Jumatatu, 1 Oktoba 2018

NAIBU WAZIRI OLE NASHA AITAKA KAMPUNI YA UJENZI KUWASILISHA MICHORO NDANI YA WIKI MOJA


Naibu waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha ametoa wiki moja kwa mtaalamu Elekezi wa Kampuni ya Archquants Service Limited kuhakikisha inawasilisha michoro ya kazi za nje ya Chuo cha ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi Namtumbo kilichopo Mkoani Ruvuma ili ujenzi wa chuo hicho uweze kukamilika.

Mheshimiwa Ole Nasha ametoa agizo hilo wakati wa kukagua maendeleo ya ujenzi wa chuo hicho ambapo amesema ucheleweshwaji wa michoro hiyo unapelekea kuchelewesha ukamilishaji wa mradi huo.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akipokea taarifa ya Elimu ya Mkoa wa Ruvuma kutoka kwa Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Pololet Mgema wakati wa ziara ya kukagua miradi ya Elimu Mkoni huko.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Ole Nasha ameitaka Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi VETA kuhakikisha   wanaanzisha kozi ya ufundi wa zana za kilimo (Agro mechanics) katika Chuo cha Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi kilichopo Songea ili kupata vijana wengi watakaosomea fani hiyo.

Naibu Waziri amesema ukanda wa Nyanda za Juu Kusini unategemea sana kilimo, hivyo kuanzishwa kwa kozi hiyo kutasaidia wananchi wengi kupata uelewa wa kina kile wanachokisoma na baadae kutekeleza kwa vitendo.

 “Serikali inatilia mkazo Elimu ya ufundi na imejielekeza katika kuhakikisha inapanua fursa ya vijana wengi kupata Elimu ya ufundi na ndio maana  Serikali ya awamu ya Tano imeamua kuweka Vyuo vya VETA katika kila Wilaya na Mkoa,” alisisitiza Naibu Waziri Ole Nasha
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akipata maelezo kutoka kwa mwalimu wa somo la uchomeleaji (welding) Onesmo Pela katika Chuo cha Ufundi Veta Songea namna anavyotekeleza majukumu yake.

Naibu Waziri Ole Nasha yuko mkoani Ruvuma kwa ziara ya kikazi ya siku mbili kwa ajili ya kukagua miradi ya Elimu inayotekelezwa na Wizara ya Elimu, Sayasni na Teknolojia.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akikagua maendeleo ya ujenzi wa Chuo cha Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi cha Namtumbo kilichopo katika Wilaya ya Namtumbo Wilayani Ruvuma

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni