Jumamosi, 6 Oktoba 2018

SERIKALI YAWATAKA WALIMU KUACHA KUFANYA UDANGANYIFU KATIKA MITIHANI


Serikali imewataka walimu wote nchini kuacha kufanya vitendo vya udanganyifu wakati wa mitihani huku ikiwataka wanafunzi kuhakikisha wanatoa  taarifa kuhusu vitendo vya udanganyifu vinapokuwa vinatokea.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako wakati wa sherehe za kuadhimisha miaka 25 tangu kuanzishwa kwa shule ya sekondari Don Bosco Didia iliyopo mkoani Shinyanga.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia  Prof. Joyce Ndalichako akiangalia maonesho ya picha na maandishi mbalimbali kuhusu mwanzilishi wa Shule ya Sekondari ya Don Bosco ambayo ilianzishwa mwaka 1993-2018 na kuwa sasa  imetimiza miaka 25.

Waziri Ndalichako amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango unaotolewa na Mashirika ya kidini katika kuwaandaa vijana kitaaluma na kinidhamu na ndiyo maana hakuna vitendo vya udanganyifu katika mitihani kwenye shule hizo kwa kuwa wanafunzi wanaandaliwa vya kutosha pia wana maadili.

“Nichukue fursa hii kuwasihi sana walimu nchini kote kuacha kufanya vitendo vya udanyifu wakati wa mitihani kwa sababu tunawaharibu watoto  na tunatengeneza vijana ambao hawana uwezo kitaaluma, kama tunawafanyia mitihani wakija kupata kazi pia tutawafanyia kazi?

“Nimependa Moto wa shule hii ya Don Bosco Didia kuwa ni kulea, kuwafunza nidhamu watoto kwa lengo la kutimiza ndoto zao naunga mkono juhudi zinazofanywa na viongozi wa shule hii sasa pia ni vyema na shule nyingine zikaiga,” alisisitiza Waziri Ndalichako.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akipokea picha ya mfano wake ambayo imechorwa na mwanafunzi wa shule ya Sekondari ya Don Bosco mkoani Shinyanga wakati wa kuadhimisha miaka 25 tangu shule hiyo ianzishwe.

Waziri Ndalichako ameihakikishia Shule ya Sekondari ya Don Bosco kuwa Serikali iko  pamoja kushirikiana na shule hiyo kwa kuwa mambo wanayoyafanya wanaunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya Tano.

Kwa upande Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Zainab Telack ameisifu shule hiyo ya Don Bosco kwa kuendelea kufanya vizuri katika mitihani ya kidato cha nne na kuwa mkoa unajivunia sana kuwepo kwa shule hiyo ambapo amewasisitiza wanafunzi kuhakikisha wanaendelea kushirikiana ikiwa ni pamoja na kusoma kwa makundi pamoja na kuwasaidia wale ambao uwezo wao ni mdogo.
Waziri Ndalichako akizungumza wakati wa sherehe za kuadhimisha miaka 25 tangu kuanzishwa kwa shule ya sekondari Don Bosco Didia iliyopo mkoani shinyanga.

Katika kuadhimisha miaka 25 tangu kuanzishwa kwa shule hiyo mwaka 1993 Baba Vicent alisimikwa rasmi kuwa Baba wa kiroho kwa ajili ya shule hiyo ya Sekondari.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni