Jumatano, 9 Mei 2018

DK. SEMAKAFU AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA UNICEF


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Ave Maria Semakafu leo amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe kutoka UNICEF kwa lengo la kujengeana uelewa wa pamoja juu ya kile wanachokitekeleza kuhusuiana na Sekta ya Elimu.

Mazungunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Wizara Jijini Dodoma ambapo wote kwa pamoja wamekubaliana kuimarisha mawasiliano ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu katika sekta hiyo.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Avemaria Semakafu akisisitiza jambo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Timu ya Ujumbe kutoka UNICEF juu ya namna bora ya kutekeleza majukumu ya kielimu katika Sekta hiyo.

Shirika la Kimataifa la kuhudumia watoto UNICEF wanatekeleza shughuli za kielimu katika mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe, Songea, Kigoma na Tabora kwa kutoa mafunzo kwa waratibu Elimu Kata, mafunzo kwa walimu kazini kuhusu Elimu Jumuishi, lishe, uongozi na utawala kwenye Elimu. 


Kikao hicho pia kimejumuisha wajumbe kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI). 
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Avemaria Semakafu na Timu ya Ujumbe kutoka UNICEF, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) wakiwa katika mazungumzo ya namna bora ya kutekeleza shughuli za kielimu za Sekta hiyo.





WAZIRI NDALICHAKO: MAABARA YA KISASA INAYOJENGWA TANZANIA KUDHIIBTI MIONZI NCHI ZA AFRIKA.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako Leo ametembelea na kukagua hatua za mwisho za usimikaji wa vifaa mbalimbali ndani ya maabara ya kisasa ya Kuhakiki vifaa vinavyopima mionzi katika Tume ya nguvu za Atomiki- TAEC iliyopo mkoani Arusha.

Akizungumza mara baada ya kutembelea maabara hiyo Waziri Ndalichako amesema serikali imejenga maabara hiyo ya kisasa ili kudhibiti masuala ya mionzi kwa nchi za Afrika.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akipokea maelezo kuhusu usimikaji wa vifaa vya kisasa katika maabara ya nyuklia kwenye Tume ya nguvu za Atomiki iliyoko mkoani Arusha.

Alisema maabara hiyo ambayo sasa ipo katika hatua za kufungwa vifaa mbalimbali vya kisasa itawezesha nchi mbalimbali kuja kujifunza namna ya kupima masuala mbalimbali ya mionzi.

Waziri Ndalichako amesema kuwa hadi sasa serikali imeshatoa kiasi cha sh. bilioni 2.38 huku Umoja wa Ulaya (EU) ikitoa vifaa vyenye thamani ya sh.  bilioni 11.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akiangalia kwa karibu moja ya kifaa kilichosimikwa kwa ajili ya upimaji wa mionzi kwenye maabara ya kisasa ya nyuklia kwenye Tume ya nguvu za Atomiki, TAEC mkoani Arusha.

Ijumaa, 4 Mei 2018


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA

Anuani ya simu “ELIMU”
Simu: 026  296 35 33
Baruapepe:  info@moe.go.tz
Tovuti: www.moe.go.tz




  
Chuo cha Masomo ya  Biashara na Sheria,
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Jengo Na. 10,
S. L. P. 10,
40479 DODOMA          

Tarehe:  4 Mei, 2018

TAARIFA KWA UMMA
Kumekuwa na taarifa za upotoshaji ambazo zinasambaa kwenye mitandao ya kijamii, ambazo zinaonesha dosari na makosa katika vitabu. Mojawapo ni picha inayoelezea viungo vya mwili wa mwanadamu na nyingine iko katika Kitabu cha Kiingereza chenye maneno yanayosomeka “The Big City of Tanzania”.
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inapenda kuutarifu umma kuwa kitabu kinachosambazwa kinachoelezea viungo vya mwili wa mwanadamu si chapisho la Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na wala si miongoni mwa vitabu ambavyo vimesambazwa kwenye shule. Kitabu hicho hakina uhusiano wowote na wala hakifanani na vitabu ambavyo vimechapishwa hivi karibuni na TET.
Aidha, kuhusu kitabu cha Kiingereza, hilo ni chapisho la mwaka 2016 ambalo limefanyiwa marekebisho katika chapisho la mwaka 2018.
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inawasihi watanzania kupuuza taarifa hizo ambazo siyo za kweli na zina nia ya kupotosha na kuleta usumbufu kwa jamii. Wizara pia inatumia fursa hii kuwakumbusha wananchi kuzingatia Sheria za Matumizi ya Mitandao na kutambua kuwa kutoa taarifa za uongo ni kosa la jinai.
                                                  Imetolewa na:      
Mwasu Sware
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
04/05/2018

Jumanne, 24 Aprili 2018

NAIBU WAZIRI OLE NASHA AFUNGA MKUTANO WA BARAZA LA WAFANYAKAZI


·        ASISITIZA UWAJIBIKAJI MAHALI PA KAZI


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha amewataka Wafanyakazi wa Wizara hiyo kufanya kazi kwa kufuata kanuni, taratibu  ikiwa ni pamoja na kuwa na ushirikiano miongoni mwao ili kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. William Ole Nasha akizungumza na wajumbe wa Mkutano wa 25 wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Mkutano huo wa siku mbili umehitimishwa leo  Mkoani Morogoro.

Naibu Waziri huyo ametoa kauli hiyo wakati akifunga mkutano wa 25 wa baraza la wafanyakazi ambapo amesisitiza kuwa mkutano huo upo kisheria na kuwa unasaidia kuainisha haki za Wafanyakazi pamoja na Wajibu wao katika utumishi wa Umma.
Viongozi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wakiwa wameshikana mikono kuonesha umoja wao wakati wa  kufunga Mkutano wa 25 wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo uliofanyika mkoani Morogoro.

Mheshimiwa Ole Nasha amewataka Wafanyakazi hao kuhakikisha Elimu inayotolewa hapa nchini inakuwa bora kwa kuwa Elimu ndiyo msingi pekee wa kufikia Uchumi wa viwanda.
Wajumbe wa Mkutano wa 25 wa Baraza la Wafanyakazi wa wizara  wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia wakati wa kufunga Mkutano wa baraza la Wafanyakazi mkoani Mkoani Morogoro.

Pia amewataka makatibu wakuu wa Wizara hiyo kushughulikia kikamilifu maazimio yote yalifikiwa katika mkutano huo wa siku mbili wa baraza la Wafanyakazi kabla ya kufanyika kwa mkutano mwingine wa baraza hilo unaotarajiwa kufanyika mapema Oktoba mwaka huu.


Kauli mbiu ya mkutano wa baraza hilo inasema: “Elimu Jumuishi, Sayansi na Teknolojia ni msingi wa Maendeleo, Endelevu ya Uchumi wa viwanda Tanzania.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe akizungumza na wajumbe wa mkutano wa 25 wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (hawapo pichani), wakati wa kufunga mkutano huo uliofanyika Mkoani Morogoro amabye amesisitiza kuwa jukumu la Wizara hiyo ni kuweka viwango vya ubora vya Elimu.

Jumatatu, 23 Aprili 2018

BARAZA LA WAFANYAKAZI WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA WAKUTANA MKOANI MOROGORO


·         WAJADILIANA NAMNA YA KUFIKIA UCHUMI WA VIWANDA

Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Clifford Tandari ameishauri Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kusomesha vijana wengi katika fani ya ufundi ili kupata wataalamu watakaofanya kazi katika viwanda ili kuendana na sera ya serikali ya awamu ya Tano ya kuwa na uchumi wa Kati na wa viwanda ifikapo mwaka 2015.

Tandari amesema hayo Mkoani Morogoro wakati akifungua Mkutano wa 25 wa Baraza la wafanyakazi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na kusisitiza kuwa Serikali inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli imeweka misingi imara itakayowezesha kila Mtanzania kupata Elimu bora na yenye tija kwa Taifa ili kufikia malengo ya Taifa.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Clifford Tandari akizungumza na wajumbe wa Mkutano wa 25 wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia mkoani Morogoro. 

Akizungumza na baraza hilo la Wafanyakazi Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Leonard Akwilapo amesema kufanyika kwa baraza hilo ni matokeo ya utekelezaji wa Sera ya kuwashirikisha wafanyakazi katika uongozi wa pamoja mahali pa kazi na kuwa mkutano huo pia utapitia na kujadili utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia mwaka 2017/18 na mwelekeo wa bajeti ya mwaka 2018/19.


kwa upande wake Katibu wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo Gerald Mweli amesema Baraza hilo ndio chombo cha juu kabisa cha sheria ya majadiliano kazini kinachojumuisha wafanyakazi wote kujadiliana kwa pamoja mafanikio, changamoto na kuweka mipango ya namna ya kutatua changamoto zinazowakabili.
Viongozi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wakiwa wameshikana mikono kuonesha umoja wao wakati wa Mkutano wa 25 wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo.

Mkutano huo wa siku mbili ulioanza leo utakamalizika kesho ukiwa na kauli mbiu inayosema “Elimu Jumuishi, Sayansi na Teknolojia ni Msingi wa maendeleo Endelevu ya Uchumi wa Viwanda Tanzania".

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Leonard Akwilapo akizungumza na wajumbe wa mkutano wa 25 wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (hawapo pichani), ambapo amesisitiza suala la Umoja, Upendo na ushirikiano mahali pa kazi. (hawapo pichani)

Jumamosi, 21 Aprili 2018

KIBAHA SEKONDARI KINARA WA INSHA, SHULE NYINGINE ZATAKIWA KUJIFUNZA KUTOKA KWAO


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Ave Maria Semakafu amezitaka Shule za Sekondari nchini ambazo zimekuwa zikishindwa katika mashindano ya insha za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za kusini mwa Afrika SADC kujifunza kupitia shule ambazo zimekuwa zikifanya vizuri.

Dkt. Semakafu ameyasema hayo mjini Dodoma wa wakati hafla ya kuwazawadia washindi wa insha hizo kwa mwaka 2017 ambapo amesema ni vema kukawa na  utaratibu wa kuzikutanisha shule hizo mara moja kwa mwaka ili kujadiliana mbinu mbalimbali zitakazowawezesha kufanya vizuri katika mashindano hayo.

Semakafu amesema ushindi huu ni dhahiri kuwa Elimu  inayotolewa nchini  ni Elimu bora na diyo maana wanafunzi wa kitanzania wameweza kushinda tuzo na kuongoza  katika ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Nchi za kusini mwa Afrika.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Ave Maria Semakafu akimkabidhi zawadi ya fedha mshindi wa Jumla wa Insha za Jumuiya ya Afrika Mashariki Michael Msafiri kutoka Shule ya Sekondari Kibaha iliyopo Mkoni Pwani.

Afisa Elimu Mkuu wa sekretaieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki James Otieno kauli aliunga mkono  kauli hiyo kwa kusema kuwa Elimu nchini Tanzania ni bora kwa Nchi za ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwasababu wanafunzi kutoka Tanzania wamekuwa wakifanya vizuri katika mashindano hayo.


Kwa upande wake Mwanafunzi bora wa mashindano ya insha hizo kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Michael Msafiri kutoka Shule ya Sekondari Kibaha ndiye atakuwa mwakilishi wa washindi wote katika Mkutano Mkuu wa Wakuu wa nchi za Jumuiya hiyo utakaofanyika baadae mwaka huu mkoani Arusha.

Kaimu Mratibu wa mashindano hayo Salum Salum kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia amesema mshindano haya huanza mara baada ya kikao cha wakuu wa Nchi wanachama kutoa azimio la mwaka na kwamba mada zinazoshindanishwa huzingatia makubaliano ya wakuu wa nchi.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Ave Maria Semakafu akikabidhi zawadi kwa mwanafunzi Anord Matungwa kutoka shule ya Sekondari Kagemu mkoani Kagera aliyeshinda kutoka kundi la shule zenye mazingira magumu.

Jumatano, 18 Aprili 2018

WAZIRI NDALICHAKO AZINDUA JENGO LA GHOROFA 10 DIT • AITAKA TAASISI HIYO KUTUNZA MIUNDOMBINU

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako leo amezindua Jengo la kufundishia la ghorofa 10 katika Taasisi ya Teknolojia  Dar es salaam- DIT – Teaching Tower Complex.

Akizungumza mara baada ya kutembelea na kukagua jengo hilo amesema kuzinduliwa kwa jengo hilo kutasaidia kuongeza udahili wa wanafunzi kwa kuwa jengo hilo linauwezo wa kuchukua wanafunzi zaidia ya Mia Tisa kwa mara moja.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako azindua Jengo la ghorofa 10 DIT na ameitaka Taasisi hiyo kutunza miundombinu kwa kuwa imejengwa kwa gharama kubwa na fedha zilizotumika ni za ndani.

Ndalichako amesema kuwa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuondoa upungufu wa kero ya Miundombinu iliyokuwa inaikabili DIT kwa muda mrefu ambapo jengo hilo limeigharimu Serikali zaidi ya Bilioni Tisa ambazo ni fedha za ndani.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akizungumza  na watendaji pamoja na wanafunzi wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam(hawapo pichani) wakati wa kuzindua  Jengo la kufundishia la ghorofa 10.

Kwa upande wake Mkuu wa chuo cha DIT Profesa Preskedis Ndomba ameishukuru Serikali kwa uwekezaji huo  uliofanywa na Serikali ambapo amemhakikishia Waziri wa Elimu kuwa  watailinda miundombinu hiyo ili iweze kutumika kwa muda mrefu kwa lengo la kuongeza tija ya kuwepo kwa wataalamu wa fani mbalimbali hapa nchini


Baadhi ya Watumishi wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam –DIT -wakisikiliza kwa makini hotuba ya Prof Joyce Ndalichako wakati wa kuzindua Jengo la kufundishia la ghorofa 10