Ijumaa, 15 Februari 2019

WAZIRI NDALICHAKO AAHIDI USHIRIKIANO MAANDALIZI YA ZANZIBAR JAMBO REE


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia ambaye pia ndiye  Rais wa Skauti Profesa Joyce Ndalichako amewaahidi ushirikiano Viongozi wa Chama cha Skauti Tanzania katika kufanya maandalizi ya sherehe za  Zanzibar Jambo Ree inayotarajiwa kufanyika mwezi wa sita mwaka huu Visiwani Zanzibar..

Waziri Ndalichako amesema hayo wakati alipokutana na kuzungumza na Viongozi wa  Juu wa Skauti Tanzania kwa lengo la kumuelezea  Waziri hatua iliyofikiwa katika maandalizi ya sherehe hizo.

Waziri Ndalichako amewaambia viongozi hao wa skauti kuwa ni vyema wakaliangalia kwa makini pendekezo lao la kutaka kupeleka washiriki 24 Visiwani Zanzibar kutoka kila mkoa wa Tanzania bara kwani namba hiyo itakuwa ni kubwa, na kuzifanya sherehe hizo kuonekana ni za Bara badala ya Zanzibar.


 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na Skauti Mkuu Mwantumu Mahizi na Kamishana Mkuu Grace Joseph jijini Dar es salaam ambapo Waziri amewaahidi viongozi wa skauti ushirikiano katika maaandalizi ya Sherehe za Jambo Ree zinazotarajiwa kufanyika visiwani Zanzibar.



 “Ninawashauri kuangalia kwa undani na makini suala la idadi ya washiriki kutoka Bara kwa kila mkoa washiriki 24, idadi hii ni kubwa na tutawazidi kwa kuwa Zanzibar  ina mikoa michache kuliko sisi na sherehe hizi zitaonekana kuwa ni za Bara na si Zanzibar,” alisema Waziri.

Skauti Mkuu Mwantumu Mahiza alimwelezea Waziri kuwa Chama cha Skauti Tanzania kinatekeleza agizo la Makamu wa Rais alilolitoa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Skauti Dunia na Maadhimisho ya miaka mia moja ya Skauti hapa nchini ya kukitaka chama hicho kufanya sherehe  hizo Visiwani Zanzibar.

Mahiza pia alimtambulisha Kamishna Mkuu mpya Grace Joseph Kado aliyeteuliwa hivi karibuni na kueleza kuwa sasa safu ya uongozi  kwa sasa imekamilika.
Skauti Mkuu Mwantumu Mahizi akisisitiza jambo kwa Rais wa Skauti Tanzania ambaye pia ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako wakati wa kujadiliana kuhusu maandalizi ya sherehe za Jambo Ree zinazotarajiwa kufanyika visiwani Zanzibar.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni