Jumatatu, 4 Februari 2019

WAZIRI NDALICHAKO AAGIZA KUSIMAMISHWA KAZI WATUMISHI 6 CHUO CHA UALIMU PATANDI.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Leonard Akwilapo kuwasimamisha kazi watumishi 6 wa Chuo cha Ualimu Patandi kutokana na kushindwa kusimamia vyema ujenzi wa shule ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu inayojengwa Wilayani Arumeru mkoani ARUSHA.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Jerry Muro, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Ave Maria Semakafu na watendaji wengine wakikagua hali ya ujenzi wa shule ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu inayojengwa katika Chuo Cha Ualimu Patandi mkoani ARUSHA.

Waziri Ndalichako ameyasema hayo baada ya kukagua hali ya ujenzi unaoendelea wa vyumba vya madarasa, jengo la Utawala, na bwalo la chakula na kisha kuwa na kikao cha pamoja na watendaji wa Chuo hicho kwa ajili ya kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali ambayo yameripotiwa na Mkaguzi Mkuu wa ndani wa Wizara hiyo baada ya kufanyika ukaguzi wa mradi huo wa ujenzi.


Mkuu wa Wilaya ya Arumeru akimuonesha Waziri wa Elimu Prof. Ndalichako hatua za ujenzi wa shule ya wanafunzi wenye mahitaji Maalumu inayojengwa Patandi, shule hiyo ikikamilika itakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 640.

Kufuatia hali hiyo, Waziri aliagiza kusimamiashwa kazi kwa  Kaimu Mkuu wa Chuo hicho Issac Myovela, Afisa manunuzi Charles Njarabi, Mhasibu Rose Kijaka, M/Kiti wa kamati ya  mapokezi Peter Mosha na  Msimamizi wa ujenzi huo Israel Mayage.

Wengine ni aliyekuwa Afisa manunuzi wa Chuo hicho Henry Matei ambaye alihamishiwa Chuo cha Ualimu Monduli na kuwa Waziri ameelekeza arudishwe chuoni hapo na asimamishwe kazi mara moja.


Muonekano wa Jengo la Utawala la Shule ya Wanafunzi wenye mahitaji maalumu inayojengwa katika Chuo cha Ualimu Patandi.

Pia Waziri amemuagiza Katibu Mkuu Dkt. Akwilapo kumpunguzia majukumu ya kazi Mkuu wa Chuo cha Patandi Lyana Mbaji kutokana na kuwa ni mgonjwa na badala yake ateuliwe Mkuu mwingine aweze kuendelea na majukumu katika Chuo hicho.

Mpaka sasa tayari Wizara imekwishatoa kiasi cha shilingi Bilioni 2.3, mradi utakapokamika kiasi ha sh. 2.56 zitakuwa zimetumika.
Muonekano wa Bwalo la Wanafunzi wenye mahitaji maalumu linalojengwa katika Shule ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika Chuo cha Ualimu Patandi, Arumeru mkoani Arusha.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni