Jumatatu, 6 Novemba 2017

Makamu wa Rais afungua Kongamano la Elimu, Waziri wa Elimu ashiriki

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Elimu ya Ufundi ndiyo nguzo muhimu ya kufikia ajenda ya serikali ya kuwa Tanzania ya viwanda na kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akifungua kongamano la kimataifa la wadau wa Elimu ya Ufundi na mafunzo jijini Dar es salaam, na kusisitiza kuwa dira ya Maendeleo ya 2025 imeipa Elimu kipaumbele cha juu kwa kuwa ndiyo kitovu katika kuleta mabadiliko ya kiuchumi katika jamii.

Makamu wa Rais amesema kuwa serikali kipitia baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi litaendelea kusimamia na kuratibu utoaji wa mafunzo katika taasisi za Elimu ya Ufundi ili Taifa liwe na wataalamu wa kutosha na wenye weledi katika fani mbalimbali kwa Maendeleo ya Taifa.

Viongozi wengine walioshiriki mkutano huo wa siku tatu ni pamoja na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa. Joyce Ndalichako, Naibu Katibu Mkuu Dkt. Avemaria Semakafu, Wakuu wa Taasisi  na wadau mbalimbali.


Kauli mbiu katika mkutano huo ni Wekeza katika Elimu ya Ufundi na Mafunzo kwa Tanzania kuwa ya uchumi wa viwanda.



Alhamisi, 2 Novemba 2017

Ndalichako: Tanzania imedhamiria kufikia malengo ya maendeleo endeleve

Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imedhamiria kufikia malengo ya Maendeleo endelevu kwa kuhakikisha inatimiza malengo yaliyowekwa ikiwa ni pamoja na kutoa Elimu bure kuanzia Elimu ya awali mpaka kidato cha Nne, uboreshaji wa miundombinu ya kujifunzia na kufundishia, uboreshaji wa vyuo vya ualimu pamoja na kuboresha mazingira kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

Hayo yameelezwa jana na Waziri wa Elimu , Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako wakati akihutubia mkutano mkuu wa 39 wa UNESCO, Mjini Paris nchini Ufaransa, ambapo katika kufikia malengo hayo walimu 68,799 tayari wamepatiwa mafunzo maalumu ya mtaala ulioboreshwa, KKK.

Waziri Ndalichako aliwaeleza wajumbe wa mkutano huo kuwa suala la wanafunzi wenye mahitaji maalumu bado linahitaji kuangaliwa kwa mapana zaidi hivyo kuziomba nchi wanachama kutoa kipaumbele katika kuandaa  mazingira ambayo yatakuwa rafiki kwa wanafunzi wa kike na wale wa kiume ambao wana mahitaji maalumu.

Waziri Ndalichako Pia alieleza kuwa tayari vifaa vya maabara na vitabu kwa shule za Sekondari limesambazwa kwa nchi nzima ili kutilia mkazo masomo ya Sayansi.


Waziri Ndalichako pia tayari ameshiriki mikutano mbalimbali inayohusu tume za UNESCO zilizoanza oktoba 30, 2017 ambapo amepokea taarifa zinazohusu fursa mbalimbali za namna ya kupata misaada ya maendeleo kutoka UNESCO na washirika wake wa kimataifa.

Pia kupitia mkutano huo Mkuu viongozi wa Tume za Taifa za  UNESCO  duniani wanapata fursa ya kukutana na kubadilishana uzoefu na kupeana mbinu mbalimbali za kuandika kazi miradi kwa maslahi ya nchi zao.

Mkutano huo mkuu wa 39 wa UNESCO ulianza Oktoba 30, 2017 ambapo  Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni -UNESCO -IRINA BOKOVA alisema Tume hiyo  imekuwa na mafanikio kutokana na  ushirikiano inaoupata kutoka kwa nchi wanachama.

Katika mkutano huo waziri wa Elimu Profesa Ndalichako ameambatana na Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa Balozi Samwel Shelukindo, Mkurugenzi wa Sera na Mipango Petro Lyatuu kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya UNESCO  Dkt. Moshi Kimizi.

Mkutano huo Mkuu hufanyika kila baada ya miaka miwili na unahusisha nchi zote wanachama za UNESCO.




Jumatano, 1 Novemba 2017

Waziri kuwasilisha msimamo wa Tanzania kwa UNESCO leo


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce   Ndalichako leo anawasilisha taarifa  yenye msimamo wa Serikali ya  Jamuhuri ya muungano wa Tanzania katika mkutano mkuu wa 39 wa shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi, Utamaduni, habari na Mawasiliano -UNESCO.

 Waziri Ndalichako pia tayari ameshiriki mikutano mbalimbali inayohusu tume za UNESCO zilizoanza oktoba 30, 2017 ambapo amepokea taarifa mbalimbali zinazohusu fursa mbalimbali za namna ya kupata misaada ya maendeleo kutoka UNESCO na washirika wake wa kimataifa, pia viongozi wa Tume za Taifa za  UNESCO  duniani kubadilishana uzoefu na kupeana mbinu mbalimbali za kuandika kazi miradi kwa maslahi ya nchi zao.

Mkutano huo mkuu wa 39 wa UNESCO ulianza juzi Oktoba 30, 2017 ambapo  Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni -UNESCO -IRINA BOKOVA alisema Tume hiyo   ina nguvu kwa sababu ya ushirikiano inaoupata kutoka kwa nchi wanachama.

Katika mkutano huo waziri wa Elimu Profesa Ndalichako ameambatana na Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa Balozi Samwel Shelukindo, Mkurugenzi wa Sera na Mipango Petro Lyatuu kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya UNESCO  Dkt. Moshi Kimizi.
Mkutano huo Mkuu hufanyika kila baada ya miaka miwili na unahusisha nchi zote wanachama za UNESCO.



Jumanne, 31 Oktoba 2017

TEWW yatakiwa kutekeleza  majukumu yake

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Ole Nasha ameitaka Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima kuendelea kutekeleza majukumu yake ya kimuundo badala ya kufikiria kufanya miradi ambayo imekuwa ikiwaondoa kwenye mwelekeo wa malengo ya uanzishwaji wa Taasisi hiyo.
Naibu Waziri Ole Nasha ametoa wito huo leo jijini Dar es Salaam alipotembelea Taasisi hiyo  ikiwa ni muendelezo wa ziara zake za kuzitambua taasisi zilizo chini ya wizara pamoja na utendaji wa majukumu yake.
Akiwa katika Taasisi hiyo amesema nchi bado inaihitaji Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima pamoja na aina ya elimu ambayo inatolewa na taasisi hiyo, hivyo ameitaka taasisi hiyo  kutekeleza majukumu yake iendane na hali halisi ya mazingira ya elimu.
Ole Nasha amesema ukiangalia utekelezaji wa miradi  hiyo inabaki kuitwa elimu ya watu wazima lakini namna inavyoendeshwa haziakisi uhalisia wake na badala yake zinabaki kuwa kama mifumo mingine ya utoaji wa elimu ya mfumo rasmi.

Naibu Waziri Ole Nasha akiwa katika taasisi hiyo amepata fursa ya kutembelea chumba cha Uchapaji vitabu  majarida, Karakana, Maktaba na idara ya Elimu ya masafa na Studio za kuandaa vipindi vya kuelimisha umma vya Elimu ya Watu Wazima.
Aidha, Naibu Waziri ametembelea Tume ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia Elimu, Habari, utamaduni  ya UNESCO na kuwataka kuitisha kikao cha wadau wanaohusika na Tume hiyo ili kuzungumzia changamoto za kimfumo na muundo zinazoikabili taasisi hiyo.






Naibu Waziri Ole Nasha atoa maagizo kwa Bodi ya Mikopo na Tume ya Vyuo Vikuu


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha amezitaka Tume ya Vyuo Vikuu na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kuhakikisha wanakamilisha taratibu za udahili na utoaji mikopo kwa wakati ili wanafunzi wanaojiunga na masomo ya elimu ya juu waanze mara moja bila kuchelewa.

Naibu waziri Ole Nasha ameyasema hayo jijini Dar es Salaam alipofanya ziara katika Taasisi hizo ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu kuteuliwa ili kujionea utendaji kazi wa taasisi hizo.

Naibu Waziri amesema serikali imeidhinisha takribani shilingi bilioni 427 kwa ajili ya wanafunzi 122,000 wanaoanza na kuendelea na masomo ya elimu ya juu kwa mwaka 2017/18.
“lengo la Serikali ni kuona wanafunzi wote wanaanza masomo bila kuchelewa na katika kutekeleza hilo tayari serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 147 kwa Bodi ya Mikopo kwa ajili ya robo ya kwanza ya kuwawezesha wanafunzi wenye sifa na vigezo wanaoanza na wale wanaoendelea masomo yao hivyo hatutegemei kusikia malalamiko yoyote kutoka kwa wanafunzi wanaostahili mikopo hiyo” alisisitiza Ole nasha

Pia ameitaka Bodi kutoa taarifa kwa umma majina yote ya wadaiwa sugu wa mikopo ambao mpaka sasa hawajaonyesha utayari wa kurejesha mikopo hiyo kwani lengo la serikali ni kuona bodi ya mikopo inaanza kujiendesha yenyewe badala ya kutegemea ruzuku kutoka serikalini.
Katika hatua nyingine Mhe. Ole Nasha ameitaka Tume ya Vyuo Vikuu nchini kuhakikisha mfumo unaotumika kudahili wanafunzi  kutochelewesha wanafunzi kupata mikopo kwa wakati ili kuwawezesha kujiunga  na vyuo mapema.

Ole Nasha ameitaka Taasisi hiyo kushirikiana na wanafunzi kwa karibu katika kipindi hiki cha udahili ili kufikia Novemba 2 mwaka huu zoezi hili la udahili liwe limekamilika.




Waziri Ndalichako ashiriki mkutano wa UNESCO, nchini Ufaransa.


Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni -UNESCO -IRINA BOKOVA amesema Tume hiyo   ina nguvu kwa sababu ya ushirikiano inaoupata kutoka kwa nchi wanachama, hivyo ameziomba  nchi hizo kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano ili kufikia malengo waliyojiwekea.

Bukova ameyasema hayo hii leo wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa 39 wa UNESCO unaohusiha nchi wanachama duniani kote ambapo amesisitiza pia suala la kudumisha amani, upendo miongoni mwa nchi hizo.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako pamoja na Balozi wa Tanzani nchini Ufaransa balozi Samweli Shelukindo wameshiriki mkutano huo.


Alhamisi, 19 Oktoba 2017

Mradi wa kuwawezesha watoto wa kitanzania kupata elimu wazinduliwa


Kaimu Mkurugenzi mafunzo ya Ualimu Basiliana Mrimi  amezindua mradi wa shilingi milioni 500 utakaosaidia kuimarisha Ufundishaji na ujifunzaji kwenye Chuo cha Ualimu, Patandi kilichopo mkoani Arusha.

Akizundua Mradi huo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Mrimi amesema  mradi huo utasaidia Kupima macho watoto wa shule za msingi na kuwapatia vifaa wanafunzi wenye uoni hafifu, Kutoa mafunzo kazini kwa wakufunzi 12 na walimu 4 wa shule za msingi zilizopo kwenye mradi.

Pia mradi huo utasaidia Kusomesha mkufunzi 1 kwa ngazi ya Shahada ya Uzamivu (PhD), Kusomesha wakufunzi 4 kwa ngazi ya Shahada ya Uzamili (Masters) na kuwa mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano wa Tanzania na Norway.