Ijumaa, 12 Oktoba 2018

NAIBU WAZIRI OLE NASHA ATOA MIEZI MITATU KWA HALMASHAURI YA MBULU KUKAMILISHA MIRADI YA ELIMU


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha ameiagiza Halmashauri ya Mji wa Mbulu, mkoani Manyara kuhakikisha inatafuta fedha za kukamilisha miradi ya elimu inayosimamiwa na Wilaya hiyo katika kipindi cha miezi mitatu.

Ole Nasha ametoa agizo hilo baada ya kutembelea na kukagua miradi hiyo na kukuta haijakamilika kutokana na halamashauri hiyo kukosa fedha za kukamilisha hali iliyosababishwa na kutofuata maelekezo ya mradi huku wakipanga kuchangisha wazazi wa wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo ili kukamilisha miradi hiyo.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akikagua moja ya bweni linalojengwa na Wizara kupitia fedha za EP4R katika Shule ya Sekondari ya Chief Sarwatt iliyoko katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu mkoani Manyara

Naibu Waziri ametaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na ule wa ujenzi wa mabweni, madarasa na matundu ya vyoo ndio ambayo inatekelezwa katika shule ya Sekondari Chief Sarwatt iliyopo katika kata ya Endagikot Mkoani humo na kutaka ikamilike bila kuhusisha wanafunzi ama wazazi wao.

 “Suala kuchangisha wanafunzi liko wazi kwa kila mtu, Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli amekataza suala la kuchangisha mwanafunzi au mzazi wa mwanafunzi yeyote eti kwa kuwa mwanafunzi anasoma katika shule fulani, suala la michango linatakiwa kuhusisha jamii nzima bila kujali huyu ni mzazi wa mwanafunzi ama la na linafanyika kupitia ofisi ya Mkurugenzi na si walimu na katika hili mlipaswa kuishirikisha jamii kabla ya kuanza ujenzi,” alisisitiza Naibu Waziri Ole Nasha.

Naibu Waziri Ole Nasha alisema Wizara ya Elimu ilitoa fedha kiasi cha Shilingi milioni 215,500,000 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni 2 ya Wanafunzi, vyumba vitatu vya madarasa na matundu matano ya vyoo na kupaswa kutekelezwa kulingana na maelekezo, lakini halmshauri ilikuja na mpango mwingine wenye makisio tofauti na yale ya Wizara.

“kama mliona kuna chanagamoto mlipaswa kushirikisha Wizara kabla ya kufanya maamuzi mliyofanya ingesaidia kuondokana na kasoro ambazo zinaonekana sasa, na hiki si kitu kipya zipo Halmashauri zinapekelewa fedha kwa ajili ya Hosteli lakini wanaiomba Wizara kubadilishiwa kulingana na uhitaji walionao kwa wakati ule mngefanya hivyo kabla ya kuanza ujenzi ili kupata maelekezo,” aliongeza Naibu Waziri Ole Nasha.
Muonekano wa hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa bweni katika shule ya sekondari ya Chief Sarwatt iliyoko katika halmashauri ya mji wa Mbulu mkoani Manyara

Nae Mwenyekiti wa Bodi ya shule ya Chief Sarwatt Emmanuel Tangao alisema walifikia hatua ya kuanza ujenzi bila kuwashirikisha wananchi kwa kuwa walikuwa wakikimbizana na tamko la Serikali kwamba mwaka huu walipaswa kupokea wanafunzi wa kidato cha tano, lakini pia watakapoishia wangejua ni kiasi gani cha fedha kilichohitajika kukamilisha ujenzi ndipo wachangishe.

Naibu Waziri Ole Nasha amekamilisha ziara yake ya kikazi mkoani Manyara ya kukagua uboreshaji wa miundombinu ya kujifunzia na kufundishia inayotekelezwa katika Halmashauri za Babati, Hanang, Mbulu na Mbulu, pia alitembelea na kukagua Shule ya Sekondari Gehandu, Chuo cha Maendeleo ya Wananchi.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akipata maelezo wa kile wanachojifunza kutoka kwa mwanafunzi anayechukua kozi ya huduma za mifugo katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Tango kilichopo Halmashauri ya mji wa Mbulu Mkoani Manyara.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni