Jumatano, 13 Machi 2019

WIZARA YA ELIMU YAAHIDI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA WADAU WA TEHAMA KUENDELEZA VIPAJI VYA WANAFUNZI

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeahidi kuendelea kushirikiana na Taasisi za Serikali na zisizo za Serikali ambazo zinajihusisha na masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA) kuibua vipaji vya wanafunzi na kuviendeleza.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako wakati wa hafla ya kufunga mafunzo na mashindano ya kitaifa ya wasichana na Tehama yaliyoandaliwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Jijini Dodoma.

Waziri Ndalichako amesema ni vyema vipaji vya wanafunzi washiriki wa mafunzo na mashindano ambavyo vimeibuliwa vikaendelezwa kwa kuwa vinalenga kutumia TEHAMA kutatua changamoto zilizopo katika jamii yetu na kusisitiza kuwa Serikali inahimiza matumizi sahihi ya teknolojia ya habari na mawasiliano kwa maendeleo ya Taifa.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akitoa zawadi kwa mwanafunzi Khatija Saphy kutoka mkoa wa Tabora mmoja kati ya washindi 6 walioibuka  kidedea katika mashindano ya  wanafunzi wa kike na TEHAMA  yaliyoandaliwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa wote jijini Dodoma. 
Kiongozi huyo ameipongeza UCSAF kwa kuandaa mafunzo na mashindano hayo kwa wanafunzi wa kike kutoka shule mbalimbali za umma nchini, ambapo pia amesisitiza kuwa vijana wote wa kike na wa kiume wana vipaji na ni wabunifu wanachohitaji ni vipaji vyao kuibuliwa kwa kupewa fursa na kuendelezwa.

“Niwasihi sana wadau wote, vijana na hususan wanafunzi kuhakikisha mnatumia vema teknolojia ya habari na mawasiliano kwa sababu inaweza kuwakuza kitaaluma, kiuchumi na kijamii kwa ujumla wake kama ikitumika vizuri,” alisema Waziri Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akizungumza  wakati wa hafla ya kufunga mashindano ya kitaifa ya wasichana na TEHAMA yaliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Dodoma, Jijini Dodoma. Amewataka wanafunzi kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika masuala yanayowasaidia kitaaluma.
Amesema nia ya serikali ni kuona mchango wa sayansi, teknolojia na ubunifu unaongeza tija katika uzalishaji hususan katika sekta ambazo zinagusa wananchi walio wengi ikiwemo kilimo, mifugo, viwanda pamoja na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma katika jamii.

“Mnaweza kuona hapa wanafunzi wa kike wametengeneza application ya kutoa huduma kwa mama mjamzito na hayo ni mafunzo ya siku nne tu, je wangeongezewa muda? Hii inaonesha watoto wa kike wanaweza,“ aliongeza Waziri Ndalichako.

Aidha Waziri Ndalichako amewataka watanzania hususan vijana kutumia teknolojia ya habari na Mawasiliano kwenye shughuli za kimaendeleo badala ya kujikita katika mitandao ya kijamii ya facebook na instagram huku akiwaasa wanafunzi kutumia Tehama katika masuala yanayoleta tija badala ya kutumia muda mwingi kuchat vitu visivyo na tija.
Baadhi ya wanafunzi walioshiriki mafunzo na mashindano ya kitaifa ya wasichana na TEHAMA wakifuatilia hotuba ya Waziri wa elimu.
Naye Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, Mhandisi Peter Ulanga amesema Mfuko huo katika mikakati yake imejipanga kuhakikisha inafikisha elimu ya TEHAMA pamoja na kutoa vifaa kwa shule za umma hapa nchini na kwamba hadi sasa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote umekwisha peleka kompyuta katika shule za umma 500 ambapo kila shule imepata kompyuta 5 ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo ya TEHAMA kwa walimu zaidi ya 500.

Mhandisi Ulanga, alieleza kuwa mafunzo na mashindano hayo ni sehemu ya maadhimisho ya kimataifa ya siku ya MTOTO WA KIKE na TEHAMA Duniani yanayoadhimishwa mwezi Aprili kila Mwaka na kuhusisha wanafunzi wa kike toka mataifa mbalimbali. Maadhimisho hayo yaliyoambatana na mafunzo ya siku nne yalikuwa na Kaulimbiu isemayo ‘Kuongeza mipaka na kubadili mitizamo’ na yameshirikisha wanafunzi wa kike zaidi ya 240 kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani ambapo wanafunzi 6 kati yao wameibuka washindi na kuzawadiwa vikombe pamoja na kompyuta na fursa ya kushiriki katika Maadhimisho ya kimataifa yatakayofanyika nchini Ethiopia.


Ulanga aliongezea kuwa UCSAF itaendelea na mpango huo na kuongeza idadi ya washiriki ili kukuza ujuzi na kuhamasisha matumizi sahihi ya TEHAMA miongoni mwa wanafunzi wa kike nchini na kuwashukuru wadau wote walioshiriki kufanikisha maadhimisho hayo mwaka huu, ikiwemo, Vodacom, DIT, UDOM, CBA Bank na TERMET.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa kike walioshiriki mashindano ya kitaifa ya wasichana na TEHAMA yaliyofanyika Jijini Dodoma.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni