Jumatano, 27 Februari 2019

SERIKALI YA TANZANIA NA ILE YA SUDAN KUSINI KUSHIRIKIANA KATIKA ELIMU

Serikali ya Tanzania na ile ya Sudan Kusini zimetiliana saini makubaliano ya ushirikiano katika sekta ya elimu ambapo wanafunzi wa Sudan Kusini watajifunza lugha ya Kiswahili lakini pia nchi ya Tanzania itapeleka walimu wa lugha ya Kiswahili Sudan Kusini pamoja na kubadilishana uzoefu na ujuzi kati ya nchi hizi mbili.

Makubaliano hayo yamefanyika mkoani Dodoma ambapo kwa upande wa Tanzania Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako ndiye aliyetia saini makubaliano hayo huku nchi ya Sudan Kusini ikiwakilishwa na Waziri wa Elimu wa nchi hiyo Deng Deng Hoc Yai.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako (Tanzania) na Waziri wa Elimu Deng Deng Hoc (Sudan Kusini) wakitiliana saini makubaliano ya kushirikiana katika masuala mbalimbali yahusuyo Elimu katika nchi hizi mbili. 

Waziri Ndalichako amesema makubaliano yanalenga kufungua fursa katika nchi hizo mbili, na kuwa Tanzania iko tayari kuhakikisha inaisaidia nchi ya Sudan Kusini kufikia malengo waliyojiwekea.

“Tukio hili ni muhimu, ambapo nchi ya Sudan Kusini wameomba ushirikiano katika sekta ya Elimu na kuwa Tanzania tunaihakikishia nchi  hiyo ushirikiano kwa kuchapisha vitabu vya somo la Kiswahili, Tanzania pia iko tayari  kwa walimu wa Kiswahili kwenda Sudan kufundisha somo hilo pia nchi hizo mbili zitaweza kubadilishana uzoefu katika eneo la mafunzo ya ufundi stadi," alisema Waziri Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako (Tanzania) na Waziri wa Elimu (Sudan Kusini) Deng Deng Hoc wakionesha mkataba wa makubaliano unaohusu ushirikiano katika sekta ya elimu ambapo wote kwa pamoja wamekubaliana kuendelea kudumisha umoja na ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.

Kwa upande wake Waziri wa Elimu wa Sudan Kusini Deng Deng Hoc Yai ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kudumisha umoja na ushirikiano kati ya nchi hizi mbili huku akisisitiza kuwa Tanzania ni nyumbani.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza wakati wa hafla ya utilianaji saini wa makubaliano ya mashirikiano katika masuala mbalimbali yahusuyo elimu. Amesema makubaliano hayo yanalenga kufungua fursa kwenye sekta ya elimu katika nchi hizo mbili ikiwa ni pamoja na kubadilishana uzoefu na ujuzi.

Waziri Deng Deng amesema kwa sasa Kiswahili ni miongoni mwa lugha zinazoweza kushindanishwa na lugha nyingine za kimataifa kama vile Kingereza na  Kiarabu hivyo nchi hiyo imeona umuhimu kwa shule zao kuanza kufundisha lugha ya kiswahili shuleni.

Waziri wa Elimu Tanzania na Waziri wa Elimu Sudan Kusini wakifurahia jambo baada ya  kutiliana saini makubaliano ya ushirikiano katika masuala mbalimbali  kwenye sekta ya elimu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni