Alhamisi, 21 Juni 2018

PROFESA MDOE APONGEZA UBUNIFU NA KUWATAKA WANAFUNZI WABUNIFU KUJITOKEZA KWA WINGI


Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa James Mdoe amewataka wanafunzi ambao wanakipaji cha ubunifu kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi ili waweze kuonyesha vipaji vyao, kwa kuwa bunifu zao zinatakiwa zitatue changamoto mbalimbali hapa nchini.

Profesa Mdoe ameyasema hayo leo mkoani Dodoma wakati akifunga jukwaa la Maonesho ya ubunifu kwa vijana wenye umri kuanzia miaka 13 hadi 21 yanayosimamiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia chini ya Mradi wa kukuza Ujuzi, na stadi za kazi, ESPJ.
Kaimu Katibu Mkuu huyo amesema vijana wabunifu wakiendelezwa vyema watapata fursa ya kuchangia uchumi wa Taifa kupitia bunifu zao mbalimbali.
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe akizungumza na wadau mbalimbali wa masuala ya ubunifu wakati akifunga maonesho ya ubunifu yaliyohusisha wanafunzi wa shule za msingi na Sekondari kutoka Tanzania bara na Visiwani, yaliyofanyika mkoani Dodoma.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Dk. Ave Maria Semakafu akizungumza katika maonesho hayo ametambua mchango wa kijana Keton Mbwiro ambaye amehitimu Elimu yake ya Msingi na ameweza kubuni kijiko maalumu cha gari ambacho hutumika kuchimba na kuchota mchanga. Pia amebuni gari la kubeba vifaa vya ujenzi hivyo ameahidi kuwa kijana huyo atapelekwa shule ya ufundi ili aweze kujiendeleza.

“Keton Mbwiro ni kijana mdogo lakini ameweza kubuni kitu ambacho miaka ya nyuma tulizoea kuona vitu vya namna hii vinafanywa na wanafunzi wa vyuo vikuu, hivyo uwezo wake lazima tuuendeleze kwa kuhakikisha anakwenda shule ya Ufundi, pia ni vyema watanzania tukaachana na dhana ya kuwa vyuo vya ufundi ni vya useremala pekee bali ni zaidi ya hapo.” anasema Dk. Semakafu.
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe akiwa na baadhi ya watendaji wa Wizara hiyo wakiangalia moja ya ubunifu uliohusisha mashine ya kusafishia/kuondoa uchafu kwenye mazulia. Maonesho hayo yamefanyika katika Chuo Kikuu cha Dodoma, Mjini Dodoma. 

Mradi wa kukuza Ujuzi na Stadi za kazi, ESPJ ni mradi wa miaka miatano ambao unatekelezwa kwa ushirikiano wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Benki ya Dunia, lengo likiwa ni kuhakikisha mkakati wa Serikali wa Tanzania kuwa
nchi ya Uchumi wa viwanda mpaka 2025 inatimia.
Prof. James Mdoe ambae ni Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia akiwa ameshika chupa yenye dizeli iliyotokana na kuyeyushwa kwa chupa za plastiki ambazo zimekwisha matumizi yake.


Jumatano, 13 Juni 2018

NAIBU WAZIRI WA ELIMU ASEMA SERIKALI HAITAFUMBIA MACHO VITENDO VYA UDHALILISHAJI DHIDI YA WANAFUNZI


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mheshimiwa William Ole Nasha amesema Serikali haitafumbia macho vitendo vya udhalilishaji dhidi ya wanafunzi na kuwa Sheria kali zitachukuliwa kwa wale wote watakaobainika kuhusika na vitendo hivyo.

Naibu Waziri Ole Nasha ametoa kauli hiyo leo Mkoani Dodoma wakati wa mahojiano maalumu na Shirika la Utabgazaji la Taifa - TBC ambapo amesema Sheria za nchi ziko wazi kwa mtu yeyote atakaebainika kufanya vitendo vya ngoni basi adhabu yake ni miaka 15 jela hadi kifungo cha maisha.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mheshimiwa William Ole Nasha akifanya mahojiano na mtangazaji wa Shirika la Utangazaji Tanzania-TBC wakati huu ambapo Mataifa mbalimbali yakijielekeza katika kudhimisha siku ya mtoto wa Afrika. Mahojiano hayo yamefanyika Jijini Dodoma ambapo Naibu Waziri ameelezea pia mafanikio mbalimbali kuhusu sekta ya Elimu. 

Mheshimiwa Ole Nasha pia ameitaka Idara ya Uthibiti Ubora wa Shule nchini kuhakikisha unafanya ufuatiliaji kwa lengo la kuhakikisha Elimu bora inapatikana nchini kwa kuwa hilo ndiyo jukumu lao.

“Kuna maeneo bado Idara ya uthibiti ubora haijafanya vizuri, mfano katika hili tukio la St. Florence Idara hiyo ina kitu cha kujibu,” licha ya kuwa vyombo vingine vya Sheria vinaendelea na uchunguzi lakini na sisi ndani ya Wizara tunafanya uchunguzi kuona nani kazembea katika suala hilo,” alisisitiza Naibu Waziri Ole Nasha.

Naibu Waziri pia amewataka wazazi kuhakikisha watoto wote waliofika umri wa kwenda shule wanakwenda shule kwa kuwa hivi sasa Elimu msingi kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha Nne inatolewa bure.

Akizungumzia kuhusu viwanda Mheshimiwa Ole Nasha amesema vyuo vya ufundi ndiyo njia sahihi ya kulipeleka Taifa katika Uchumi wa Kati, hivyo kupitia vyuo hivyo Taifa litapata  nguvukazi na  sahihi ambayo itatumika kwenye viwanda.


Ijumaa, 8 Juni 2018

SERIKALI YASEMA HAITAVUMILIA WALIMU WANAOSHIRIKI VITENDO VYA UDHALILISHAJI KWA WANAFUNZI


Serikali imesema haitavumilia vitendo vya udhalilishaji ambavyo vimekuwa vikijitokeza katika baadhi ya shule hapa nchini na kusisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukukuliwa kwa wale wote watakaobainika kuhusika na vitendo hivyo.

Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako mkoani Dodoma wakati akikabidhi tuzo kwa wanafunzi waliofanya vizuri kitaifa katika masomo yao ya kuhitimu darasa la saba, Kidato Cha Nne na kidato Cha Sita kwa shule za serikali na zisizokuwa za serikali.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akitoa cheti na fedha kwa mwanafunzi bora kitaifa katika masomo ya sayansi Sophia Juma  aliyefanya vizuri katika matokeo ya kumaliza kidato cha sita mwaka 2017. Utoaji wa tuzo hizo umefanyika mkoani Dodoma katika kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Elimu

Waziri Ndalichako amewataka wanafunzi nchini kote kusoma kwa bidii, kuwa na nidhamu pamoja na kuishi kwa kufuata maadili ya kitanzania na siyo kuiga maadili ya watu wa nje.

“Wakuu wa shule nchini kote nawaagiza kuhakikisha mnasimamia kwa weledi malezi ya wanafunzi, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha walimu mnakemea vitendo vya udhalilishaji ambavyo vimekuwa vikijitokeza katika shule hapa nchini. Suala hili nasema si la kufumbia macho na wale wale wote watakaobainika kuhusika na vitendo hivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa,” amesema Waziri Ndalichako.

Waziri Ndalichako amewaeleza wanafunzi hao kuwa suala la kupata ushindi ni rahisi lakini kudumu katika ushindi si kazi nyepesi.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Leonard Akwilapo akizungumza na wajumbe walioshiriki kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Elimu (hawapo pichani) amesisitiza kuwa lengo la utoaji wa tuzo katika Wiki ya Elimu ni kutoa motisha na kuongeza ari kwa wanafunzi ili wafanye bidii katika masomo yao. Hafla ya utoaji wa tuzo hizo umefanyika leo Mkoani Dodoma katika Shule ya Sekondari Dodoma. 

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dk. Binilith Mahenge amewapongeza wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo yao kitaifa ambapo amesema Silaha pekee ya ujenzi wa Taifa na rasilimali za Taifa ni Elimu, ambapo pia amewataka wanafunzi kudumisha nidhamu  na maadili.

Akizungumza kwa niaba ya Serikali ya Uingereza katika maadhimisho hayo ya wiki ya Elimu Gertrude Mapunda  amesema serikali ya Uingereza itaendelea kuisaidia  Serikali ya Tanzania katika kuboresha sekta ya Elimu.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akipokea maelezo ya awali kutoka kwa Mkurugenzi wa Sera na Mipango Gerald Mweli kuhusu vigezo vilivyozingatiwa katika kupata wanafunzi bora waliofanya vizuri kitaifa katika masomo yao ya kuhitimu darasa la saba, kidato cha nne na kidato cha sita kwa Shule za serikali na zisizokuwa za Serikali.  

Jumatano, 6 Juni 2018

WAZIRI NDALICHAKO ASHIRIKI KUAGA NA KUZIKA MAPACHA WALIOUNGANA MARIA NA CONSOLATA


·         AWATAKA WATANZANIA KUISHI KWA KUPENDANA
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia amewataka watanzania kujenga tabia ya kupendana, kuvumilia na kuhurumiana katika maisha ya kila siku.

Waziri Ndalichako ameyasema hayo leo mkoani Iringa mara baada ya kuongoza mamia ya wananchi wakati wa ibada ya kuaga miili ya mapacha walioungana Maria na Cosolata katika viwanja vya Chuo Kikuu Cha RUAHA mkoani Iringa.   

Amesema Maria na Consolata katika uhai wao waliishi wakiwa wameungana kwa hiyo waliishi kwa kuvumiliana na kupendana pia.
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akiaga miili ya mapacha walioungana Maria na Consolata katika viwanja vya Chuo Kikuu cha RUAHA Mkoani Iringa.

Amesema, Watanzania wanatakiwa kujiuliza kwa nini Maria na Consolata wamezaliwa Tanzania na Siyo nchi nyingine? amesisitiza kuwa watoto hao wamezaliwa nchini hapa ili iwe funzo kwa watanzania.

Maria na Consolata watazikwa kwenye jeneza moja litakalokuwa na misalaba miwili.
Maria na Consolata Mwakikuti walifariki jumamosi saa mbili usiku Juni 2 mwaka huu na miili yao itapumzishwa kwenye nyumba yao ya milele kwenye makaburi ya viongozi wa Kanisa Katoliki Tosamaganga mkoani Iringa.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akilia kwa huzuni mara baada ya kuaga miili ya mapacha walioungana Maria na Consolata katika Viwanja vya Chuo Kikuu cha RUAHA Nkoani Iringa.

Kwa upande wake sista Calista Ludega ambaye ni Mkuu wa Shirika la Mtakatifu Theresa wa Mtoto wa Yesu Jimbo Katoliki la Iringa amesema kuwa wamewazika Maria na Consolata mahala wanapolala Masista wa Maria Consolata kwa ajili ya kuwaenzi masista wa Wamishionari wa Consolata kwa kuwa wao wamekuwa sehemu kubwa ya malezi tangu waliopozaliwa watoto hao hadi wanapomaliza maisha yao duniani.

Familia ya Baba na mama wa mapacha hao kutoka Mkoani Mbeya na Kagera, masista wa Consolata wa Iringa na waombolezaji wengine wameungana katika kuwasindikiza katika safari yao ya mwisho duniani.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akiweka saini kitabu cha maombolezo ya Msiba wa mapacha walioungana Maria na Consolata.

OLE NASHA: SERIKALI YAAHIDI KUSHIRIKIANA NA DFID


Serikali imehaidi kuendelea kushirikiana na wadau wa Sekta ya Elimu katika kuhakikisha watoto wa kitanzania wanapata Elimu iliyo bora ili kufikia malengo ya mkakati wa kuwa na uchumi wa viwanda.

 Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mheshimiwa Wiliam Ole Nasha jijini Dar es Salaam katika kikao cha pamoja kilichowakutanisha Wadau wa Elimu walio chini ya Shirika la  Maendeleo ya Kimataifa ya Uingereza-DFID

Naibu Waziri Ole Nasha amesema ushirikiano wa serikali ambao umekuwepo kwa muda mrefu na wadau hao wa Elimu umechangia katika kuhakikisha mtoto wa Kitanzania anapata Elimu iliyo bora.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha akizungumza na wajumbe katika kikao kilichoandaliwa na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa ya Uingereza-DFID. Kikao hicho kimewashirikisha wadau wa Elimu kutoka EQUIP –T, EP4R, HDIF,GPE, British Council, GPE, na RISE
“Elimu bora kwa kila mtoto wa kitanzania ndiyo msimamo wa Serikali, katika kutekeleza hilo sera ya Elimu bila malipo imekuwa  na baadhi ya chagamoto  na katika kukabiliana nazo ndiyo maana wamekuwepo wadau wa Elimu ambapo sasa wanafanya kazi kwa kushirikiana na Serikali ili kutimiza malengo yanayokusudiwa, kwani hatuwezi kuboresha Elimu kama kila mtu atafanya kazi peke yake, Umoja ni Nguvu.”amesema Mheshimiwa Ole Nasha.

Ole Nasha amesema mpaka sasa wadau hao wa Elimu kupitia Mpango wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R) wameshatoa  kiasi cha zaidi ya bilioni 200 ambazo zimekusudiwa kufanya uboreshaji wa Miundombinu ya shule za msingi na Sekondari, pamoja na kukarabati na kujenga vyuo vya Ualimu.


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha akishiriki katika moja ya majadiliano ya pamoja katika kikao kilichoandaliwa na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa ya Uingereza-DFID kikao ambacho kimefanyika jijini Dar es salaam.

Naye Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa ya Uingereza-DFID Jane Miller ameishukuru serikali ya Tanzania kwa ushirikiano ambao wamekuwa wakiupata katika kuhakikisha fedha zinazotolewa zinatumika kama zilivyokusdiwa. Kikao hicho kimewashirikisha wadau wa Elimu kutoka EQUIP –T, EP4R,HDIF,GPE, British Council, GPE, na RISE