Jumatano, 13 Juni 2018

NAIBU WAZIRI WA ELIMU ASEMA SERIKALI HAITAFUMBIA MACHO VITENDO VYA UDHALILISHAJI DHIDI YA WANAFUNZI


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mheshimiwa William Ole Nasha amesema Serikali haitafumbia macho vitendo vya udhalilishaji dhidi ya wanafunzi na kuwa Sheria kali zitachukuliwa kwa wale wote watakaobainika kuhusika na vitendo hivyo.

Naibu Waziri Ole Nasha ametoa kauli hiyo leo Mkoani Dodoma wakati wa mahojiano maalumu na Shirika la Utabgazaji la Taifa - TBC ambapo amesema Sheria za nchi ziko wazi kwa mtu yeyote atakaebainika kufanya vitendo vya ngoni basi adhabu yake ni miaka 15 jela hadi kifungo cha maisha.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mheshimiwa William Ole Nasha akifanya mahojiano na mtangazaji wa Shirika la Utangazaji Tanzania-TBC wakati huu ambapo Mataifa mbalimbali yakijielekeza katika kudhimisha siku ya mtoto wa Afrika. Mahojiano hayo yamefanyika Jijini Dodoma ambapo Naibu Waziri ameelezea pia mafanikio mbalimbali kuhusu sekta ya Elimu. 

Mheshimiwa Ole Nasha pia ameitaka Idara ya Uthibiti Ubora wa Shule nchini kuhakikisha unafanya ufuatiliaji kwa lengo la kuhakikisha Elimu bora inapatikana nchini kwa kuwa hilo ndiyo jukumu lao.

“Kuna maeneo bado Idara ya uthibiti ubora haijafanya vizuri, mfano katika hili tukio la St. Florence Idara hiyo ina kitu cha kujibu,” licha ya kuwa vyombo vingine vya Sheria vinaendelea na uchunguzi lakini na sisi ndani ya Wizara tunafanya uchunguzi kuona nani kazembea katika suala hilo,” alisisitiza Naibu Waziri Ole Nasha.

Naibu Waziri pia amewataka wazazi kuhakikisha watoto wote waliofika umri wa kwenda shule wanakwenda shule kwa kuwa hivi sasa Elimu msingi kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha Nne inatolewa bure.

Akizungumzia kuhusu viwanda Mheshimiwa Ole Nasha amesema vyuo vya ufundi ndiyo njia sahihi ya kulipeleka Taifa katika Uchumi wa Kati, hivyo kupitia vyuo hivyo Taifa litapata  nguvukazi na  sahihi ambayo itatumika kwenye viwanda.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni