Jumanne, 24 Mei 2016




JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA


TAARIFA KWA UMMA
USAJILI WA SHULE ZA AWALI, MSINGI, SEKONDARI NA VITUO VINAVYOTOA ELIMU NJE YA MFUMO RASMI NA SEKONDARI HURIA  

Serikali kupitia Sheria ya Elimu Sura ya 353 inaelekeza  shule zote kusajiliwa kabla ya kusajili wanafunzi. Azma hii ya serikali ni kuhakikisha kuwa kunakuwa na utaratibu madhubuti wa kusimamia Ubora wa Elimu.

Hata hivyo, kumekuwepo na baadhi ya wadau wanaanzisha na kuendesha shule au vituo vinavyotoa elimu nje ya mfumo rasmi  bila kupata Usajili.

Wanafunzi wanaotoka katika shule au vituo hivi hufanya mitihani ya taifa ikiwemo  mtihani wa maarifa (QT)  na mitihani mingine ya Taifa (Kidato cha Nne na Sita)  kama watahiniwa wa kujitegemea. Aidha, baadhi ya wanafunzi hawa huingizwa kwa utaratibu usio rasmi kufanya mitihani ya Darasa la Nne na Darasa la Saba katika shule zilizosajiliwa pasipo kuzingatia mazingira ya mahali waliposomea hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa kushindwa katika mitihani hiyo.

Kwa tangazo hili serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inawataka wamiliki wote wa shule ambazo hazijasajiliwa kuwasilisha maombi yao katika Ofisi za Uthibiti Ubora wa shule Kanda, Wilaya au Idara ya Ithibati ya shule (Usajili) Makao Makuu ya wizara kabla au ifikapo tarehe 30/07/2016. Shule ambazo hazijafikia vigezo vya kusajiliwa, zitafungwa na hazitasajiliwa na Mwenye Shule husika atapaswa kuhamisha wanafunzi waliopo kwa gharama zake. 

Imetolewa na

Dkt. Leonard D. Akwilapo
KAIMU KATIBU MKUU
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA

Jumanne, 12 Aprili 2016

Profesa Ndalichako: Wekeni malengo katika utendaji kazi


Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia  na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako amewataka Watumishi wa Wizara hiyo kujiwekea malengo katika utendaji kazi wao ili waweze kutimiza malengo makubwa ya sekta ya elimu.


Profesa Ndalichako aliyasema hayo wakati  akizungumza na Watumishi wa Wizara hiyo kutoka Makao Makuu katika ukumbi wa Mikutano wa Karimjee ikiwa ni mara ya kwanza kukutana nao tangu alipoteuliwa kuwa Waziri wa Elimu, Sayansi Teknolojia na Ufundi lengo likiwa ni kuwasikiliza lakini pia kujadiliana nao namna bora zaidi ya kuboresha utendaji kazi katika wizara hiyo.

Waziri Ndalichako aliwataka wafanyakazi kufanya kazi  kujituma, kutoa huduma bora kwa wakati kwa kuwa  ni watumishi wa umma na maana ya mtumishi wa umma ni kuwa na  wajibu wa kuwatumikia wananchi ili wapate haki yao kwa wakati kwani haki iliyocheleweshwa ni sawa na haki iliyoptea.

Amewataka watumishi hao kuipende kazi yao,  kwa maana mtumishi anayependa kazi yake  uifahamu kwa undani wake na inakuwa rahisi kuwatyumika wananchi bila ya kuwa na wasiwasi na kujiamini zaidi

 “kila mfanyakazi ni lazima kujivika joho la Wizara kwa maana ya kuijua Wizara vizuri, misingi yake, dira pamoja na sera zinazotuongoza katika utendaji kazi wetu ili tuweze kufikia malengo ya kuinua ubora wa elimu” alisisitza Ndalichako.

Akizungumza kwa niaba ya watumishi Omary Mkali alimshukuru Waziri kwa kukutana na watumishi na kuahidi kufanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri ili kuweze kufikia lengo kwa pamoja la kuinua ubora wa Elimu nchini.


1   Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Profesa Joyce Ndalichako akiingia katika ukumbi wa Karimjee kuongea na wafanyakazi wa Wizara.


1      Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Maimuna Tarishi akimkaribisha Waziri wa Elimu kuongea na wafanyakazi.


1   waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Profesa Joyce Ndalichako akiongea na wafanyakazi wa Wizara.



1     wafanyakazi wa Wizara ya Elimu Sayansi Teknolojia na Ufundi wakimsikiliza Waziri wa Elimu Profesa Joyce Ndalichako.