Alhamisi, 17 Oktoba 2019

WAZIRI NDALICHAKO ATAKA MKUU WA SHULE KASANGEZI KUHAMISHWA


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako ametilia shaka matumizi ya fedha za serikali zaidi ya shilingi milioni mia tano zilizotolewa kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa shule ya sekondari Kasangezi iliyopo wilayani Kasulu mkoani Kigoma.

Akizungumza mara baada ya kukagua utekelezaji wa mradi huo waziri Ndalichako amesema shule hiyo imepatiwa zaidi ya shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 4, mabweni 4 yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 80 katika kila moja, matundu ya vyoo 10, bwalo pamoja na ukarabati wa maabara.

Ndalichako amesema  kazi iliyofanyika haiendani na fedha iliyotolewa kutokana na miundombinu hiyo kujengwa chini ya Kiwango.

“Milango ya madarasa na hata ya mabweni mmetengeneza kwa mbao laini tofauti na BOQ pamoja na kuwa laini ina uwazi hii nataka itolewe, tazama sakafu imeshaharibika hapa hata mwaka haujaisha mabweni mliambiwa ya watu themanini mmejenga ya watu sitini"
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akiangalia mlango wa darasa ambao umetengenezwa kwa mbao laini kinyume cha taratibu katika shule ya sekondari Kasangezi

Kufuatia hali hiyo ndalichako ameagiza kuwa ujenzi wa mabweni urudiwe kwa kuzingatia BoQ na ameaguza ujenzi huo uwe umekamilika ifikapo desemba.

"Nitakuja mwenyewe mwezi wa kwanza kukagua kama hayo yatakuwa hayajatekelezwa mengine yatafuata,” amesema waziri Ndalichako.

Aidha waziri Ndalichako amemuagiza  Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kasulu Mhandisi  Godfrey Kasekenya  kumuondoa  mara moja shuleni hapo mkuu wa shule hiyo kwa kushindwa kusimamia  vizuri kazi hiyo na hivyo kuisababishia hasara serikali.

“Kwanza ujenzi wa mara ya kwanza hata matofali hukununua ulichukua kwenye benki ya wananchi na tayari nilikuwa nimeleta fedha sasa kwanini hukujiongeza hata ukarekebisha ofisi ya Mkuu wa Shule ambayo iko katika hali isiyoridhisha vitu vingine ni kudhalilisha Serikali, Mkurugenzi muahamishe huyu katika shule hii,” alisema waziri Ndalichako.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako akikagua maendeleo ya  ujenzi wa moja ya bweni katika shule ya sekondari Kasangezi iliyoko Halmashauri ya wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma.

Waziri Ndalichako pia ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na  Rushwa (TAKUKURU) wilayani Kasulu   kufuatilia muenendo wa upatikanaji wa madawati miamoja themanini yaliyonunuliwa katika mradi huo kama yametimia na yamenunuliwa kwa kufuata utaratibu.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanali Saimon Anange amekiri kuwepo uzembe katika kusimamia miradi hiyo na kumuhakikishia waziri Ndalichako kuwa ofisi yake itafanyia kazi maelekezo yote aliyoyatoa katika ziara hiyo.

Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolijia Prof. Joyce Ndalichako yupo mkoani Kigoma Kwa ziara ya Kikazi akikagua miradi ya elimu inatekelezwa kupitia fedha za Programu ya lipa kwa matokeo EP4R.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akikagua mlago wa darasa ambao umetumia mbao laini tofauti na maelekezo katika shule ya sekondari Kasangezi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni