Ijumaa, 5 Oktoba 2018

NDALICHAKO AAGIZA KUONDOLEWA KWA MKUU WA CHUO CHA UALIMU SHINYANGA KWENYE NAFASI YAKE, ASEMA CHUO HICHO KINA HARUFU YA RUSHWA


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Leonard Akwilapo kumuondoa mara moja Mkuu wa Chuo Cha Ualimu Shinyanga Paschal Highmagway kwenye nafasi yake kwa kushindwa kusimamia kazi za ujenzi lakini pia kumtetea Mkandarasi wa Affrique Enginearing and Construction Company Ltd ili hali Mkandarasi huyo ameshindwa kukamilisha kazi yake katika muda uliopangwa.

Waziri Ndalichako ametoa maagizo hayo mara baada ya kukagua ujenzi wa miundombinu chuoni hapo unaotekelezwa na wakandarasi wawili tofauti ambapo Mkandarasi mmoja ni Masasi Construction Company Ltd amekamisha kazi yake kwa asilimia 98 huku Affrique Enginearing and Construction Company Ltd ikishindwa kukamilisha kazi katika muda uliopangwa.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akikagua ujenzi wa miundombinu katika Chuo cha Ualimu Shinyanga, ambapo hajaridhishwa kabisa na kasi  ya ujenzi anayokwenda nayo Mkandarasi wa Affrique Enginearing and Construction Company Ltd

Kufuatia hali hiyo Waziri Ndalichako amemwagiza Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Diwani Athumani kuanza kuchunguza miradi inayotekelezwa katika chuo hicho pamoja na maafisa manunuzi wa Wizara ya Elimu kwa kuwa katika Chuo hicho kuna dalili za rushwa.

Waziri pia amemwelekeza Mkandarasi Afrique Enginearing and Construction Company Ltd kuhakikisha anafanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha kazi hiyo inakamilika ndani ya mwezi mmoja na kuwa  tayari mkandarasi huyo  ameshalipwa kiasi cha bilioni 2 na milioni 700. 

“Haipendezi viongozi wa umma kila siku kukemea watendaji, kutumbuana kila tunapokutana kwenye majukumu, tunatakiwa tunapokutana tuwe tunakaa na kufurahi lakini kwa mtindo huu wa kushindwa kukamilisha kazi kwa wakati serikali haitamvumilia mtu.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akiwa na Mkandarasi wa Affrique Enginearing and Construction Company Ltd wakati wakikagua ukumbi wa mihadhara chuoni hapo na kuwa ujenzi wa ukumbi huo haujakamilika.

Profesa Ndalichako amesema kuwa fedha inayotolewa kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya shule ya vyuo ni sumu na endapo itatumika vibaya waliohusika wataitapika fedha hiyo. 

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko amemhakikishia Waziri kuwa Uongozi wa Wilaya utasimamia kwa karibu kuhakikisha maelekezo aliyoyatoa yanatekelezwa lakini pia amewataka wakandarasi wababaishaji wabadilike na wasipobadilika basi uongozi wa Wilaya utawabadilisha.
Mwanafunzi Skauti katika Chuo cha Ualimu Shinyanga akimvalisha skafu mgeni rasmi ambaye ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako mara baada ya kupokelewa katika Chuo cha Ualimu Shinyanga.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni