Jumatatu, 27 Januari 2020

WALIMU NA WAKUFUNZI 140 WENYE MAHITAJI MAALUM WANAPATA MAFUNZO YA TEHAMA

Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Awamu ya tano imetumiza Sh.bilioni 5.9 kununua na kusambaza vifaa maalum vya kielimu na saidizi katika shule za msingi na sekondari, zinazopokea  wanafunzi wenye mahitaji maalum nchini.

Hayo yamesemwa Jijiji Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo wakati wa ufunguzi wa  mafunzo ya ya siku 10 ya Tehama na Teknolojia saidizi kwa wakufunzi na walimu wenye mahitaji maalumu wanaofundisha shule za sekondari  ili kuwajengea uwezo wa matumizi ya Teknolojia hiyo katika utekelezaji wa majukumu yao.

Kiongozi huyo ametaja vifaa vilivyonunuliwa na kusambazwa kuwa ni Shime sikio (Hearing Aids) kwa ajili ya wanafunzi wenye baki ya usikivu, mashine za kuandikia maandishi ya breli na Vivunge vyenye fimbo nyeupe (Braille kit)kwa ajili ya wasioona.

Alisema  kuwa katika kipindi cha miaka minne ya Rais John Magufuli,  pia Serikali imefanya upanuzi na ukarabati wa Chuo cha Ualimu Patandi ili kuongeza udahili wa walimu kutoka walimu 300 na kufikia walimu 450 kwa mwaka wa masomo 2019/2020.

Pia imejenga  shule ya sekondari ya mfano katika chuo hicho yenye uwezo wa kudahili wanafunzi 640 wenye mahitaji maalum.

Aidha, shule hiyo  itasaidia wanachuo kufanya mazoezi ya kufundisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu kwa vitendo na kuwa mahiri katika fani wanazosomea.

“Mnaweza kuona jitihada ambazo serikali imekuwa ikizifanya nitoe wito kwa familia, na wadau wa maendeleo kuendelea kuona umuhimu wa kuchangia juhudi za serikali katika kuwapatia huduma stahihiki wanafunzi wenye mahitaji maalum ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika ujifunzaji, " alisema Katibu Mkuu Akwilapo

Dkt. Akwilapo amesema ushiriki wa jamii ni muhimu sana  kwani masuala ya watu wenye ulemavu ni mtambuka hivyo jitihada za pamoja zinahitajika ili kufikia malengo yaliyoanishwa katika miongozo ya kitaifa na kimataifa.

Akizungumzia mafunzo ya TEHAMA na Teknolojia saidizi yanayotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Katibu Mkuu huyo amesema  yanalenga kuwajengea uwezo wakufunzi na walimu wa Sekondari wasioona, viziwi na wenye ualbino  katika matumizi ya TEHAMA na teknolojia saidizi ili  kuboresha ufundishaji katika vyuo vya ualimu na shule za sekondari nchini.

Aliongeza kuwa mafunzo hayo yatawapatia maarifa na stadi kuhusu mfumo, vipengele na utendaji kazi wa kompyuta, utumiaji wa program saidizi za sauti na kukuza maandishi katika kompyuta, kupata stadi za matumizi ya mitandao katika kutafuta na kutuma taarifa mbalimbali katika tovuti na barua pepe pamoja  na kutumia kikamilifu maudhui ya kielektroniki katika ufundishaji na ujifunzaji.

Kwa upande wake Kaimu Kamishna wa Elimu Paulina Mkonongo  alisema, kufanyika kwa mafunzo hayo ni mkakati endelevu wa Serikali kuhakikisha elimu bora inatolewa kwa makundi yote ikiwemo kuimarisha mafunzo kazini kwa kundi hili maalum.

Awali Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu Maalumu Greyson Mlanga ameeleza kuwa mafunzo hayo yana jumla ya washiriki  140 wenye mahitaji maalumu, wakiwemo viziwi 37, wasioona na wenye uoni hafifu 103  kutoka vyuo vya ualimu vya serikali na walimu wa shule za sekondari nchini.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa mafunzo, Mkufunzi kutoka Chuo cha Ualimu Morogoro Godfrey Omary amesema anaishukuru Serikali kwa kutoa mafunzo hayo kwa kuwa yanakwenda vikwazo katika vya kiutendaji lakini pia itapunguza utegemezi na hivyo kuongeza ufanisi.

Mafunzo kuhusu matumizi ya TEHAMA na Teknolojia saidizi kwa walimu na wakufunzi na wenye mahitaji maalumu yameanza leo na yanatarajiwa kuhitimishwa  Februari 05, 2020.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni