ruangwa Mkoani Lindi.





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni