Jumanne, 2 Septemba 2014

NAIBU WAZIRI AWAAGIZA MAAFISA ELIMU KUWARUDISHA WANAFUNZI WATORO SHULENI


Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mhe.Jenista Mhagama amewaagiza Maafisa Elimu wote nchini kuhakikisha wanafunzi walioacha shule kwa sababu mbalimbali wanarudi shuleni ili kuendelea na masomo.

Naibu Waziri alitoa agizo hilo mwishoni mwa wiki  wakati wa ziara yake mkoani Pwani kukagua miradi inayojengwa na Mpango wa Maendeleo  ya Elimu ya Msingi (MMEM) na Mpango wa Elimu ya Sekondari (MMES). Shule zilizotembelewa ni Nyamisati, Mkamba na WAMA Nakayama zote zikiwa za sekondari na shule ya Msingi ya Mazoezi Vikindu, .

Aliwataka Maafisa Elimu  kufuatilia  sababu za utoro unaojitokeza shuleni na kuandika taarifa juu ya utoro huo na kutafuta njia za kupunguza utoro shuleni. Pia aliwataka Wakaguzi wa Shule wa Kanda pamoja na kazi nzuri wanayoifanya ya kukagua ufundishaji na vigezo, ukaguzi unaofanyika sasa ujikite  katika kujibu hoja ya utoro wa wanafunzi katika shule. Alimuagiza Kaimu Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Shule kutoka Wizarani Bibi Hidaya Mohamed kutopokea ripoti zisizotoa uelekeo wa namna ya kuwarudisha watoto shuleni.
“Katika kila shule ambapo kutakuwa na utoro mkubwa wa wanafunzi Wakaguzi msipokee ripoti ya ukaguzi isiyotoa majibu kwanini wanafunzi katika shule zetu za msingi na sekondari wanaendelea kutoroka na ripoti ionyeshe hatua zilizochukuliwa kuwarudisha shuleni, mipango na mikakati ya kuhakikisha suala hili halijirudii ili kuwa na ubora wa elimu.” Alisema Mhe. Mhagama   

 Kuhusiana na maslahi ya Walimu Mhe. Mhagama alimtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mkuranga kuanzisha dawati la malalamiko litakalowawezesha walimu  kupeleka malalamiko yao  na kuwataka yafanyiwe kazi haraka iwezekanavyo. Alisema kuanzishwa kwa dawati hilo kutawapunguzia adha walimu ya kupoteza muda kufuatilia madai yao na badala yake watatumia muda huo kuwafundisha wanafunzi.
                                      
“Sitaki walimu hawa tunaowaleta huku wapoteze muda mwingi katika majengo ya Halmashauri kufuatilia madai yao kwani hawa ndio watumishi wengi kwenye Halmashauri hakikisheni mnawatengea dawati maalumu la kushughulikia kero zao.”Alisema Mhe.  Mhagama.






Waraka wa elimu na. 4 wa mwaka 2014 kuhusu utayarishaji wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia

Jumatatu, 25 Agosti 2014

Waziri Kawambwa aiasa Jamii Kuchangia Elimu

 Aipongeza Airtel kwa kutoa vitabu

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dkt. Shukuru Kawambwa ameiasa jamii kuchangia kuboresha elimu nchini kwa kutoa misaada mbalimbali itakayosaidia kuimarisha ubora wa elimu inayotolewa katika ngazi mbalimbali za elimu.

Waziri Kawambwa alikuwa akizungumza katika hafla  ya uzinduzi wa Mradi wa Vitabu Airtel Shule Yetu 2014 jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki ambapo wawakilishi wa shule  za Sekondari 30 walipatiwa msaada wa vitabu vya Sayansi na Hisabati na Kampuni hiyo.




Waziri Kawambwa ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo alisema Mradi huu wa Vitabu Airtel Shule Yetu utakuwa wa manufaa makubwa sana si kwa  wanafunzi shuleni tu bali kwa sekta nzima ya Elimu hapa nchini na kwa Taifa kwa ujumla.  

Sote tunatambua kwamba kitu pekee kinachotofautisha nchi zilizoendelea na zinazoendelea siyo utajiri na mali walizonazo bali ni elimu na ujuzi.  Hii ni kwa sababu utajiri na mali havijileti vyenyewe isipokuwa huchochewa na maendeleo mazuri yaliyo jengwa katika msingi mzuri wa ELIMU. Kwa kadri kiwango cha elimu na ujuzi au maarifa kinapokuwa juu katika nchi, ndipo na kiwango cha maendeleo ya nchi yanapozidi kukua katika nchi hiyo,”alisema Dkt. Kawambwa.

Dhamira ya Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2025 (Tanzania Development Vision 2025) ni kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.  Lakini hilo litawezekana tu kwa kupitia elimu.  Yaani kuwa na Taifa lililoelimika; lenye wasomi wanaoweza kubaini na kutatua matatizo ya maendeleo ya nchi yetu.  Na katika wakati huu tulionao, Sayansi na  Tekinolojia vina nafasi  ya  pekee katika maendeleo ya nchi na ustawi wa jamii. 

“Tunaishukuru sana Airtel Tanzania kwa kutuunga mkono katika dhamira ya Serikali yetu ya kuwekeza katika sekta ya elimu nchini.  Airtel imekuwa mstari wa mbele katika kuchangia vitabu pamoja na misaada mbalimbali kwa shule zetu hapa nchini.  Vitabu hivi vilivyochangiwa na Airtel vitasaidia sana katika juhudi za Serikali za kuimarisha ubora wa elimu inayotolewa,” alisema Waziri Kawambwa. 


Hivi sasa kuna uhaba wa walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati katika shule zetu za Sekondari hapa nchini.  Takwimu zinaonesha kwamba hadi mwaka 2013/14 tulikuwa na upungufu wa walimu wa Sayansi na Hisabati 26,998.  Lakini hata kule kwenye walimu wa masomo haya bado kuna tatizo la uhaba wa vitabu.  Lakini kule ambako kuna uhaba wa walimu uwepo wa vitabu hivi utakuwa ni wa msaada sana kwa wanafunzi kuweza hata kujisomea wenyewe.  

Tukio hilo la Kampuni ya Airtel kukabidhi vitabu ni mwendelezo wa mambo mengi ambayo yamekwishafanya katika kuisadia Sekta ya elimu nchini.  Mradi huu ulianza miaka takriban kumi iliyopita na katika kipindi chote hiki mradi umeweza kupeleka vitabu na vifaa vya maabara katika shule mbalimbali na pia kufanya ujenzi na matengenezo katika shule kadhaa hapa nchini.  

Napenda kutumia fursa hii kuwahimiza makampuni mengine  na Taasisi mbalimbali nchini kuiga mfano huu wa Airtel na kusaidia sekta ya elimu ili kujenga taifa lililo bora.  Serikali iko tayari kushirikiana na Taasisi, Makampuni na asasi mbalimbali katika kuendeleza Elimu ya watoto na vijana wetu,” alisema Waziri Kawambwa. 

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Airtel Tanzania Sunil Colaso alisema kampuni yake itaendelea kuisaidia sekta ya elimu ili kuchangia katika juhudi za serikali za kuboresha elimu hapa nchini ambapo hadi hivi sasa shule za sekondari 1,000 zimefaidika kwa kupewa vitabu na kampuni hiyo.

Ijumaa, 22 Agosti 2014


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

 WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI


TANGAZO KWA UMMA
 
MKUTANO KATI YA WIZARA NA WANAFUNZI WANAOSOMA  MASHARIKI MWA UKRAINE HUSUSANI ENEO LA LUGANSK
 

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi inawatangazia wanafunzi wote wa Tanzania wanaosoma katika vyuo vya Lugansk, Ukraine na maeneo mengine  Chini ya Ufadhili wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ambao hivi sasa wako likizo hapa nchini kuwa kutakuwepo na mkutano kujadili, pamoja na mambo mengine, hali ya usalama na hatua za kuchukua kabla ya kurudi Lugansk kuendelea na masomo, mwezi Septemba, 2014.  
 Mkutano huo utafanyika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, siku ya Jumatano, tarehe 3 Septemba, 2014  saa nane mchana.  Aidha, wanafunzi wengine wanaosoma Lugansk kwa udhamini binafsi wanaombwa kuhudhuria ili kushiriki katika mkutano huo.
Imetolewa na:    Katibu Mkuu
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
7 Mtaa wa Magogoni,
Post Code 11479,
S.L.P. 9121,
DAR ES SALAAM.
 
 


 

Jumatano, 20 Agosti 2014

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI



TANGAZO KWA UMMA

MAPENDEKEZO YA MABORESHO YA MICHEPUO NA TAHASUSI ZA KIDATO CHA KWANZA MPAKA CHA NNE NA KIDATO CHA TANO NA SITA

Elimu ya sekondari katika ngazi ya Kidato cha Kwanza hadi cha Nne   imekuwa ikiongozwa na michepuo ya ama ya Sanaa, Sayansi, Ufundi na Biashara. Halika dhalika, masomo ya sekondari Kidato cha Tano na Sita yamekuwa ya kifundishwa kwa kutumia Tahasusi mbalimbali kulinga na mahitaji ya nchi ambazo kwa sasa ni PCM, PCB, PGM, CBG, EGM, CBA, CBG, CBN kwa Sayansi, na  HGL, HGK, HKL, KLF, ECA, HGE kwa Sanaa.

Mafanikio mbalimbali yamepatikana kwa kutumia mfumo huu tangu ulipoanza hadi sasa. Hata hivyo, kutokana na (a) nia ya nchi kupiga hatua zaidi katika maeneo mbalimbali ya maendeleo ya nchi kwa mujibu wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, (b) mabadiliko ya mahitaji ya ulimwengu wa ajira na kazi na (c) kuendelea kukua kwa ugunduzi na ubunifu pamoja na matumizi ya Sayansi na Teknolojia katika maeneo mbalimbali, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imeona kuna umuhimu wa kupitia upya Michepuo na Tahasusi zilizopo ili ufundishaji uweze kwenda na wakati. Michepuo na Tahasusi hizo mpya zinatarajiwa kuanza kutumika katika mwaka wa masomo 2015/2016.

Ili kufanikisha maboresho hayo, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi inakaribisha wadau wote wa Elimu na Mafunzo kutoa mapendekezo ya jinsi gani Michepuo na Tahasusi za elimu ya sekondari ziundwe au kuanzishwa katika madarasa ya kidato cha Kwanza hadi Nne na Tano hadi Sita. Mwisho wa kutuma mapendekezo ni tarehe 31/10/2014. Wadau wote mnahamasishwa kutoa maoni yenu kupitia njia mbalimbali ikiwemo vikao ama kwa kuwasiliana moja kwa moja na wizara. Majumuisho ya mapendekezo ya tawekwa kwenye magazeti na tovuti kwa maoni na hatua za mwisho katika kukamilisha maboresho haya.

Mapendekezo ya Michepuo naTahasusi mpya yatumwe kwa anuani ifuatayo:

Katibu Mkuu,
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi,
7 Mtaa wa Magogoni,
11479 DAR ES SALAAM.




Elimu Bora Inawezekana; Timiza Wajibu Wako


KATIBU MKUU

WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUN DI

Benki ya Dunia Kusaidia Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa Katika Sekta ya Elimu

Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia wamesaini makubaliano ya mkopo wa Shilingi bilioni 203 za Kitanzania (Dola za Marekani milioni 122) kwa ajili ya   kusaidia, kukuza na kuendeleza Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) katika sekta ya Elimu wenye lengo la kuimarisha na kuboresha elimu ya msingi na sekondari.
Makubaliano hayo yalitiwa saini na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Dkt. Servacius Likwelile  kwa niaba ya Serikali na Benki ya Dunia iliwakilishwa na Mkurungezi Mkazi wa Benki hiyo nchini, Philippe Dongie. Makubaliano hayo yamefanyika leo jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi Dkt. Servacius Likwelile  amesema  fedha zilizopatikana zitasaidia Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa katika Elimu kuboresha ubora wa Elimu ya Msingi na Sekondari.
Aidha, Dkt. Likwelile alisema Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa katika Elimu umelenga pamoja na masuala mengine Kuimarisha ufaulu na kuboresha uwazi shuleni kwa kupitia upangaji wa shule kitaifa kwa kuzingatia matokeo ya mitihani kwa shule za msingi na sekondari kwa kuzingatia ubora wa ufaulu na kutekeleza upimaji wa ujuzi wa stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa darasa la pili katika shule zilizochaguliwa.
Mpango huo pia umelenga kutoa  motisha kwa shule zote za Msingi na Sekondari zilizoonyesha maendeleo katika  ufaulu na zilizofanya vizuri ili kuboresha  viwango vya ufaulu na kutoa motisha zisizo za kifedha na kuondoa madai ya muda mrefu ya walimu  wa shule za Msingi na Sekondari ili Kuondoa malalamiko ya walimu hao.

Aidha, Dkt. Likwelile alisema Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa umelenga kuzisaidia shule na kuondoa ugawaji wa rasilimali usiozingatia usawa kwa kutengeneza na kusambaza vifaa vya kujifunzia kwa vitendo kwa shule za Msingi na Sekondari, kuandaa Mafunzo ya KKK kwa walimu wa shule za Msingi, utekelezaji wa  programu ya kujenga uwezo wa walimu na wanafunzi  katika ufundishaji na Ujifunzaji na kuboresha mfumo wa ufuatiliaji wa Ruzuku za Uendeshaji wa Shule.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwakilishi wa Benki ya Dunia aliipongeza Tanzania kwa kupata mkopo huo na kuitaka Serikali kutumia vizuri fedha ilizozipata  kama ilivyokusudiwa ili kuboresha Elimu nchini.
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome, ameishukuru Benki ya Dunia kwa fedha itakayotolewa ambayo itasaidia katika kuhakikisha kuwa utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) katika sekta ya Elimu unafanikiwa.

Aidha, Naibu Katibu Mkuu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Dkt. Deo Mutasiwa alisema Wizara yake imejiandaa kikamilifu kuhakikisha kuwa fedha zitakazopatikana zinatumika kama zilivyokusudiwa na kuhakikisha zinawafikia walengwa.





GPE Programme for Tanzania (LANES) Launched to Regional and District Level Education Officers

The Prime Minister’s Office, Regional Administration and Local Government (PMORALG) conducted a two day working session with all Regional Education Officers (25), District Education officers, Academic Officers and Adult Education Officers from 160 Councils.

The main aim for the session, which was launched by the PMORALG Permanent Secretary, Mr. Jumanne Sagini, was to provide an overview of the LANES programme including roles and responsibilities of officers at different levels of planning and implementation, expected programme results, and Financial Operations.



Prior to the working session, the Ministry of Education and Vocational Training (MOEVT) in collaboration with PMORALG had appointed Focal Persons who would coordinate implementation of the LANES programme at departmental level, one from each Ministry’s department. Following the appointment, a weeklong session was held in Morogoro from 21st to 26th July, concluded by a half-day session with the PMORALG Permanent Secretary.
Meanwhile, the MOEVT is in the final stages of recruiting a National Coordination Team that will facilitate implementation of the LANES Programme. The team will include a National Coordinator, M&E Specialist, Procurement Specialist, Financial Management Specialist and Adult and Non Formal Education Specialist.