Alhamisi, 28 Desemba 2017

Waziri Ndalichako afungua vyumba vya madarasa Simiyu

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,  Profesa Joyce Ndalichako amesema serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya kujifunzia na ile ya kufundishia lengo likiwa ni kuhakikisha Elimu bora inatolewa.

Waziri Ndalichako ameyasema hayo wakati akifungua vyumba viwili vya madarasa vilivyojengwa kupitia Mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo (P4R)  katika Shule ya Msingi Mahembe iliyopo Kijiji cha Mahembe kata ya Sawida mkoani Simiyu

Kupitia ziara hiyo  Profesa Ndalichako pia alizungumza na wananchi wa Kijiji cha Habiya kilichopo  Wilaya ya Itilima na kuwataka wazazi kuhakikisha watoto wote waliofika umri wa kwenda shule wanakwenda.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Itilima, Mkoani Simiyu Njalu Silanga amepongeza jitihada zinazofanywa na Serikali za kuboresha miundombinu huku akiwataka wananchi wa Jimbo lake kuitunza miundombinu hiyo kwa faida ya kijiji  hicho.



Alhamisi, 21 Desemba 2017


Wizara ya Elimu yaendeleza ujenzi wa Sekondari ya kumbukumbu ya Sokoine

Wizari ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetoa kiasi cha shilingi bilioni 1.7 kwa ajili ya kuendeleza  ujenzi wa shule ya sekondari ya kumbukumbu ya hayati Edward Moringe Sokoine inayonengwa Wilayani Mvomero mkoani Morogoro.

Akizungumza leo wakati alipofanya ziara ya kukagua miradi inayotekelezwa na Wizara hiyo katika mkoa wa Morogoro Waziri Ndalichako amepongeza juhudi zinazofanywa na Halmashauri ya Mvomero kwa kuhakikisha inasimamia fedha zinazotolewa na Serikali kuwa zinatumika kama zilivyokusudiwa.

"Nawapongeza kwa kazi nzuri, ni jambo jema la kumuenzi hayati  Edward Moringe Sokoine kwa kuhakikisha tumekamilisha ujenzi huo ili wanafunzi waweze kuanza masomo kama inavyotarajiwa, huu ni mfano basi ni vyema na halmashauri nyingine ziige hiki ambacho Mvomero imefanya"alisema Waziri Ndalichako.

Profesa Ndalichako amesema uwepo wa shule hiyo ni kumbukumbu na pia ni kielelezo kuwa Hayati Sokoine amelitumikia Taifa hili kwa Uadilifu.

Katika ziara hiyo Waziri ametembelea kituo cha Maendeleo DAKAWA kwa lengo la kujionea hali ya Miundombinu katika shule ya Sekondari Dakawa, Kituo cha Ufundi Stadi VETA na Chuo cha Ualimu.

Pia  ametembelea Chuo cha Ufundi Stadi  VETA kilichopo Kihonda na kile kilichopo Morogoro mjini ambapo ameiagiza BODI ya  VETA kuangalia upya sifa za wakuu wa vyuo waliopo hivi sasa ili kuleta tija na ufanisi katika kazi kwani  waliopo hivi sasa hawakidhi vigezo pia hawaendani na kasi ya serikali ya awamu ya Tano.





Jumatatu, 18 Desemba 2017

Waziri Ndalichako aongoza Harambee ya kuchangia ujenzi wa mabweni shule ya Sekondari Sovi

Zaidi ya shilingi milioni Mia moja zimepatikana wakati wa Harambee ya Ujenzi wa mabweni ya  wasichana katika shule ya sekondari Sovi iliyopo  kata ya Mtwango Mkoani Njombe.

fedha hizo zimepatikana wakati wa  harambee iliyoongozwa na Waziri wa Elimu, Sayasni na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako  mwishoni mwa wiki  mkoani Njombe ambapo amewataka  vijana kuwa wazalendo, pamoja na kuhakikisha wanasoma kwa bidii kwa maslahi ya Taifa.

Waziri Ndalichako pia  amewasihi vijana kuhakikisha wanaipenda nchi yao pamoja na kujiepusha na makundi ambayo hayana tija kama vile utumiaji wa dawa za kulevya, kujiingiza kwenye makundi ya uhalifu, na utumiaji wa pombe vitendo ambavyo havina faida kwa maisha yao ya sasa na ya baadae.

Waziri Ndalichako amesema kuwepo kwa mabweni kutawapunguzia wanafunzi kutembea umbali mrefu, kuwaepusha na vishawishi vya barabarani wakati wa kwenda na kurudi shuleni  na hivyo watatumia muda wao mwingi kwenye kusoma.

Ndalichako amesema kazi ya Serikali ni kuboresha miundombinu, na kuhakikisha mahitaji muhimu ya wanafunzi yanapatikana shuleni hivyo wanafunzi nao lazima watimize wajibu wao kwa kuhakikisha wanasoma na kufaulu katika mitihani yao.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka amesema mkoa wake unatambua jitihada zinazofanywa na Serikali ya awamu ya Tano katika kutatua changamoto mbalimbali katika sekta ya Elimu.


Amesema katika mkoa wake kati ya Shule Kumi za sekondari za umma shule Tisa zina mabweni lengo likiwa ni kuondoa changamoto ya upatikanaji wa mimba kwa wanafunzi, pamoja na kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wanaomaliza kidato cha Nne.




Ijumaa, 15 Desemba 2017

Ole Nasha aitaka Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima kuandaa Wataalamu katika fani za ufundishaji na ujifunzaji

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha ameiagiza Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima kurejea jukumu lake la msingi la kuwaandaa wataalamu katika fani za Elimu ya Watu Wazima na Maendeleo ya Jamii.
Naibu Waziri ametoa agizo hilo katika mahafali ya 53 ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima yaliyofanyika katika viwanja vya Taasisi hiyo jijini Dar es Salaam, ambapo amesema kwa kufanya hivyo kutasaidia kutatua  changamoto za ufundishaji na ujifunzaji wa stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesaba  (KKK) kwa vijana na watu wazima.

Naibu Waziri Ole Nasha amesema Wizara tayari ilishatoa Mwongozo wa shule za Msingi na Sekondari  kutumika kama vituo vya kutolea Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo rasmi, wakati utaratibu wa kuvitumia Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi FDC ukiwa unaendelea.

Mheshimiwa Ole Nasha amesema serikali kwa kushirikiana na wadau imeendelea kutekeleza Mipango mbalimbali ambayo inawawezesha vijana na watu wazima waliokosa fursa katika Mfumo Rasmi wa Elimu kujiendeleza kielimu na kumudu changamoto za maisha.

Naibu Waziri Ole Nasha amewataka wahitimu kwenda kufanya kazi kwa weledi katika vituo watakavyopangiwa ili kusaidia juhudi za Serikali za kupambana na adui ujinga.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Dkt. Fidelice Mafumiko amesema Taasisi i naendelea kuongeza fursa zaidi katika utoaji Elimu kwa kupitia programu za mafunzo kwa kutumia njia ya ujifunzaji huria na masafa kwa ngazi ya Stashahada.


Dtk. Mafumiko amasema hadi sasa Taasisi imeongeza vituo  vya mafunzo vya Elimu ya Watu Wazima  kutoka vituo 13 hadi kufikia 21 katika mikoa13.



Alhamisi, 14 Desemba 2017

Rais Magufuli asema Serikali iko tayari kulipa madai halali ya Walimu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli amesema Serikali iko tayari kulipa madai  ya walimu ambayo wanaidai serikali endapo madeni hayo yatakuwa yamehakikiwa na kuthibitishwa kuwa ni madai halali.

Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano wa Chama cha Walimu ambao unafanyika katika ukumbi wa Chimwaga mkoani Dodoma Rais amesema anatambua sana shida za walimu  na kuwa serikali yake iko tayari kupatia ufumbuzi changamoto hizo.

Rais Magufuli amesema mpaka sasa tayari Serikali imetumia zaidi ya shilingi bilioni 56 kulipa madeni ya walimu na  kuwa kila mwezi  serikali imekuwa ikituma ruzuku kiasi cha shilingi bilioni 18 mpaka bilioni 23 kwa ajili ya   kuwalipa walimu.

Rais Magufuli amewataka walimu na wanafunzi  kukubali kufanya kazi katika vituo wanavyopangiwa mara wanapohitimu, Pia amesisitizia suala la mwalimu kutokuhamishwa kituo cha kazi bila kulipwa fedha yake yote na hivyo amewataka walimu kuzingatia suala hilo.

Akizungumza kabla ya Kumkaribisha mgeni rasmi Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Ndalichako amewapongeza walimu kwa umoja na mshikamano ambao wamekuwa wakiuonyesha kupitia chama hicho cha walimu.

Chama hicho cha walimu kupitia Risala yao imeeleza kuwa inatambua jitihada zinazofanywa na Serikali ya awamu ya Tano katika kutatua changamoto mbalimbali zilizopo katika sekta ya Elimu.

Katika mkutano Rais Magufuli aliwaongoza viongozi wengine kuchangisha  fedha kiasi cha shilingi milioni 60 ambazo zitagawanywa kwa walimu zaidi ya 1000 ambao wanashiriki mkutano huo.





Alhamisi, 7 Desemba 2017

Finland yaahidi kuendelea kusaidia Sekta ya Elimu

Jamhuri ya Watu wa Finland imesema itaendelea kuisaidia Tanzania katika sekta ya Elimu kwenye eneo la ubunifu ili kuhakikisha vijana wanakuwa wabunifu ili kuweza kujiajiri pindi wanapomaliza masomo.

Kauli hiyo imetolewa na Balozi wa Jamhuri ya watu wa Finland nchini Tanzania Pekka Hukka wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako katika ofisi ndogo za Wizara zilizopo jijini Dar es Saalam kuhusiana na namna bora ya utekelezaji wa awamu ya pili ya programme ya ubunifu inayotekelezwa na Tume ya Taifa  ya Sayansi na Teknolojia(COSTECH).

Waziri Ndalichako amesema atahakikisha Wizara yake inasimamia kwa karibu utekelezaji wa programu hiyo ili kuhakikisha malengo ya programu yanafikiwa.
Waziri Ndalichako amesema Serikali inatambua msaada  ambao umekuwa ukitolewa na Finland katika sekta mbalimbali nchini  ikiwemo sekta ya  Elimu na kuahidi kuwa  fedha zitakazotolewa zitatumika kama zilivyokusudiwa.


Programu hiyo ya miaka mitano  inatarajiwa kuanza 2018 na kukamilika 2022.