Alhamisi, 30 Novemba 2017

Chuo Kikuu Huria chatakiwa kupanua wigo wa udahili.


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kassim Majaliwa amekitaka Chuo kikuu Hiria nchini kuhakikisha kinaongeza ubora wa utoaji Elimu na kupanua wigo wa udahili kwa wanafunzi wa chuo hicho.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo wakati wa mahafali ya 33 ya Chuo hicho ambayo yamefanyikia mkoani Singida na kusisitiza kuwa Umuhimu wa Chuo kikuu huria uko bayana katika kuhakikisha malengo ya serikali ya kutekeleza sera ya uchumi wa viwanda inafikiwa kupitia wataalamu wanaomaliza chuoni hapo.

Waziri Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya Tano inatambua na inaunga mkono juhudi zinazofanywa na uongozi wa chuo hicho huku wakisisitizwa kuzingatia vigezo, taratibu za utoaji wa Elimu iliyo bora ili wapatikane wataalamu ambao ni bora kwa maslahi ya Taifa.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema Serikali inatambua mchango wa Chuo hicho katika kipindi cha miaka 25 ambapo kimekuwa kikitoa  Elimu katika masafa ya mbali hali ambayo inahitaji mwanafunzi kuwa na nidhamu ya hali ya juu ili kifikia malengo.

Kutokana na juhudi hizo Waziri Ndalichako ameahidi Serikali itaendelea Kuimarisha miundombinu ya Tehama ili Elimu hiyo ya masafa iweze kuwafikia watu wengi zaidi.
Waziri Ndalichako amewataka wahitimu kutumia vyema ujuzi na kuhakikisha wanaimarisha utendaji kazi katika serikali na hata Sekta binafsi.

Pia amewataka wahitimu kujenga nadhani pamoja na kuwa na ari katika  uwajibikaji ikiwa ni pamoja na kuwa mabalozi katika Shughuli ambazo watakuwa wanazifanya.






Jumatatu, 27 Novemba 2017

Waziri Ndalichako: Watendaji wajibikeni acheni kulipana stahili ambazo hazifuati miongozo na nyaraka za Serikali

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amezitaka Taasisi zilizochini ya Wizara yake kuwajibika katika nafasi zao za uongozi na siyo kusubiria mpaka kiongozi wa juu aibue changamoto zinazojitokeza katika maeneo yao.

Waziri Ndalichako amesema hayo leo mkoani Morogoro wakati wa Kikao kazi kilichohusisha  Menejimenti ya Wizara na Taasisi zake cha kujadili na kujengeana uwezo kuhusu namna  bora ya kubaini na  kukabiliana na viashiria hatarishi katika maeneo ya kazi.(Risk Identification and Risk Managment).
Waziri Ndalichako amesema kupitia kikao kazi hicho watendaji wataweza kujifunza na kubaini mapema viashiria ambavyo vitaonekana kukwamisha utekelezaji wa mipango ya wizara.
"lengo  hapa ni kuzuia madhara badala ya kusubiri madhara yatokee, hivyo kupitia kikao kazi hiki watendaji watajifunza kwa lengo la kuzuia na kutekeleza malengo ya Wizara kama yalivyokusudiwa,"amesema Waziri Ndalichako
Waziri Ndalichako pia amezitaka Taasisi na Watendaji wa Wizara hiyo kuanzia leo kuacha mara moja kulipana stahili ambazo hazifuati miongozo na nyaraka za serikali.
Profesa Ndalichako ametaja baadhi ya stahili ambazo zimekuwa zikilipwa bila kufuata taratibu na miongozo hiyo kuwa ni pamoja na posho za kujikimu, Nyumba,  umeme na simu.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Elimu ,  Sayansi na Teknolojia Dkt.  Leonard Akwilapo amesema mkutano huo umelenga kuondoa viashiria hatarishi ambavyo vimekuwa vikikwamisha ufanisi katika utendaji kazi wa wizara na kuwataka washiriki wa mkutano huo kuandaa mpango mkakati wa kuweza kutambua mapema viashiria hatarishi na kuvifanyia kazi ili kufikia malengo  ya wizara.
Kikao kazi hicho ambacho kimeanza leo kitahusisha pia  Wakurugenzi wasaidizi, waratibu wa miradi na wasaidizi wa miradi, wathibiti ubora wa shule kanda, wakuu wa vyuo vya Elimu ya Ualimu, na watumishi kutoka kila Idara wa wizara hiyo.



Rais Magufuli azindua hospitali ya Mloganzila

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amezindua rasmi hospitali ya Taaluma na Tiba ya chuo kikuu cha afya na sayansi shirikishi MAMC, kilichopo wilaya ya Ubungo mkoani pwani ambapo amewataka Wakala wa Majengo ya Serikali (TBA) kuhakikisha wanakamilisha mara moja ujenzi wa mabweni, madarasa na kumbi za mihadhara katika Chuo hicho.

Rais Magufuli ametoa rai hiyo wakati wa uzinduzi wa hospitali hiyo ambapo amesema  tayari serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 13 kwa ajili ya ujenzi huo na kuwa Kati ya fedha hizo tayari  kiasi cha shilingi bilioni Nne kimelipwa kwa TBA  ili kuanza ujenzi huo na kwamba ujenzi utakapokamilika utawezesha udahili wa wanafunzi 15,000 wa afya na tiba kwa mara moja tofauti na ilivyokuwa awali wanafunzi 4500 Pekee ndiyo walioweza kudahiliwa. 

Rais Magufuli pia ameitaka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknojia na wizara ya Afya kushirikiana kwa pamoja ili kuhakikisha hospital hiyo inatekeleza majukumu yake kwa weledi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Wakati wa uzinduzi huo Rais Magufuli amesifu na kupongeza jitihada zilizofanywa na Serikali ya awamu ya Nne chini ya uongozi wake Rais mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete za kuhakikisha eneo la ujenzi linapatikana na ujenzi unafanyika na hatimaye wananchi kupata huduma za afya.

Naye Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia profesa Joyce Ndalichako amesema uwepo wa Chuo hicho chenye mitambo na vifaa vya kisasa kutalisaidia Taifa kupata wataalamu wenye uwezo ambao itsaidia kuondoa changamoto ya uhaba wa wataalnu wa afya hapa nchini.


Ijumaa, 24 Novemba 2017

Dkt. Akwilapo awataka wahitimu wa ADEM kusimamia kanuni na taratibu katika utendaji kazi.

 Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leornard Akwilapo amewataka wahitimu wa kozi za Uongozi na Usimamizi wa Elimu zinazotolewa na Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) kuhakikisha wanasimamia utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka(2014), Sheria, Kanuni na Taratibu za Elimu ili kupunguza migogoro shuleni

Katibu Mkuu ameyasema hayo katika mahafali ya Ishirini na tano (25) yaliyofanyika katika Chuo hicho kilichopo Bagamoyo Mkoani Pwani ambapo amewataka ADEM  kuendelea kusimamia utekelezaji wa Mtaala kwa ufanisi, kutoa takwimu sahihi za shule, kupanga mipango ya maendeleo ya shule inayotekelezeka, kusimamia fedha za elimu bila malipo kwa ufanisi.

Eneo lingine ambalo Katibu Mkuu ametaka litiliwe mkazo ni    pamoja na kudhibiti nidhamu za wanafunzi mara warudipo katika vituo vyao vya kazi.

Dkt. Akwilapo amesema mafunzo ya uongozi na usimamizi wa Elimu pamoja na Ukaguzi wa Shule ni muhimu katika kuwapa uwezo walimu na viongozi wa elimu kufanya kazi zao kwa weledi, ufanisi na kwa kujiamini zaidi hususani katika kipindi hiki cha maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia.

Amewataka wahitimu kuwa chachu ya mabadiliko katika Uongozi na Utawala Bora pamoja na  Uthibiti Ubora wa Shule nchini kwa kutumia ujuzi, maarifa, stadi na mbinu mpya walizozipata katika mafunzo ikiwa ni pamoja na   maarifa waliyoyapata kuyaeneza kwa walimu ambao hawajapata fursa ya kupata mafunzo hayo.





Chuo Kikuu Ardhi chaadhimisha miaka 10

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Majaliwa kassim Majaliwa amekitaka Chuo Kikuu cha Ardhi nchini kuendelea kutekeleza mpango mkakati waliojiwekea ili kufikia malengo yanayo kusudiwa na Taifa.

Waziri Mkuu  Majaliwa ameyasema hayo wakati wa maadhimisho ya miaka 10 ya chuo hicho ambapo amekitaka , Chuo hicho kuwa na kamapuni itakayosimamia ujenzi katika maeneo mbalimbali hapa nchini na siyo jina la Chuo kutumika vibaya na kuratibu sifa ya Chuo.
Waziri Majaliwa amesema  Chuo hicho kimekuwa kikiisaidia serikali kujenga majengo yenye viwango kwa garama nafuu, hivyo amezitaka taasisi za serikali kukitumia Chuo hicho katika ujenzi wa majengo mbalimbali.

 Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema Chuo kikuu cha Ardhi kimekuwa kikifanya vizuri katika ujenzi, usanifu wa majengo na kwa kutambua kazi ya Chuo hicho  tayari Wizara imetoa zaidi ya bilioni 2 kwa ajili ya ujenzi wa vyuo vya Ualimu, na shule.
Baada ya kukamilika kwa mkutano huo, Waziri Ndalichako alikutana na wanafunzi wa Chuo hicho kwa ajili ya kusikiliza changamoto mbalimbali ambapo wanafunzi walimweleza Waziri kuwa hadi sasa hawajaingiziwa mikopo yao kwa kile kilichoelezwa kuwa wanafunzi bado hawajafungua Akaunti, na ndiyo Wizara alipohitaji maelezo kutoka kwa Afisa mikopo majibu ambayo waziri hakuridhika nayo na ndiyo alipoomba maelezo.

Hata hivyo kutokana na maelezo ambayo hakuridhika nayo,Waziri aliamua kuondolewa mara moja kwa afisa mikopo katika Chuo hicho.


Jumanne, 21 Novemba 2017

China na Tanzania kuendelea kushirikiana katika Sekta ya Elimu

Jamhuri ya Watu wa China imesema itaendela kuisaidia Tanzania katika sekta ya Elimu kwenye eneo la Elimu ya Juu, utoaji wa mafunzo ya Ufundi pamoja na kusaidia garama za uchapishaji wa vitabu vya masomo ya Sayansi kwa ajili ya shule za  msingi na Sekondari.

Kauli hiyo imetolewa na Balozi wa Jamuhuri ya watu wa China nchini Tanzania Wang Ke wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia  Profesa Joyce Ndalichako katika ofisi ndogo zilizopo jijini Dar es Saalam.

Katika mazungumzo yao Waziri Ndalichako amesema garama za uchapaji wa Vitabu ni kubwa hivyo ni vyema Wizara ikawa na mitambo yake ya kuchapia vitabu ambayo itakuwa endelevu suala ambalo Balozi Wang Ke  amekubaliana nalo na kuitaka Wizara kuandaa maombi ya mashine hiyo ili ubalozi uweze kufanyia kazi.


Jumatatu, 20 Novemba 2017

Waziri Ndalichako: Ili shule isajiliwe lazima ikidhi vigezo

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema ili shule isajiliwe lazima iwe imekidhi vigezo ikiwa ni pamoja na kuwa na madarasa ya kutosha, nyumba za walimu, ofisi za walimu, matundu ya vyoo, pamoja na maabara endapo shule itakuwa ni ya Sekondari.

Waziri Ndalichako ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi wa halmashauri ya Mbulu iliyopo mkoani Manyara ambapo amesema ni kweli serikali inahitaji ziwepo shule nyingi ambazo zinavigezo, siyo kuwa na shule ambazo hazina vigezo.

"Shule za nyasi katika Serikali hii ya awamu ya tano zitabaki kuwa historia kwa kuwa serikali inajenga na kuboresha miundombinu ya kujifunzia na ile ya kufundishia, sasa ili shule isajiliwe lazima iwe imekidhi vigezo siyo bora shule bali tunahitaji shule zilizobora na zenye viwango vinavyokubalika" amesema Waziri Ndalichako.

Waziri Ndalichako amesema   kazi ya usajili ni nyepesi sana ambayo haichukui muda mrefu endapo vigezo vinakuwa vimetimia,  lakini kazi kubwa ni kuhakikisha miundombinu bora inayokubalika inakuwepo ili shule iweze kusajiliwa.

 Hivyo amewasihi wadau wote wa Elimu kuhakikisha shule zinapojengwa zinazingatia na kukidhi  vigezo kabla ya kusajiliwa.