Jumatano, 24 Aprili 2019

BARAZA LA WAFANYAKAZI WIZARA YA ELIMU LAKUTANA KUJADILI MWELEKEO WA BAJETI KWA MWAKA 2019/20.


Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Dkt. Filisi Nyimbi amesema serikali ya awamu ya tano imeweka misingi imara itakayowezesha kila mtanzania kupata elimu iliyo bora na yenye tija kwa Taifa ili kufikia malengo ya kuwa na uchumi wa kati kupitia viwanda ifikapo mwaka 2025.

Ameyasema hayo wakati akifungua mkutano wa 26 wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknoojia unaofanyika mkoani Mwanza na kusisitiza kuwa Wizara hiyo imepewa jukumu la kutunga sera, kuandaa na kusimamia miongozo mbali mbali ya Elimu itakayowezesha Elimu inayotolewa nchini kuwa bora.

Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa 26 wa Baraza la Wafanyakazi wakiwa wameshikana mikono wakati wa kiimba wimbo wa “SOLIDARIRY” kuashiria umoja, mshikamano na upendo katika utekelezaji wa majukumu yao
 


Dkt. Nyimbi amesisitiza kuwa ili kutimiza azma ya serikali ya awamu ya tano kila mtumishi ana wajibu wa kufanya kazi kwa bidii na kwa weledi wa hali ya juu.

Dkt. Nyimbi ameipongeza Wizara ya Elimu kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya kujifunzia na kufundishia katika Shule za Sekondari, Vyuo vya Ualimu, Elimu ya Juu, Vyuo vya Ufundi,  na Vyuo vya Maendeleo ya wananchi (FDCs) lengo likiwa ni kuweka mazingira bora ya kielimu katika kuandaa vijana wenye sifa katika kujenga uchumi wa nchi.



Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Dkt. Filisi Nyimbi Akizungumza na washiriki katika Mkutano wa  26 wa  Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambapo watumishi wametakiwa kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia kanuni, taratibu na sheria.


Pia ameipongeza Wizara kwa kuendelea kuimarisha na kuboresha  idara ya Uthibiti Ubora wa shule kwa kununua magari ili idara hiyo iendelee kukagua shule na kutoa ushauri wa kitaalamu  na kitaaluma.

Akizungumza katika mkutano huo Naibu Katibu Mkuu Prof. James Mdoe amesema pamoja na mambo mengine kikao hicho kitapitia utekelezaji wa bajeti kwa mwaka 2018/19 na kujadili mwelekeo wa bajeti kwa mwaka 2019/20.



Mgeni rasmi Dkt. Filisi Nyimbi akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi na  washiriki wa Mkutano wa 20 wa Baraza la Wafanyakazi wakiwa kwenye picha ya pamoja. Kikao kazi hicho kimefanyikia mkoani Mwanza.
 


“Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeendelea kusimamia kikamilifu utekelezaji wa majukumu yake kwa lengo la kuboresha sekta ya Elimu hapa nchini, hivyo niwaase watendaji wote kuendelea kufanya kazi kwa kufauta kanuni, taratibu na sheria zinazosimamia utendaji katika maeneo yenu ya kazi,”alisisitiza Prof. Mdoe.

Mkutano huu umehudhuriwa na wajumbe zaidi ya 120 kutoka Wizara ya Elimu na wajumbe kutoka Chama cha Walimu Tanzania ( CWT ) na Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na  Afya (TUGHE).   Kauli mbiu ya Mkutano huo wa 26 wa baraza la wafanyakazi ni: “Elimu bora na Uwajibikaji wa pamoja ni Chachu ya Maendeleo ya Uchumi wa Viwanda Tanzania”



Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa 26 wa Baraza la Wafanyakazi wakifuatilia hotuba ya  mgeni rasmi wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo unaofanyika Jijini Mwanza



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni