Alhamisi, 16 Agosti 2018

WAZIRI NDALICHAKO AAGIZA CHUO CHA VETA NKASI KUTOA MAFUNZO YA MUDA MFUPI


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.  Joyce Ndalichako ameigiza Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi VETA Kanda ya Kusini Magharibi kuhakikisha Chuo Cha Wilaya ya Nkasi cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi kinaanza kutoa mafunzo ya muda mfupi kuanzia  mwezi Septemba mwaka huu.
Waziri Ndalichako ametoa agizo hilo akiwa ziarani mkoani Rukwa  kwa ajili ya kukagua miradi ya Elimu inayotekelezwa na wizara hiyo katika mkoa wa  Rukwa ambapo amesema majengo yaliyopo yanaweza kuendelea kutumika kutoa mafunzo ya muda mfupi huku serikali ikiendelea na utaratibu wa kufanya  ukarabati katika majengo hayo.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akiangalia ramani ya Chuo Cha Wilaya ya Nkasi cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi wapofanya ziara katika majengo ya chuo hicho yaliyopo katika Wilaya ya Nkasi Mkoani Rukwa. Waziri aliagiza majengo hayo yaanze kutumika kwa kutoa kozi fupi.


Waziri Ndalichako amesema majengo hayo ni imara pamoja na kwamba hayajatumika kwa zaidi ya miaka mitatu lakini miundombinu ya majengo hayo bado ipo vizuri na inahitaji tu kupakwa rangi na kurekebisha  masuala ya umeme . 

“Ukiangali unaona raslimali ya serikali inapotea kuna majengo ambayo yangeweza kutumika kutoa mafunzo kwa vijana wa Nkasi ili kuwapatia ujuzi lakini hayatumiki, bado nasisitiza mtumie majengo haya kwa kuanzia yatumike kwa kutoa kozi za muda mfupi,”alisisitiza Waziri  Ndalichako
Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kusini Magharibi Justine Ruta (Mwenye suti ya Khaki) akitoa ufafanuzi kuhusu Chuo cha VETA Nkasi kwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akijadiliana na Mkuu wa Wilaya hiyo Iddi Kamanta 

Waziri Ndalichako amesema dhamira ya serikali ni kufikia vijana wengi katika kuwapatia ujuzi na maarifa na vijana wa Nkasi ni sehemu ya vijana hao wanahitaji kuwezeshwa kupata ujuzi na maarifa ili kuziona fursa nyingi za kimaendeleo.

Akiwa mkoani Rukwa Waziri Ndalichako pia ametembelea shule ya Sekondari ya Nkasi kwa lengo la kukagua maendeleo ya ukarabati wa miundombinu ya shule hiyo unaofanywa na wadau wa Elimu ambapo katika kuunga mkono juhudi hizo ametoa mifuko 100 ya simenti itakayosaidia katika ujenzi wa miundombinu hiyo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Iddi Kimanta amesema serikali ya wilaya ipo tayari kushirikiana na VETA katika kuhakikisha Chuo hicho kinaanza mapema.

Maoni 1 :

  1. Mkuu WA WILAYA ya Nkasi kwa sawa sio IDD Kimanta Bali ni Said Mtanda

    JibuFuta