Jumatatu, 1 Oktoba 2018

DKT. SEMAKAFU AFUNGUA MAFUNZO YA FORCE AKAUNTI NA KUWATAKA WASHAURI ELEKEZI KUTIMIZA WAJIBU WAO

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Ave Maria Semakafu amewataka washauri elekezi ( consultant) kuhakikisha wanatimiza wajibu  katika kutekeleza majukumu yao pindi wanapokabidhiwa miradi ya kusimamia, na kuwa haipendezi miradi inapoenda kukaguliwa kuwa na masuala ya kutumbuliwa.

Dkt. Semakafu amesema hayo leo mkoani Morogoro wakati akifungua mafunzo ya matumizi ya Force Akaunti ambao ni utaratibu unaotumika kwenye ujenzi au ukarabati kwa kutumia malighafi za ujenzi na mafundi waliopo eneo husika.



Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Ave Maria Semakafu akizungumza wakati akifungua mafunzo ya matumizi ya Force Akaunti yanayofanyika mkoani Morogoro ambapo amewataka washiriki wa mafunzo kuwa wazalendo wanaposimamia miradi ya ujenzi inayotekelezwa na Serikali.

Dkt. Semakafu amesema Force Akaunti ikitumika vizuri inaonyesha thamani ya Fedha lakini pia utaratibu huo hauna mabadiliko ya gharama wakati wa kutekeleza ujenzi au ukarabati tofauti na kutumia mkandarasi katika kutekeleza miradi ya Serikali.

“Force Akaunti ipo kisheria na kinachohitajika ni uzalendo, pia fedha inayotengwa kwa ajili ya ujenzi haiguswi na kuwa  hii inatakiwa ioneshe thamani ya Fedha kwa maana matokeo makubwa kwa fedha kidogo,” alisisitiza Dkt. Semakafu.



Washiriki wa mafunzo wakiwemo Wakurugenzi wa Halmashauri, Wakurugenzi  na Wakurugenzi wasaidizi wa VETA, Maafisa VETA wakifuatilia  mafunzo ya Force Akaunti.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi Dkt. Noel Mbonde   amezitaka Mamlaka za Ufundi Stadi  VETA kuhakikisha zinaleta mabadiliko ili nchi iweze kufikia malengo ya uchumi wa viwanda.

Mafunzo hayo ya siku mbili yanaratibiwa na mradi wa kukuza Maarifa, Stadi na ujuzi (ESPJ) yanahusisha Wakurugenzi wa halmashauri za Kasulu,Ngorongoro,Kongwa,Nyasa, Wakurugenzi wa  Kanda VETA, Wakurugenzi wasaidizi kutoka Makao Makuu VETA, Maafisa kutoka VETA.


Picha ikimuonesha Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Ave Maria Semakafu baada ya kuwasili katika ukumbi wa mkutano mkoani Morogoro akiwa ameongozana na  Mkurugenzi wa Ufundi na mafunzo ya Ufundi Stadi Dkt. Noel Mbonde, na mratibu wa mradi wa kukuza Maarifa, stadi na Ujuzi (ESPJ) Dkt. Keneth Hosea

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni