Ijumaa, 31 Agosti 2018

PROF. MDOE AITAKA ESPJ KUACHA ALAMA NA KUTEKELEZWA KATIKA MUDA ULIOPANGWA


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa James Mdoe ameutaka Mradi wa Kukuza Ujuzi na Stadi za Kazi kwa lengo la kuzalisha ajira (ESPJ) kuhakikisha inatekeleza vizuri malengo ya mradi yaliyokusudiwa ikiwa ni pamoja na kuonyesha thamani ya fedha ili Taifa liweze kufikia malengo ya nchi ya kufikia uchumi wa viwanda hadi ifikapo mwaka 2025.

Profesa mdoe ametoa maagizo hayo mkoani Morogoro wakati wa kikao kazi cha waratibu wanaohusika na mradi wa ESPJ kutoka kwenye Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na sekta binafsi na kusisitiza kuwa mradi huo unatakiwa kufanya mambo ambayo yataacha alama ikiwa ni pamoja na  kuhakikisha unafanyika katika muda uliopangwa.

“Bado tuko nyuma katika utekelezaji, wadau na viongozi wanajiuliza umuhimu wa huu mradi, sasa tutekeleze vizuri mradi  ili thamani ya fedha ionekane. Mradi huu upo kwenye moyo wangu nitafurahi kuona unaacha alama na katika kujifunza tuangalie namna mradi wa EP4R ulivyoacha alama, sasa ESPJ na yenyewe ifanye hivyo hivyo,”amesema Profesa Mdoe.
Naibu katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa James Mdoe akizungumza na Waratibu wa Mradi wa Kukuza ujuzi na Stadi za Kazi kwa lengo la kuzalisha ajira (ESPJ), hawapo pichani ambapo ameutaka mradi huo utekelezwe na uwe na matokeo chanya.

Naibu Katibu Mkuu huyo pia amesema kuwa kiuhalisia mradi umechelewa kuanza sasa katika kuutekeleza lazima umakini uwepo ili matokeo chanya ya mradi huo yaweze kuonekana.

Kikao kazi hicho kinahusu uwasilishaji wa  ripoti mbalimbali zinazohusu utekelezaji wa mradi , ikiwa ni pamoja na kufanyika majadiliano ya pamoja kwa lengo la kujengeana uwezo kutoka Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Elimu, Idara ya Elimu ya juu, Kitengo cha Sheria, Idara ya Sera na Mipango, mratibu kutoka ofisi ya TPSF, pamoja na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini.
Waratibu wa Mradi wa Kukuza ujuzi na Stadi za Kazi kwa lengo la kuzalisha ajira (ESPJ) wakiwa katika kikao kazi cha kujengeana uwezo mara baada ya kuwasilishwa kwa ripoti mbalimbali kuhusu utekelezaji wa mradi huo. Kikao hicho kinafanyika kwa siku mbili, Agosti 31 mpaka Septemba 1 mkoani Morogoro.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni