Jumatano, 10 Oktoba 2018

WATUMISHI WANNE NA MWENYEKITI WA BODI YA SHULE WASWEKWA NDANI KWA MATUMIZI MABAYA YA FEDHA ZA MIRADI


Naibu waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Willam Ole Nasha amemuagiza mkuu wa Wilaya ya Mbulu Chelestine Mofuga kuwachukulia hatua za kisheria wale wote waliohusika kubadilisha matumizi ya fedha za miradi ya Shule ya Sekondari Tumatu iliyoko Wilayani Mbulu Mkoni Manyara.

Mheshimiwa Ole Nasha ametoa agizo hilo wakati akikagua ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya Elimu mkoani humo na kukuta fedha zilizotolewa na Wizara ya Elimu kiasi cha sh milioni 141, 600,000 kwa ajili ya ujenzi wa majengo mapya ya madarasa, bweni na vyoo zimetumika kukamilisha jengo la bweni na maktaba ambavyo vilijengwa kwa nguvu za wananchi.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akikagua ujenzi wa bweni katika Shule ya Sekondari Tumatu wilayani Mbulu Mkoani Manyara

Naibu Waziri Ole Nasha amesema shule hiyo ilipatiwa kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya Ujenzi wa bweni moja la wanafunzi, madarasa 3 na matundu ya vyoo 6 lakini fedha hizo hazikuelekezwa kwenye kile kilichokusudiwa badala yake zimetumika kukamilisha majengo ambayo tayari wananchi walianza kujenga kwa gharama ambazo hazina uhalisia.

 "Hapa kuna harufu ya ubadhirifu wa fedha za umma haiwezekani gharama za kumalizia majengo ambayo tayari wananchi wameanza kujenga na kukaribia kukamilika kutumia fedha za kujenga majengo mapya, kujua hili haiitaji mtu kuwa mhandisi ni mahesabu ya kawaida tu, hatua zichukuliwe dhidi ya waliohusika.” Aliongeza Naibu Waziri Ole Nasha
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akitoa maelekezo kwa Viongozi na watendaji wa Halmashauri ya Mbulu kuhusu ujenzi wa bweni la Wasichana uliofanyika  katika Shule ya Sekondari Tumatu iliyoko katika Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara. 

Naibu Waziri Ole Nasha amesema   Serikali ya Awamu ya Tano ya Mhe. Dk. John Pombe Magufuli inatoa kipaumbaele kwenye Sekta ya Elimu na ndio maana kila mahali kuna miradi ya Elimu hivyo fedha za miradi zitumike vizuri na kwamba haitasita kuchukua hatua dhidi ya mtu yeyote atakaebanika anafanya ubadhirifu wa fedha za miradi hiyo.

Kufuatia agizo hilo Mkuu wa Wilaya hiyo amewaweka chini ya ulinzi kwa saa 48 wafanyakazi hao ambao ni Afisa Elimu Sekondari wa Wilaya ya Mbulu Ludovic Longino, Fundi Sanifu (Civil tehnician) wa Halmashauri Moses Nguvava, Mwenyekiti wa Bodi ya Shule Bryson Panga, Mkuu wa shule hiyo Killian John na Afisa Ugavi Faustine Safari kutokana na tuhuma hizo na kuagiza TAKUKURU kuanza uchunguzi mara moja.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akiongea na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Yaeda Ampa pamoja na wanakijiji wa eneo hilo ambapo kwa pamoja amewataka kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano anazozifanya katika kuboresha Sekta ya Elimu. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni