Ijumaa, 10 Novemba 2017


Kauli ya Serikali kuhusu udahili na utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu mwaka 2017/18 iliyotolewa na Prof.  Joyce Ndalichako (MB) - Bungeni, Dodoma; Novemba 09, 201

#Udahili wa wanafunzi walioomba kujiunga na vyuo vya elimu ya juu ulifanyika kwa awamu tatu na ulihusisha jumla ya vyuo na taasisi za elimu ya juu 67.
#Katika awamu ya kwanza majina 77,756 yakipokelewa TCU, wanafunzi 44,627 walichaguliwa.

#Baada ya uhakiki waombaji 36,831 waliidhinishwa na kujiunga na shahada ya kwanza. Waombaji 7,796 walikuwa na kasoro mbalimbali kwenye taarifa zao hivyo kukosa sifa ya kujiunga na vyuo.

#Awamu ya pili ililenga waombaji waliokosa udahili awamu ya kwanza ambapo jumla ya waombaji 19,488 walijitokeza na walioidhinishwa kuwa na sifa za kujiunga ni 9,525.
#Awamu ya tatu ilikuwa kwa ajili ya kutoa nafasi ya mwisho kwa wanafunzi waliokosa vyuo ambapo jumla ya waombaji 7,418 waliidhinishwa kujiunga na vyuo.

Hadi kukamilika kwa awamu ya  tatu waombaji 63,737  waliidhinishwa kujiunga na vyuo  na  waombaji 28,466 kati yao walikuwa wamechaguliwa zaidi ya chuo kimoja.

#Serikali katika mwaka wa fedha 2017/18 imepanga kutumia Shilingi Bilioni 427.54 kugharamia mikopo kwa ajili ya wanafunzi wenye uhitaji na waliodahiliwa na vyuo vya elimu juu hapa nchini.

#Mikopo hii ni kwa ajili ya wanafunzi 122,623 ambapo wanafunzi 30,000 ni wa mwaka wa kwanza na wanafunzi 92,623 ni wanaoendelea na masoma.

#Katika robo ya kwanza ya mwaka huu wa masomo, Wizara imepokea Shilingi Bilioni 147.06 kwa ajili ya ada za wanafunzi na kwa ajili ya kugharamia chakula, malazi, vitabu, viandikia na mahitaji maalum ya masomo.

#Utoaji wa mikopo umezingatia vigezo vilivyowekwa ambavyo ni ulemavu, uyatima na uhitaji hasa katika programu za kipaumbele.

*Changamoto Zilizojitokeza Katika Utoaji wa Mikopo. 
                           
#Baadhi ya waombaji kutozingatia mwongozo na maelekezo ya uombaji kwa kutoambatanisha nyaraka muhimu zinazothibisha uhitaji wao.

#Baadhi ya wanafunzi waliopangiwa mikopo kuamua kuripoti kwenye vyuo tofauti walivyothibitisha udahili wa awali ambapo mikopo yao  imelipwa kwenye vyuo tofauti na waliporipoti.

#Dhana ya mikopo ni ya elimu ya juu ni kwa ajili ya wanafunzi wote na hivyo hata wanafunzi wasio na sifa kulingana na vigezo kutaka wapate mikopo.

*Hatua Zilizochukuliwa Kukabiliana na Changamoto Zilizojitokeza. 

#Kupokea taarifa na nyaraka za ziada na kusahihisha taarifa za maombi kutoka kwa wahitaji walioshindwa kukamilisha taarifa husika wakati wa kipindi cha maombi.

#Kukamilisha utaratibu wa kufungua dirisha la rufaa ili baadhi ya wanafunzi watakaokuwa hawajapangiwa mikopi kufikia tarehe 10/11/2017 waweze kuwasilisha rufaa zao ili wale watakaofanikiwa kwenye rufaa wapangiwe mikopo kabla ya tarehe 30/11/2017.

#Kupokea taarifa za usajili za wanafunzi wenye mikopo ili wale ambao mikopo iko vyuo tofauti ihamishwe kwenye vyuo walivyoripoti.

#Serikali imeshawaagiza wakuu wote wa vyuo vya Elimu ya Juu kuacha urasimu katika utoaji wa fedha kwa wanufaika wa mikopo.

#Inasikitisha sana kuona kuwa baadhi ya vyuo vinadiriki hata kuwakataa wanafunzi waliowadahili wao wenyewe.

#Nampongeza Rais Dkt. Magufuli kwani haijawahi kutokea, fedha kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu zikatolewa mwezi mzima kabla ya vyuo kufunguliwa 

Jumatano, 8 Novemba 2017

Katibu Mkuu ataka fedha za tafiti zitumike kama zilivyopangwa.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt Leornard Akwilapo amesema Serikali itahakikisha fedha zilizotolewa  na Serikali ya Sweden kupitia Shirika la Kimataifa la misaada la nchi hiyo (SIDA) zinatumika kama zilivyokusudiwa kwa ajili ya masuala ya tafiti na kuhakikisha matokeo tarajiwa yanapatikana kikamilifu.

Dkt. Akwilapo ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya miaka 40 ya ushirikiano katika tafiti kati ya Tanzania na Sweden yanayofanyika jijini Dar es Salaam ambapo nchi ya Sweden imetoa zaidi ya bilioni 78 kwa ajili ya kuendeleza masuala ya tafiti kwa kipindi cha 2015 hadi 2020.

Dkt Akwilapo amezitaja taasisi zilizonufaika na zinazoendelea kunufaika na ushirikiano huo kuwa ni Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Chuo Kikuu Ardhi (ARU), Chuo Kikuu cha tiba na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambao wamekuwa wakifanya tafiti katika masuala mbalimbali ya kitaaluma na kijamii. 


Ushirikiano kati ya Tanzania na Sweden umewezesha Tanzania kupata wataalam 455 katika ngazi ya uzamili na 82 katika ngazi ya uzamivu kwa mwaka 1998 hadi 2009 na mpaka sasa zaidi ya wanafunzi 200 wanaendelea na masomo ya katika ngazi uzamili na wengine 80 katika ngazi uzamivu kutokana na ushirikiano Kati ya nchi hizo mbili.




Jumanne, 7 Novemba 2017

Naibu Katibu Mkuu Dkt. Semakafu asisitiza umuhimu wa kuboresha Sera na Programu za watot

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Avemaria Semakafu amesema zaidi ya watoto milioni mia mbili duniani hawafikii malengo kutokana na umasikini  na utapiamlo wanaoupata wakiwa katika umri mdogo.

 Dkt. Semakafu ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa pili wa kimataifa wa kujadili maendeleo ya makuzi ya watoto na kusisitiza kuwa kupitia mkutano huo wadau wataweza kuboresha sera na kuwa na programu ambazo zitasaidia katika makuuzi ya watoto wa kitanzania.

Kupitia mkutano huo wadau watapata fursa ya kuwa na uelewa wa pamoja, kushirikisha uzoefu kati ya nchi moja na nyingine pamoja na kushawishi wadau kuweka nguvu ya pamoja kwa ajili ya watoto.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Chuo Kikuu Cha Aghakan Tanzania na Taasisi ya IHD Profesa. Kofi Marfo amesema kuwa maendeleo na makuzi ya watoto hutegemea  wazazi, familia na  jamii  kwa ujumla amesisitiza pia suala la  lishe bora kwa watoto, kukua na kuandaa vituo vya afya na hospitali kwa ajili ya upatikanaji wa huduma zilizo bora.

Mkutano huo wa siku tatu umeanza leo na umehusisha nchi ishirini na tano ambapo Tanzania mwenyeji wa Mkutano huo.





Jumatatu, 6 Novemba 2017

Makamu wa Rais afungua Kongamano la Elimu, Waziri wa Elimu ashiriki

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Elimu ya Ufundi ndiyo nguzo muhimu ya kufikia ajenda ya serikali ya kuwa Tanzania ya viwanda na kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akifungua kongamano la kimataifa la wadau wa Elimu ya Ufundi na mafunzo jijini Dar es salaam, na kusisitiza kuwa dira ya Maendeleo ya 2025 imeipa Elimu kipaumbele cha juu kwa kuwa ndiyo kitovu katika kuleta mabadiliko ya kiuchumi katika jamii.

Makamu wa Rais amesema kuwa serikali kipitia baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi litaendelea kusimamia na kuratibu utoaji wa mafunzo katika taasisi za Elimu ya Ufundi ili Taifa liwe na wataalamu wa kutosha na wenye weledi katika fani mbalimbali kwa Maendeleo ya Taifa.

Viongozi wengine walioshiriki mkutano huo wa siku tatu ni pamoja na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa. Joyce Ndalichako, Naibu Katibu Mkuu Dkt. Avemaria Semakafu, Wakuu wa Taasisi  na wadau mbalimbali.


Kauli mbiu katika mkutano huo ni Wekeza katika Elimu ya Ufundi na Mafunzo kwa Tanzania kuwa ya uchumi wa viwanda.



Alhamisi, 2 Novemba 2017

Ndalichako: Tanzania imedhamiria kufikia malengo ya maendeleo endeleve

Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imedhamiria kufikia malengo ya Maendeleo endelevu kwa kuhakikisha inatimiza malengo yaliyowekwa ikiwa ni pamoja na kutoa Elimu bure kuanzia Elimu ya awali mpaka kidato cha Nne, uboreshaji wa miundombinu ya kujifunzia na kufundishia, uboreshaji wa vyuo vya ualimu pamoja na kuboresha mazingira kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

Hayo yameelezwa jana na Waziri wa Elimu , Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako wakati akihutubia mkutano mkuu wa 39 wa UNESCO, Mjini Paris nchini Ufaransa, ambapo katika kufikia malengo hayo walimu 68,799 tayari wamepatiwa mafunzo maalumu ya mtaala ulioboreshwa, KKK.

Waziri Ndalichako aliwaeleza wajumbe wa mkutano huo kuwa suala la wanafunzi wenye mahitaji maalumu bado linahitaji kuangaliwa kwa mapana zaidi hivyo kuziomba nchi wanachama kutoa kipaumbele katika kuandaa  mazingira ambayo yatakuwa rafiki kwa wanafunzi wa kike na wale wa kiume ambao wana mahitaji maalumu.

Waziri Ndalichako Pia alieleza kuwa tayari vifaa vya maabara na vitabu kwa shule za Sekondari limesambazwa kwa nchi nzima ili kutilia mkazo masomo ya Sayansi.


Waziri Ndalichako pia tayari ameshiriki mikutano mbalimbali inayohusu tume za UNESCO zilizoanza oktoba 30, 2017 ambapo amepokea taarifa zinazohusu fursa mbalimbali za namna ya kupata misaada ya maendeleo kutoka UNESCO na washirika wake wa kimataifa.

Pia kupitia mkutano huo Mkuu viongozi wa Tume za Taifa za  UNESCO  duniani wanapata fursa ya kukutana na kubadilishana uzoefu na kupeana mbinu mbalimbali za kuandika kazi miradi kwa maslahi ya nchi zao.

Mkutano huo mkuu wa 39 wa UNESCO ulianza Oktoba 30, 2017 ambapo  Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni -UNESCO -IRINA BOKOVA alisema Tume hiyo  imekuwa na mafanikio kutokana na  ushirikiano inaoupata kutoka kwa nchi wanachama.

Katika mkutano huo waziri wa Elimu Profesa Ndalichako ameambatana na Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa Balozi Samwel Shelukindo, Mkurugenzi wa Sera na Mipango Petro Lyatuu kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya UNESCO  Dkt. Moshi Kimizi.

Mkutano huo Mkuu hufanyika kila baada ya miaka miwili na unahusisha nchi zote wanachama za UNESCO.




Jumatano, 1 Novemba 2017

Waziri kuwasilisha msimamo wa Tanzania kwa UNESCO leo


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce   Ndalichako leo anawasilisha taarifa  yenye msimamo wa Serikali ya  Jamuhuri ya muungano wa Tanzania katika mkutano mkuu wa 39 wa shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi, Utamaduni, habari na Mawasiliano -UNESCO.

 Waziri Ndalichako pia tayari ameshiriki mikutano mbalimbali inayohusu tume za UNESCO zilizoanza oktoba 30, 2017 ambapo amepokea taarifa mbalimbali zinazohusu fursa mbalimbali za namna ya kupata misaada ya maendeleo kutoka UNESCO na washirika wake wa kimataifa, pia viongozi wa Tume za Taifa za  UNESCO  duniani kubadilishana uzoefu na kupeana mbinu mbalimbali za kuandika kazi miradi kwa maslahi ya nchi zao.

Mkutano huo mkuu wa 39 wa UNESCO ulianza juzi Oktoba 30, 2017 ambapo  Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni -UNESCO -IRINA BOKOVA alisema Tume hiyo   ina nguvu kwa sababu ya ushirikiano inaoupata kutoka kwa nchi wanachama.

Katika mkutano huo waziri wa Elimu Profesa Ndalichako ameambatana na Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa Balozi Samwel Shelukindo, Mkurugenzi wa Sera na Mipango Petro Lyatuu kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya UNESCO  Dkt. Moshi Kimizi.
Mkutano huo Mkuu hufanyika kila baada ya miaka miwili na unahusisha nchi zote wanachama za UNESCO.