Jumatano, 10 Aprili 2019

SERIKALI YA TANZANIA NA ROMANIA WAKUBALIANA KUSHIRIKIANA KATIKA SEKTA YA ELIMU


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Heshima wa Romania Daniela Gitman pamoja na ujumbe wa Kamati ya Wakuu wa Vyuo Vikuu vya Romania na kukubaliana kushirikiana katika sekta  ya elimu.

Akizungumza na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Ndalichako jijini Dodoma, Balozi Gitman amesema  hii ni mara ya kwanza kwa nchi yake kuingia katika Ukanda wa Afrika Mashariki kwa lengo la kushirikiana katika nyanja mbalimbali za maendeleo.
Balozi Gitman amesema nchi yake imeiteua Tanzania kuwa chimbuko la kuanzishwa kwa  ushirikiano kati Serikali ya Romania na nchi za Afrika Mashariki kwenye maeneo mbalimbali ambapo wanaanza na sekta ya elimu na baadaye wataaangalia sekta za utalii na biashara.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako, Naibu Katibu Mkuu Prof. Prof. James Mdoe, Kaimu Mkurgenzi Elimu ya Juu na Mkurugenzi wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu Dkt. Kipanyula wakiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Heshima kutoka Romania na  Wajumbe wengine.

Katika Kikao hicho wamekubaliana kutoa ufadhili wa masomo ya shahada za juu kwa wahadhiri na wataalamu katika Vyuo Vikuu vya Tanzania katika fani ambazo Umoja wa Wakuu wa Vyuo Vikuu Tanzania utapendekeza kulingana na vipaumbele vya nchi.

Pamoja na kufadhili wahadhiri, Wamekubaliana kupitia Vyuo Vikuu kuanza utaratibu wa kubadilishana uzoefu na utaalamu “fellowships”, ambapo wahadhiri kutoka Tanzania wataenda Romania na Romania kuja Tanzania kwa vipindi vifupi vifupi.

Waziri Ndalichako ameishukuru serikali ya Romania na kuahhidi kushirikiana nao katika kuendeleza sekta ya elimu na kuuwataka Umoja wa Wakuu wa Vyuo Vikuu nchini kuhakikisha wanakamilisha kuandaa makubaliano ya ushirikiano huo pamoja na taratibu za utekelezaji wa ushirikiano huo.

Katika hatua nyingine Romania imetoa fursa ya kufadhili masomo ya Elimu ya Juu kwa wanafunzi 5 katika kila fani itakayopendekezwa kusoma katika Vyuo Vikuu nchini humo. Wizara ya Elimu kwa kushirikiana na vyuo vikuu wataratibu upatikanaji wa wanufaika.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe na  Mkurugenzi wa Elimu Juu Wizara ya Elimu Sayansi na teknolojia na Wakurugenzi wa Wizara hiyo ambapo utakelezaji wa makubaliano hayo unatarajiwa kuanza mara baada ya kusaini makubaliano ya ushirikiano na programu za maunzi kwa wanufaika zinatarajiwa kuanza mwezi Oktoba Mwaka huu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni