Ijumaa, 21 Juni 2019

NAIBU WAZIRI OLE NASHA ATAKA WATOTO KULINDWA NA KUWEZESHWA ILI WAWEZE KUSHIRIKI FURSA MBALIMBALI ZA ELIMU

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha amesema Serikali  inatambua  na kuthamini umuhimu wa mtoto wa kitanzania na ndio maana imekuwa ikizifanyia kazi haki za msingi za mtoto ili aweze kuishi katika mazingira mazuri ikiwa ni pamoja na kupata elimu. 

Naibu Waziri Ole Nasha ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyoandaiwa na Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF) ambapo amesema watoto wanapaswa kulindwa na kuwezeshwa ili waweze kushiriki katika  fursa mbalimbali zilizopo kwenye elimu. 


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afirika yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam Juni 20, 2019.
 Amesema maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yanatoa fursa ya kujadili changamoto na fursa katika kuhakikisha kuwa haki za mtoto zinalindwa na kwamba  Serikali imefanya jitihada kubwa na za makusudi katika kuhakikisha kuwa watoto wanapata haki zao za msingi katika jamii zetu za kitanzania.


Ole Nasha amezitaja jitihada hizo kuwa ni pamoja na kuridhiwa kwa mikataba mbalimbali ya Kimataifa inayolinda haki za watoto, kutunga  sheria zinazolinda haki za watoto dhidi ya uonevu na ubaguzi wowote na pia imepitisha Sera zinazowalinda na kuwapatia fursa watoto.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akichangia mjadala wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Jitihada nyingine ni pamoja na ujenzi wa shule karibu na makazi ya watu ili kupunguza watoto kutembea umbali mrefu, ujenzi wa mabweni na pia  mafunzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuweka mkazo juu ya stadi za maisha, elimu ya afya ya uzazi na ujinsia katika shule za msingi na sekondari na vyuo vya ualimu.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Ole Nasha ameutaka umma kutambua kuwa jukumu la kuwaendeleza watoto kielimu ni la kila mmoja wetu na kwamba ifahamike kuwa watoto wa kike na wa kiume wote ni sawa, hivyo hatuna budi kuwapunguzia watoto wa kike mzigo wa kazi za nyumbani ili wapate muda wa kujisomea sawa na ilivyo kwa watoto wa kiume.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akipokea risala kutoka kwa mmoja wa watoto walioshiriki Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika Jijini Dar es Salaam.
Siku ya Mtoto wa Afrika huadhimishwa Juni 16 ya kila mwaka ambapo kwa mwaka 2019 maadhimisho hayo Kitaifa yamefanyika Mkoani Geita na yalikuwa na Kauli Mbiu isemayo “Mtoto ni Msingi wa Taifa Endelevu: Tumtunze, Tumlinde na Kumuendeleza.”

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni