Ijumaa, 5 Oktoba 2018

CHUO CHA MUST CHAPONGEZWA KWA KUSIMAMIA UKARABATI CHUO CHA UALIMU TANDALA VIZURI


Serikali imekipongeza Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) kwa kusimamia kwa ufanisi ukarabati wa Chuo cha Ualimu Tandala kilichopo Wilaya ya Makete Mkoani Njombe.

Kauli hiyo ya Serikali imetolewa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha wakati akikagua ukarabati wa miundombinu ya Chuoni hapo mradi ambao unafadhiliwa na Wizara hiyo.

 “Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya wamekuwa wakifanya kazi nzuri za kuridhisha katika miradi yao yote waliokabidhiwa na Wizara na hivi ndivyo inavyotakiwa, Serikali inapotoa fedha kwa ajili ya kurejesha hadhi ya miundombinu ya shule, vyuo na miundombinu mingine zilenge kukamilisha kazi hizo na sio kutanguliza maslahi binafsi na kuingiza Serikali kwenye hasara,” alisema Naibu Waziri Ole Nasha
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akiangalia katika picha muonekano wa zamani kabla ya ukarabati na baada ya ukarabati wa miundombinu ya Chuo cha Ualimu Tandala kilichopo Wilaya ya Makete Mkoani Njombe wakati alipotembelea Chuoni hapo kukagua ukarabati uliofanyika.

Naibu Waziri huyo amezitaka Taasisi nyingine za Serikali kuwa waadilifu katika matumizi ya fedha pindi Serikali inapotoa fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ili malengo yaliyokusudiwa yaweze kutimia huku akiwataka wanafunzi wa chuo hicho kusoma kwa bidii na kufaulu kwa kiwango cha juu.

Kiongozi huyo ameeleza kuwa Serikali ilisitisha kutoa ajira kwa wingi kwa lengo la kupitia mifumo ya ajira upya kwani iliyokuwepo ilizalisha wafanyakazi hewa na wenye vyeti feki hivyo ilikuwa ni lazima kufanya hivyo ili kuiepusha Serikali kuingia kwenye hasara.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akikagua miundombinu ya Chuo cha Ualimu Tandala kilichopo Wilaya ya Makete Mkoani Njombe  baada ya ukarabati.

Nae Mkuu wa Chuo cha Ualimu Tandala Philip Khamisi alisema mpaka sasa Chuo hicho kina wanachuo 225 huku wakitegemea kupokea wanachuo 342 ambapo itafanya idadi ya kufika 567.

Wizara ilitoa zaidi ya shilingi bilioni moja kwa ajili ya kukarabati miundombinu ya Chuo cha Tandala ambacho miundombinu yake ilikuwa imechakaa.
Muonekano wa sasa wa mabweni ya wavulana katika Chuo cha ualimu Tandala kilichopo wilayani Makete mkoani Njombe.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni