Jumatano, 18 Julai 2018

NDALICHAKO AZITAKA TAASISI ZA ELIMU YA JUU ZENYE MAPUNGUFU ZIJIREKEBISHE


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amezitaka Taasisi za Elimu ya Juu nchini ambazo matokeo ya uhakiki yalibainisha kuwa na mapungufu kurekebishe kasoro hizo kama walivyoelekezwa na Mamlaka husika.

Waziri Ndalichako ametoa  agizo hilo Leo Jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi   wa Maonesho ya kumi na tatu ya Elimu ya Juu ambapo amesema taasisi hizo zisipofanya hivyo basi hatua stahiki zitachukuliwa, ikiwa ni pamoja na kufutiwa usajili.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na wadau wa Elimu ya Juu (hawapo pichani) ambao wanashiriki katika maonesho ya kumi na tatu ya Elimu ya Juu wakati wa ufunguzi wa maonesho hayo yanayofanyika katika viwanja vya Mnazi mmoja Jijini Dar es alaam ambapo amezitaka Taasisi zote za Elimu nchini kuzingatia ubora wa Elimu wanayoitoa.

Waziri  Ndalichako pia amewaagiza Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU) na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) kuendelea kusimamia kwa karibu na kwa  umakini masuala yote yanayohusu ubora wa Elimu inayotolewa na Taasisi za Elimu ya Juu.

” Katika Awamu hii ya Tano watu wanaofanya kazi kwa mazoea hawana nafasi, lazima muwe wabunifu nampitie upya zana mnazotumia kuhakiki ubora wa vyuo. Haiwezekani kila siku tunasikia malalamiko kuhusu ubora wa wahitimu wakati TCU na NACTE mpo” amesisitiza Prof. Ndalichako.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. James Mdoe wakisikiliza ufafanuzi kuhusu masuala mbalimbali ya elimu  kutoka kwa mmoja wa washiriki wa maonesho ya kumi na tatu ya Elimu ya Juu yanayofanyika jijini Dar es Salaam, ambapo washiriki hao wametakiwa kujitadhimini kuhusu utoaji wao wa Elimu ya Juu 

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo  Prof. James Mdoe amesema maonesho hayo ya Elimu ya Juu yatazisaidia Taasisi mbalimbali za Elimu kujitathmini na kupata mrejesho kutoka  kwa wadau namna  wanavyotekeleza majukumu yao.

Maonesho ya Taasisi za Ellimu ya Juu ambayo yatafanyika kwa siku nne yanalenga kutoa elimu kwa umma kuhusu fursa zinazopatikana kwenye Taasisi za Elimu ya  Juu,  kutoa nafasi kwa wananchi wanaotarajia kujiunga na Elimu ili elimu ya kujiridhisha na programu za masomo na huduma zinazotolewa.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. James Mdoe akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa Tume ya Vyuo Vikuu ambao ni waandaaji wa maonesho ya kumi na tatu ya Elimu ya Juu yanayofanyika jijini Dar es Salaam.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni