Ijumaa, 20 Septemba 2019

SERIKALI KUSHIRIKIANA NA WADAU WA ELIMU KUONDOA CHANGAMOTO DHIDI YA ELIMU KWA MTOTO WA KIKE

Serikali inatambua na kuthamini mchango wa Asasi za Kijamii, ikiwemo HakiElimu, katika kuweka mkazo kuhusu umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike kwa maendeleo ya jamii na taifa kwa jumla.
 
Kauli hiyo ya Serikali imetolewa Jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo wakati wa uzinduzi wa ripoti ya utafiti ya HakiElimu kuhusu changamoto za Elimu ya mtoto wa Kike.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo akikata utepe kuashiria uzinduzi wa ripoti ya Utafiti kuhusu wasichana kushindwa kuendelea na masomo iliyofanyika jijini Dodoma.
Dkt. Akwilapo amesema nia ya Serikali ni kushirikiana na wadau wa elimu ili kuona kuwa vikwazo vyote dhidi ya elimu kwa mtoto wa kike vinapatiwa suluhisho sahihi.

“Ili kufanya maamuzi sahihi, Wizara ninayoiongoza hutumia uthibitisho unaotokana na tafiti mbalimbali zinazofanywa na Wizara yenyewe na wadau wengine wa elimu. Sisi kama watunga sera hatuwezi kufanya kazi kwa ufanisi bila ya kutumia matokeo ya utafiti,” Alisema Dkt. Akwilapo.

Dkt Akwilapo ameipongeza Taasisi ya HakiElimu kwa kuwa mstari wa mbele katika kufanya tafiti mbalimbali ambazo zinatoa mchango mkubwa katika sekta ya elimu.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa ripoti ya Utafiti kuhusu wasichana kushindwa kuendelea na masomo iliyofanyika  jijini Dodoma. Utafiti huo umefanywa na HakiElimu ikiwa ni utekelezaji wa Mpango Mkakati wao katika kumsaidia mtoto wa kike kupata elimu bora.
“Ripoti ya utafiti ninayoizindua leo ni mfano hai wa kile ninachokisema kuhusu mchango wa Sekta binafsi kwani inahusu changamoto zinazosababisha wasichana kushindwa kuendelea na masomo na kuvuka katika hatua nyingine. Utafiti huu unaendana na lengo la Serikali la kuhakikisha kuwa wasichana wanaoandikishwa katika Elimumsingi wanamaliza safari yao ya elimu kwa mafanikio makubwa,” aliongeza Dkt. Akwilapo.

Akizungumzia jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuhakikisha mtoto wa kike anapata elimu Dkt. Akwilapo amesema Serikali imekuja na Sera ya Elimu bila malipo katika ngazi ya Elimumsingi ambayo imewezesha wasichana wengi kuandikishwa katika shule ikiwa ni pamoja na Ujenzi wa mabweni ambayo yamesaidia kuwaweka wasichana karibu na shule na kuepuka vishawishi vya barabarani wakati wa kwenda na kurudi shule.
Baadhi ya Wanafunzi na Wajumbe walioshiriki katika hafla ya uzinduzi wa ripoti ya Utafiti kuhusu wasichana kushindwa kuendelea na masomo wakifuatilia hotuba ya Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo jijini Dodoma.
Jitihada nyingine ni kutunga sheria ambayo inawabana watu wanaotaka kuoa watoto wa shule au kushirikiana nao kimapenzi, na hivyo kuwaharibia masomo kwa kuwapa ujauzito pamoja na kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike.
Mkurugenzi Mtendaji HakiElimu, Dkt. John Kalaghe akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa ripoti ya Utafiti kuhusu wasichana kushindwa kuendelea na masomo iliyofanyika Jijini Dodoma.
Naye Mkurugenzi Mtendaji HakiElimu, Dkt. John Kalaghe amesema azma ya kufanya utafiti huu imechagizwa na kampeni ya Elimu ya mtoto wa kike ambayo HakiElimu inaifanya.  Amesema kampeni hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa mwaka 2017 hadi 2021 ambao wamejiwekea na umejikita katika kushirikiana na Serikali pamoja na wadau mbalimbali kuhakikisha kwamba watoto wa kitanzania wakiwemo watoto wa kike wanapata elimu bora itakayowawezesha kukabili changamoto katika maisha yao na kusaidia ujenzi wa Taifa letu.

“HakiElimu tunatilia mkazo katika kuhamasisha utolewaji wa elimu jumuishi yenye ubora na usawa pamoja na elimu kwa watoto wa kike ikiwa ni pamoja na kupunguza au kuondoa kabisa unyanyasaji wa watoto shuleni na nje ya mipaka ya shule,” Alisema Dkt. Kalaghe.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa hafla ya uzinduzi wa ripoti ya Utafiti kuhusu wasichana kushindwa kuendelea na masomo iliyofanyika Jijini Dodoma.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni