Ijumaa, 8 Juni 2018

SERIKALI YASEMA HAITAVUMILIA WALIMU WANAOSHIRIKI VITENDO VYA UDHALILISHAJI KWA WANAFUNZI


Serikali imesema haitavumilia vitendo vya udhalilishaji ambavyo vimekuwa vikijitokeza katika baadhi ya shule hapa nchini na kusisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukukuliwa kwa wale wote watakaobainika kuhusika na vitendo hivyo.

Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako mkoani Dodoma wakati akikabidhi tuzo kwa wanafunzi waliofanya vizuri kitaifa katika masomo yao ya kuhitimu darasa la saba, Kidato Cha Nne na kidato Cha Sita kwa shule za serikali na zisizokuwa za serikali.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akitoa cheti na fedha kwa mwanafunzi bora kitaifa katika masomo ya sayansi Sophia Juma  aliyefanya vizuri katika matokeo ya kumaliza kidato cha sita mwaka 2017. Utoaji wa tuzo hizo umefanyika mkoani Dodoma katika kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Elimu

Waziri Ndalichako amewataka wanafunzi nchini kote kusoma kwa bidii, kuwa na nidhamu pamoja na kuishi kwa kufuata maadili ya kitanzania na siyo kuiga maadili ya watu wa nje.

“Wakuu wa shule nchini kote nawaagiza kuhakikisha mnasimamia kwa weledi malezi ya wanafunzi, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha walimu mnakemea vitendo vya udhalilishaji ambavyo vimekuwa vikijitokeza katika shule hapa nchini. Suala hili nasema si la kufumbia macho na wale wale wote watakaobainika kuhusika na vitendo hivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa,” amesema Waziri Ndalichako.

Waziri Ndalichako amewaeleza wanafunzi hao kuwa suala la kupata ushindi ni rahisi lakini kudumu katika ushindi si kazi nyepesi.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Leonard Akwilapo akizungumza na wajumbe walioshiriki kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Elimu (hawapo pichani) amesisitiza kuwa lengo la utoaji wa tuzo katika Wiki ya Elimu ni kutoa motisha na kuongeza ari kwa wanafunzi ili wafanye bidii katika masomo yao. Hafla ya utoaji wa tuzo hizo umefanyika leo Mkoani Dodoma katika Shule ya Sekondari Dodoma. 

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dk. Binilith Mahenge amewapongeza wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo yao kitaifa ambapo amesema Silaha pekee ya ujenzi wa Taifa na rasilimali za Taifa ni Elimu, ambapo pia amewataka wanafunzi kudumisha nidhamu  na maadili.

Akizungumza kwa niaba ya Serikali ya Uingereza katika maadhimisho hayo ya wiki ya Elimu Gertrude Mapunda  amesema serikali ya Uingereza itaendelea kuisaidia  Serikali ya Tanzania katika kuboresha sekta ya Elimu.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akipokea maelezo ya awali kutoka kwa Mkurugenzi wa Sera na Mipango Gerald Mweli kuhusu vigezo vilivyozingatiwa katika kupata wanafunzi bora waliofanya vizuri kitaifa katika masomo yao ya kuhitimu darasa la saba, kidato cha nne na kidato cha sita kwa Shule za serikali na zisizokuwa za Serikali.  

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni