Jumatano, 11 Julai 2018

WAZIRI NDALICHAKO AMTAKA KATIBU MKUU WIZARA YA ELIMU KUWACHUKULIA HATUA WALIOHUSIKA NA SAKATA LA VIFAA VYA MAABARA CHUO CHA UALIMU KASULU


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amemtaka Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kuwachukulia hatua wale wote waliohusika na uagizaji na upokeaji wa vifaa vya maabara katika Chuo cha Ualimu Wilayani Kasulu mkoani Kigoma.

Waziri Ndalichako ametoa kauli hiyo Wilayani Kasulu alipofanya ziara katika Chuo hicho na kukuta idadi kubwa ya kemikali za maabara zisizohitajika lakini pia vifaa vya maabara kutokuwa na ubora huku chuo kikiomba kununuliwa tena vifaa vya maabara na kemikali.

“Haiwezekani kwa sasa manasema mna upungufu wa vifaa pamoja na kemikali wakati mmevijaza hapa chuoni tena kwa utaratibu usiofaa, huku mkisema vitaharibika kwa kuwa havihitajiki, ni nani aliviagiza na ni kwanini mliviagiza bila ya kuwa na uhitaji, kwa hili sio la kufumbia macho ni lazima hatua zichukuliwe kwa wale wote waliohusika katika suala hili”alisema Profesa Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akipokelewa na Mwenyekiti wa Bodi pamoja na Watumishi wa Chuo cha Ualimu Kasulu kilichopo Mkoani Kigoma wakati alipowasili chuoni hapo. 
Waziri Ndalichako pia ameitaka Idara ya Elimu ya Ualimu katika Wizara hiyo pamoja na Chuo cha Ualimu Kasulu kutoa taarifa ya kina ya uagizaji na upokeaji wa vifaa hivyo kwa kuwa kumekuwepo na kutokuelewana baina yao ni nani alitoa mahitaji halisi ya vifaa hivyo hali iliyoisababishia Serikali hasara ya kununua vifaa visivyohitajika wakati zipo shule za Sekondari zingeweza kupata vifaa hivyo.

“Bahati mbaya bodi yenu haina taarifa ya manunuzi haya, wakuu wa vyuo muache tabia ya kuficha mambo yanayoendelea chuoni hapa nachukua hatua na bodi iangalie hatua za kuchukua hatuwezi kuruhusu mtu anayefanya uhalifu huu akabaki salama,” alisema Profesa Ndalichako.
Wzairi wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akikagua kemikali za Maabara katika Chuo cha Ualimu Kasulu

Awali Mkuu wa Chuo cha Ualimu Kasulu Josephat Mwangamila katika hotuba yake alisema Chuo hicho kina deni la takribani shilingi milioni 64 kwa ajili ya ununuzi wa Kemikali na Vifaa kwa ajili ya matumizi ya ofisi (stationary) kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha sita waliofanya mitihani.

Mkuu wa Chuo alisema walifikia uamuzi wa kununua kemikali hizo kwa kuwa hawakuwa nazo chuoni hapo lakini pia zilizokuwepo hazihitajiki kwa matumizi chuoni hapo.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akikagua miundombinu ya majengo ya Chuo Cha Ualimu Kabanga Mkoani Kigoma. Akiwa Chuoni hapo Profesa Ndalichako amezungumza na wakufunzi pamoja na watumishi wa chuo na kuahidi kujenga upya Chuo hicho kwa kuwa miundombinu yake imechakaa. 

Serikali imenunua vifaa vya maabara  vyenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni Moja ambavyo vimesambazwa katika vyuo vyote vya ualimu nchini ikiwa ni juhudi za kuhakikisha walimu wanapata mafunzo kwa vitendo ili wakaweze kufundisha kwa umahiri pindi wanapomaliza masomo yao.

Waziri wa Elimu pia ametembelea Chuo cha Ualimu Kabanga ambapo ameahidi kujenga upya chuo hicho katika mwaka wa fedha ulioanza 2018/19 kwa kuwa majengo yake ni chakavu na kuvitaka vyuo ambavyo vimekarabatiwa kuwa na dhamira ya dhati ya kutunza miundombinu ya vyuo.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akikagua miundombinu ya ngazi za mabweni ambayo imechakaa katika Chuo Cha Ualimu Kasulu, Wilayani Kasulu Mkoani Kigoma

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni