Alhamisi, 2 Agosti 2018

NDALICHAKO: ANDAENI WANAFUNZI WENYE UJUZI NA UMAHIRI


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.  Joyce Ndalichako amekiagiza Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kuhakikisha kinaandaa wanafunzi mahiri na wenye ujuzi utakaowawezesha kuchangia katika uchumi wa Taifa.

Ndalichako ametoa agizo hilo wakati wa uzinduzi wa hosteli ya wanafunzi, uliofanyika katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akizungumza na watendaji pamoja na wanafunzi wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (hawapo pichani) wakati wa kuzindua  hosteli ya wanafunzi yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 720 kwa mara moja.

 Amesema kwa kufanya hivyo mtakuwa mnatekeleza Dira ya Elimu ambayo inataka Taifa kuwa na Mtanzania aliyeelimika na mwenye maarifa, stadi, umahiri, uwezo na mitazamo chanya ili kuweza kuchangia katika maendeleo ya Taifa.

 Waziri Ndalichako ameupongeza uongozi wa chuo hicho kwa kuingiza masomo ya uongozi, maadili na uzalendo katika mitaala ya ngazi zote za kitaaluma kwa kuwa ni muhimu katika kuwajengea vijana uzalendo, moyo wa kujituma na kulipenda Taifa.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akizindua hosteli katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na kuwataka wanafunzi wa Chuo hicho kutunza miundombinu hiyo ili iweze kuwasaidia wanafunzi wengine watakaojiunga na Chuo hicho.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Profesa Shadrack Mwakalila amesema hosteli hiyo ni ya ghorofa 5 na ina uwezo kuchukua wanafunzi 720 kwa mara moja hivyo kupunguza tatizo la malazi ya wanafunzi katika chuo hicho.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akikagua baadhi ya miundombinu katika hosteli mpya aliyoizindua katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni