Alhamisi, 18 Aprili 2019

WAZIRI NDALICHAKO AZINDUA MACHAPISHO YA LUGHA YA KISWAHILI


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako (Mb) amezindua machapisho ya kitaaluma yaliyoandikwa kwa lugha ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Uzinduzi huo uliofanyika jijini Dar es Salaam ambapo amesema kwa muda mrefu machapisho ya kitaaluma yamekua yakiandikwa kwa lugha ya Kiingereza na kupelekea watanzania wengi kutopata majibu ya tafiti zinazofanywa na wanataaluma hao.

Waziri Ndalichako amewapongeza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa hatua hiyo kubwa ya  matumizi ya  lugha ya Kiswahili katika kuhakikisha maarifa yanawafikia wananchi wote hasa katika kipindi hiki ambapo nchi inapoelekea uchumi wa kati kupitia viwanda.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizindua machapisho ya Kitaaluma yaiandikwa kwa lugha ya Kiswahili, uzinduzi huo umefanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam jijini Dar es Salaam.
Aidha, Waziri  Ndalichako ahimiza watanzania kuchangamkia fursa zilizopo katika lugha ya Kiswahili.

"Nawapongeza wanataaluma kwa kutoa machapisho ya tafiti zao  kwa kutumia Lugha Adhimu ya Kiswahili endeleeni kufanya tafiti zaidi kwa maendeleo ya nchi," amesema Ndalichako.

Akimkaribisha Waziri kuzindua machapisho hayo Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. William Anangisye amempongeza Waziri kwa kuwa mstari wa mbele katika kusimamia elimu nchini.

Prof. Anangisye amesisitiza kuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kitaendeleza kazi yake muhimu ya utafiti kwa ubora wa hali ya juu na kutoa machapisho katika majarida ya kitaaluma yenye hadhi ya juu ya kimataifa na kitaifa.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akionyesha moja ya Chapisho mara baada ya kuzindua machapisho ya Kitaaluma yaiandikwa kwa lugha ya Kiswahili, uzinduzi huo umefanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam jijini Dar es Salaam

Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili, Victor Eliah ameipongeza serikali  chini ya uongozi wa Rais Mhe. Dkt John Pombe Joseph Magufuli kwa jitihada kubwa za kukikuza na kukitumia Kiswahili.

Akiongea kwa niaba ya waandishi wa machapisho mbalimbali ya tafiti Eliah amekishukuru Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kumuwezesha kuandika kitabu kinachohusu Matumizi ya Kiswahili katika Vyombo vya Habari ikiwa  ni juhudi za kuhakikisha jamii inapata kazi za waandishi wa habari katika umahiri wa hali ya juu.

Nae Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Prof. Bonaventure Rutinwa amewataka wananchi kununua na kusoma vitabu mbalimbali ili kujichotea maarifa na kujiendeleza katika lugha hasa ya Kiswahili kwa sababu ina fursa nyingi sana za ajira ndani na nje ya nchi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni