Alhamisi, 20 Septemba 2018

OLE NASHA: TCU NA BODI YA MIKOPO SHIRIKIANENI WANAFUNZI WAPATE MIKOPO KWA WAKATI

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia mheshimiwa William Ole Nasha ameiagiza Tume ya Vyuo Vikuu nchini  (TCU) kuhakikisha  inakamilisha uratibu wa udahili wa wanafunzi wa Elimu ya Juu ili kuwezesha zoezi la upangaji wa mikopo kufanyika  katika muda uliopangwa.

Naibu Waziri ametoa agizo hilo alipokutana na viongozi wa TCU  jijini Dar es Salaam ili kupata taarifa ya maendeleo ya udahili huo ambapo amesema kukamilika mapema kwa taratibu za udahili itawezesha Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB)  kupanga na kutoa mikopo kwa wanafunzi hao mapema.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe.Wiliam Ole Nasha akizungumza na viongozi wa Tume ya Vyuo Vikuu nchini alipokutana nao Jijini Dar es Salaam ili kupata taarifaya uratibu wa udahili wa wanafunzi wa Elimu ya juu.
“TCU mkifanya vibaya katika uratibu wa udahili Bodi ya Mikopo ndio inayoathirika kwani lawama zote huishia huko na  siyo TCU, hivyo ili kuweka utaratibu mzuri ni vyema mkafanyakazi kwa ukaribu na kushirikiana ili kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza,” amesisitiza Naibu Waziri huyo.

 Katika hatua nyingine,  Naibu Waziri amekutana na watendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu na kuwataka kuhakikisha wanashughulikia kwa haraka upangaji na utoaji wa mikopo kwa wanafunzi ikiwa ni pamoja na kuwasadia wanafunzi pale zinapotokea changamoto .
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Abdul Razaq Badru akizungumza na Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha wakati wa kikao kilichofanyika jijini Dar es Salaam.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni