Ijumaa, 31 Agosti 2018

KATIBU MKUU WIZARA YA ELIMU AWATAKA WAKUU WA VYUO VYA UALIMU KUFUATA TARATIBU KATIKA UTENDAJI


Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Leonard Akwilapo amewataka Wakuu wa Vyuo vya Ualimu vya Serikali kuacha kufanya kazi kwa mazoea badala yake wafuate taratibu wakati wa kutekeleza majukumu yao ya kikazi ikiwa ni pamoja na kushirikisha watumishi na wanafunzi wa Chuo taarifa za mapato na matumizi ya fedha.

Dk. Akwilapo ameyasema hayo leo Jijini Dodoma wakati alipokutana na Wakuuu wa Vyuo hivyo kwa lengo la kujadili mafanikio, changamoto na mikakati waliyonayo katika kuhakikisha majukumu na uendeshaji wa vyuo yanatekelezeka bila changamoto ili waweze kufikia azma ya kuandaa walimu bora.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Leonard Akwilapo akizungumza na Wakuu wa Vyuo vya Ualimu vya Serikali (hawapo pichani) katika kikao kazi cha kujadili mafanikio, changamoto na Mikakati bora ya kuwezesha Vyuo  kutekeleza majukumu yake bila changamoto Mkoani Dodoma. 

Pia Katibu Mkuu huyo amewataka Wakuu wa Vyuo kuwasirikisha wale wanaowasimamia katika kuandaa mikakati ya utendaji ili waweze kutoa mchango katika kutekeleza mikakati hiyo na kufikia malengo mapana ya Wizara ambayo ni kutoa Elimu bora.

Katika hatua nyingine Dk. Akwilapo amewataka Wakuu wa Vyuo hao kuanisha mahitaji ya rasilimali watu ambayo inahitajika vyuoni inayoendana na kozi zinazofundishwa katika Chuo husika ili kuepuka kuwa na rasilimaliwatu isiyoendana na mahitaji ya Chuo. 
Baadhi ya Wakuu wa Vyuo wakifuatilia maelekezo ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Leonard Akwilapo wakati wa kikao cha pamoja kilichofanyika leo  Agosti 31, 2018 katika Chuo Kikuu cha Dodoma Jijini Dodoma.  

Naye Mwenyekiti wa Wakuu wa Vyuo vya Ualimu vya Serikali ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha Ualimu Morogoro Agustine Sahili amesema wanaishukuru Wizara kwa kuandaa vikao vya aina hiyo kwani vinawasaidia kuwakumbishia taratibu za kazi na kuahidi kutekeleza yale yote waliyoagizwa ili kuimarisha utendaji katika maeneo ya kazi.

Kikao kazi hicho kimeshirikisha Wakuu wa Vyuo vya Ualimu vya Serikali 35 vilivyopo hapa nchini.
Wakuu wa Vyuo vya Ualimu vya Serikali wakiwa katika picha ya pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Leonard Akwilapo 

Maoni 1 :

  1. Kwakweli hilo la mapato na matumizi ni ugonjwa kwa vyuo vingi

    JibuFuta